KITAIFA

 

SHEREHE ZA MIAKA 49 YA MUUNGANO

 



 

MAONYESHO YA NDEGE ZA KIVITA KATIKA SHEREHE ZA MUUNGANO






 WAISLAM WATAKIWA KUFUATA MWONGOZO WAO

WAUMINI wa dini ya kiislam wametakiwa kufuata mwongozo bora na kufahamu juu ya imani ya kweli kwa Muislam.

Hayo yamesemwa na ust Abdulrahman Mabwalo wakati akihutubia katika Msikiti wa Dhinureyn uliopo Wilolesi, manispaa ya iringa.

Amewataka wafahamu kuwa msingi wa maisha bora ya muislam upo katika kitabu kitukufu cha Quran hivyo ni vyema kuishi kwa kufuata kitabu hicho na Sunna za Mtume Muhamad (S.A.W).
 
Aidha amewataka Waumini hao wawe na subra katika maisha pindi wapatapo mitihani ili waweze kuishi vyema.

 

Vigogo Ardhi, Tamisemi kortini

 Maofisa waandamizi serikalini wamefikishwa katika Mahakama tofauti Dar es Salaam  na Korogwe jana wakituhumiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya ofisi na kuhujumu uchumi.

Maofisa hao wanatoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
Kesi ya Dar
Mpimaji  wa Wizara ya Ardhi, Revocatus Wachawendera na Mpimaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Steven Kongwa walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili, likiwamo la matumizi mabaya ya ofisi. Kongwa aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke na alistaafu miaka miwili iliyopita.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wakili Hussein Mussa jana alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando kuwa washtakiwa hao walifanya makosa hayo kati ya Januari 2000 na Desemba 2001. Akisoma hati ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, Wakili Mussa alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa waajiriwa wa ofisi ya umma, walitumia madaraka yao vibaya.
Alisema walikiuka mamlaka ya ofisi zao kwa kugawa eneo la wazi lililopo Mbezi ambalo lilitengwa kwa ajili ya bustani kinyume cha sheria. Wakili Mussa alidai katika shtaka jingine kuwa maofisa hao kwa pamoja walikiuka Kifungu cha 35 cha Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa kuligawa eneo hilo.
Alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja katika kipindi hicho cha Januari 2000 na Desemba 2001 wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa makusudi walikiuka sheria hiyo ya mipango miji na kugawa eneo la Mbezi Kitalu L bila ya kupata kibali kutoka mipango miji. Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana na Wakili Mussa alisema upelelezi umekamilika, hivyo aliiomba Mahakama kuipangia kesi hiyo siku nyingine ili kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Ili kupewa dhamana, Hakimu Mmbando aliwataka kila washtakiwa kila mmoja wao kuwa na mdhamini anayeaminika ambaye anafanya kazi katika taasisi inayotambulika kisheria.
Sharti jingine ni la kila mdhamini kusaini bondi ya Sh10 milioni. Washtakiwa walikamilisha masharti hayo na kesi yao imeahirishwa hadi Mei 20, mwaka huu.
Kesi ya Korogwe
Takukuru wilayani Korogwe imewashtaki vigogo watatu kwa makosa manne likiwamo la kuhujumu uchumi na kusababishia hasara ya Sh56 milioni kwenye Halmashauri ya Korogwe mkoani Tanga.
Mwendesha mashtaka wa Takukuru, George Magoti  alimsomea mashtaka mshtakiwa wa pili tu, Declley Nyato.
Mshtakiwa wa kwanza, ambaye ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri wa wilaya hiyo, Christine Midello na mshitakiwa wa tatu, Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Emmanuel Ntatiye hawakuwapo mahakamani.
Mbali na kumsomea mashtaka, Magoti aliiomba Mahakama ya Wilaya ya Korogwe kutoa hati zitakazowezesha kukamatwa kwa washtakiwa hao wengine.
Magoti aliiambia Mahakama kuwa kati ya Julai na Agosti mwaka 2011, Nyato na wenzake walitumia nyadhifa zao vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Sh15 milioni kwa Kampuni ya Concise pasipo kuishirikisha Bodi ya Zabuni.
Katika kosa la pili, Nyato anadaiwa kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Sh41,050,000 kwa Kampuni ya Concise Geo Solution bila ya kuishirikisha bodi ya zabuni na shtaka la tatu, wote wanatuhumiwa kupanga njama za kutenda kosa namba moja na mbili.
Shitaka la nne ni la kuhujumu uchumi. Wote kwa pamoja wanadaiwa kuisababishia Halmashauri ya Mji wa Korogwe, hasara ya Sh56,185,000 na kuvunja Sheria ya Kuhujumu Uchumi.
Nyato aliyakana mashtaka yote. Hakimu Arnold Kirekiano aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu baada ya kutoa masharti likiwamo la kuwa na mdhamini mmoja, ambaye ni mwajiriwa wa umma au shirika linalotambuliwa ambaye ana makazi ya kudumu Korogwe au fedha taslimu Sh9.4 milioni au hati ya mali isiyohamishika au maelezo yatakayothibitisha mali hiyo aliyonayo mdhamini ina thamani sahihi iliyotajwa na kusalimisha pasi za kusafiria mahakamani.

No comments: