Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imepuuza malalamiko ya baadhi ya wananchi
na vyama vya siasa kuhusu dosari zilizojitokeza kwenye uchaguzi wa
mabaraza ya Katiba na imeamua kwamba inaendelea na mchakato kama
kawaida.
Aidha, imesema haishughulikii vitendo vya rushwa, upandikizaji wa
mamluki na mivutano ya kisiasa au kidini vilivyojitokeza kwenye chaguzi
hizo kwa kuwa kuna vyombo vingine vya dola vinavyoshughulikia mambo
hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti
wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alisema mchakato mzima wa kuandaa
hadi kupata Katiba mpya utawahusisha wananchi na siyo matwaka ya asasi,
chama au kikundi fulani.
Alisema kundi au watu ambao hajakuridhika na uchaguzi huo wanaweza
kwenda kulalamika kwenye vyombo vya dola vinavyoshughulikia dosari
husika.
“Tunatengeneza Katiba ya Tanzania, hatutengenezi ya vyama wala ya
kikundi. Natoa wito tena kwa viongozi wa vyama vya siasa, Jumuiya na
Taasisi zingine ziwaache wananchi watoe maoni yao kuhusu rasimu ya
Katiba kwa uhuru,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Tunaomba vikundi visikilize wananchi wanasemaje, wananchi wana ndoto zao tusije tukalazimisha ndoto zetu zikawa zao.”
AKIRI KUSIKIA MALALAMIKO YA RUSHWA
Kuhusu rushwa, Jaji Warioba alisema kwamba baadhi ya maeneo chaguzi hizo
zilitawaliwa na rushwa, lakini akashauri wananchi waende kwenda
kulalamika kwenye vyombo husika.
“Hilo (la rushwa) lilikuwapo na hata kuleta mamluki kwenye uchaguzi,
nilistaajabu kusikia watu wanahonga ili wachaguliwe kuingia kwenye
mabaraza haya...makosa haya sisi hatushughuliki nayo, yanapaswa
kuripotiwa kwenye vyombo husika,” alisema.
Alisema dosari nyingine ni baadhi ya wananchi kuendelea na misimamo na
tofauti zao za kisiasa kwa kudhani kwamba Mabaraza ya Katiba ni jukwaa
la kutetea maslahi na misimamo ya vyama vya siasa kuhusu Katiba mpya.
Hata hivyo, alisema pamoja na dosari zilizojitokeza, chaguzi
zimekamilika kwa asilimia 99.8 Tanzania Bara na asilimia 96.4 Zanzibar.
Jaji Warioba alisema jumla ya kata 3,331 kati ya 3,339 na Shehia 323
kati 335, zimekamilisha vizuri mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza
ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.
Alisema tume yake inafanya kazi iliyopewa kwa weledi mkubwa na kwamba
ilitumia busara kuwashirikisha wananchi kwenye uundaji wa mabaraza ya
Katiba japokuwa sheria inairuhusu tume kufanyakazi hiyo yenyewe.
Alifafanua kuwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 inaeleza
kwamba kutakuwa na aina mbili za mabaraza; moja ambalo litaundwa,
kusimamiwa na kuendeshwa na Tume yake na lingine ni la hiari
litakaloundwa na asasi, taasisi au makundi ya watu wenye malengo
yanayofanana.
Alisema aina ya pili ya mabaraza hayo yatajiunda, kujisimamia na
kujiendesha yenyewe kisha kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba
kwa tarehe ambazo zitapangwa na Tume.
Alisema kwenye uundwaji wa aina ya kwanza ya mabaraza, Tume iliona
busara kuwashirikisha wananchi hivyo ikatoa mwongozo wa kuchagua wajumbe
kwa kutumia utaratibu uliowekwa na sheria ya Serikali za Mitaa sura 287
na 288 kupitia mikutano kwa ajili ya jambo maalum la Kata.
Alisema inashangaza kunaibuka malalamiko kwamba mabaraza hayo ni ya
kisiasa wakati utaratibu huo umekuwa ukitumika kuchagua kamati za
kusimamia mambo mbalimbali ya kata kama elimu, afya, miradi na
maendeleo.
Kuhusu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kususia mchakato huo
kama utaratibu hautasitishwa, Jaji Warioba alisema hataki kujiingiza
kwenye malumbano ya kisiasa kwa kuwa watakaokubali au kukataa katiba ni
wananchi.
Alisema: “Kama tusipoondokana na hii ya kujiweka vipande vipande hatutafikia mwafaka.”
Jaji Warioba ambaye alifuatana na Makamu wake, Jaji Augustino Ramadhan,
alisema tayari Tume imeanza kupokea majina ya watu wote waliochaguliwa
kuwa wajumbe pamoja na majina ya madiwani wote, mkurugenzi wa baraza la
manispaa, makatibu wa mabaraza ya miji na halmshauri za wilaya.
Alisema mchakato wa uwasilishaji wa majina itakamilika leo na kwamba
kwenye kata na shehia ambazo uchaguzi ulivurugika, Tume inaendelea
kuwasiliana na watu wa maeneo hayo ili kurudia uchaguzi.
Aliongeza kuwa kata ambazo hazijafanya uchaguzi ni tatu ambazo ni za mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kagera.
MAAMUZI MAGUMU
Alisema hivi sasa Tume inaandaa rasimu ya katiba na kwamba inatekeleza kazi hiyo kwa weledi mkubwa.
“Hali halisi inayojitokeza ni kwamba Tume italazimika kufanya maamuzi
magumu, wananchi zaidi ya 300,000 na makundi maalum zaidi ya 160 yametoa
maoni yao. Katika mambo mengi ya msingi maoni yanakinzana na katika
hali hiyo, lazima Tume ichague moja kati ya maoni hayo na kuyaacha
mengine,” alisema.
Alisema Tume yake itafanya maamuzi magumu kwa manufaa ya nchi kwa kuingiza kwenye Katiba hoja ambazo zitalisaidia Taifa.
“Kwa msingi huo, tume inawashauri wananchi nao wawe tayari kufanya
maamuzi magumu, kama kila mmoja akitaka wazo lake likubalike
haitawezekana kufikia mwafaka. Kila mmoja awe tayari kusikiliza mawazo
ya wengine. Ni lazima wote tuwe tayari kufanya maamuzi magumu,” alisema
Jaji Warioba.
Alitoa mfano kwamba baadhi ya maoni yanayokinzana ni wengine wanataka
kuvunja Muungano wakati wengine wakitaka uendelee na wengine wanataka
Muungano wa mkataba.
Alisema baadhi ya wananchi wanataka serikali nne yaani ya Pemba, ya
Unguja, ya Tanganyika na Jamhuri ya Muungano, wengine wanataka moja,
mbili na wengine tatu.
“Katika hali hii ni lazima tume ichague moja na kuyaacha mengine na tuko
tayari kujieleza kwanini tulichukua hili tukaache lile,” alisema.
Alitoa wito kwa vyama vya siasa, jumuiya, taasisi au makundi ya watu
wenye malengo yanayofanana kutumia fursa ya kisheria kuunda mabaraza ya
katiba na kutoa maoni yao kuhusu rasimu.
Maelezo hayo ya Jaji Warioba yamelenga kupuuza maoni yaliyotolewa na
Chadema bungeni baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe,
kusema kwamba chama hicho kitasusia mchakato wa katiba unaoendelea kwa
kuwa inaonekana kwamba mabadiliko yaliyokusudiwa yanaelekea kuilinda CCM
na Serikali yake na kuendeleza baraka za “Status Quo”.
Alisema ushahidi wa mwanzo unaonyesha kwamba utaratibu wa kupata
mabaraza ya katiba ni mabaraza ya CCM na siyo mabaraza ya Watanzania
kutokana na wajumbe hao kuchaguliwa na kamati ya maendeleo ya kata na
kwamba umelenga kuwagawa wananchi.
No comments:
Post a Comment