Friday, March 25, 2016
MUFTI WA TANZANIA AMUOMBEA DUA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM
MUFTI wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubery amemuombea dua, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Rais Dk. John Magufuli ili waweze kulitumikia vema taifa na kuliletea maendeleo.
Zubery alimfanyia dua hiyo Makonda Dar es Salaam leo asubuhi alipofika nyumbani kwake kujitambulisha na kumjulia hali pamoja na kumueleza mambo kadhaa ya maendeleo yaliyofanyika.
"Tunakuomba mola wetu kuwapa moyo wa imani na uzalendo na kuwaepusha na mabaya yote Mkuu wetu wa Mkoa Paul Makonda, Rais wetu Magufuli pamoja na viongozi wote ili waliongoze taifa letu kwa amani" alisema Mufti Zubery" wakati akiomba dua hiyo.
Makonda akizungumza na Mufti Zubery nyumbani kwake Mikocheni alimwambia kuwa kuna mambo kadhaa ameyafanya kwa kushirikiana na watendaji wenzake kwa kukutana na waendesha boda boda ili kuwawezesha kupata mkopo utakaowasaidia kupata vitendelea kazi zao kama kupata kofia ngumu mbili za kuvaa dereva na abiria wake ili kuwasaidia katika shughuli zao za kusafirisha abiria.
Makonda alitaja mambo mengine kuwa ni suala nzima la kupambana na uhalifu ambao bado unaonesha kupamba moto hasa ujambazi wa kutumia silaha za moto.
Alitaja mambo mengine kuwa ni mkutano alioufanya hivi karibuni wa kukutana na wenyeviti wa mitaa na maofisa watendaji ili kuzungumzia suala la utunzaji wa mazingira na mambo mengine ambapo alisema ameandaa mpango wa kumzawadia mwenyekiti atakayefanya vizuri kwenye mtaa wake.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum alisema jambo alilofanya Makonda la kumtembea Mufti ni jambo zuri na kuwa kumuona mufti ni sawa kama amewaona waislam wote nchini.
Alisema wanamuombea Makonda mungu amzidishie wepesi katika kazi zake kwani ni viongozi wachache wanaopata madaraka ambao uwakumbuka viongozi wa dini kama alivyofanya Makonda.
Katika hatua nyingine Makonda alifanya ukaguzi wa barabara kadhaa za Manispaa ya Kinondoni ambazo hivi karibuni aliagiza zifanyiwe marekebisho ikiwa ni pamoja na kuchimba mifereji baada ya kuharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment