Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeziagiza bodi na kamati za shule
nchini kupitia upya mikataba iliyoingiwa kati ya shule na
wafanyabiashara waliojenga maduka, baa zikamo nyumba za kulala wageni
kwenye uzio wa shule.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya
Elimu, Kassim Majaliwa, alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza katika
kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One Sterio.
Majaliwa alisema kuruhusu ujenzi wa baa, maduka na nyumba za kulala
wageni kwenye uzio wa shule kunaleta athari kwa wanafunzi kimasomo,
hivyo kamati za shule na bodi ziangalie upya mikataba hiyo ikiwezekana
isitishwe.
Alisema serikali imeshatoa waraka kwa wakurugenzi wa halmashauri
kusimamia suala hilo na kwamba mkurugenzi atakayeshindwa kufanya hivyo
atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Tumeshatoa waraka kwa wakurugenzi wasimamie suala la upitiaji wa
mikataba hiyo na kwa mkurugenzi atakayeshindwa kufanya hivyo itabidi
tumchukulie hatua kama atakuwa ameshindwa kuwajibisha viongozi wa shule
husika,” alisema Majaliwa.
Kwa muda mrefu kumekuwa na tatizo la baadhi ya viongozi wa shule kwa
kushirikiana na bodi na kamati za shule kuingia mikataba na
wafanyabiashara ambao wanajenga maduka na baa katika uzio wa shule kwa
lengo la kujipatia fedha bila kujali athari wanazoweza kupata wanafunzi.
No comments:
Post a Comment