UMUHIMU WA SWALA NA NAFASI YAKE KATIKA UISLAMU
A: HUKUMU YA SWALA KWA MUJIBU WA
QUR-ANI NA SUNNAH
Ewe ndugu yangu mpenzi; hebu kwa
msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu tuzianze nasaha zetu kwa kumuomba Mola wetu
Mtukufu atuwafikshe na kutuongoza katika kuijua haki, kuikubali na ksha
kuifuata-Aamiyn Baada ya dua hiyo, hebu sasa tutazame kwa pamoja natujiulize
nini hukumu ya ibada ya swala ndipo tutafahamu ni ipi nafasi na hukumu ya mtu
asiye swali .
Ndugu yangu mpenzi, elewa na ufahamu
kwamba swali katika sheria ni FARDH yaani WAJIBU. Haya ni kwa mujibu wa aya
chungu mzima za Qur-ani Tukufu. Hebu tusitafakari kwa pamoja aya hizi zifuatazo
"…BASI SIMAMISHENI SWALA, KWANI
HAKIKA SWALA. IMEKUWA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA WAKATI MAALUM"
[4:103]
Ukizingatia aya hii utakuta inaeleza
kwa ufumbulizo na uwazi kabisa kwamba swali ni FARDHI, tenasi fardhi tu bali ni
fardhi iliyowekewa wakati maalum na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake
waumini kauli ya Mola karim Aliposema: "… HAKIKA SWALAKWA WAUMINI NI
FARDHI ILIYOWEKEWA WAKATI MAALUM " ni ishara na dalili bayana kwamba swala
ndio kielelezo kikubwa cha Imani ya mja. Kwa maneno mengine tunaweza kusema
kuwa hana Imani, mtu asiyeswali. Ikiwa mtu hana Imani , vipi unamtazamia kuwa
na dini? Hii ndio maana Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie akasema:
Mkimuona mtu aizoya Msikiti basi mshudieni kuwa yuna Imani kauli hii ya Bwana
Mtume inazidi kutuonyesha ukweli usio pingika kwamba swala ndio nembo na
kielelezo kikubwa cha Imani ya mja. Hebu tuitafakari na aya hii:-
"HIFADHINI (angalieni sana) SWALA (zote kuziswali) NA (khasa) ILE SWALA YA
KATI NA KATI "[2:238]
Tukilizingatia neno la mwanzo
lilotumika katika aya (HIFADHINI) tukaliweka katika sarufi ya kiarabu (Arabic
Grammar), tutaambiwa na watu wa fani ya lugha kuwa neno hili ni tendo la amri.
Kwa hivyo basi neno hili (HIFADHINI) inbamaanisha kuwa suala la kuhifadhi swala
ni amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu kuja kwa waja wake na wala sio ombi.
Sasa
kama tunakubaliana na ukweli huu ulio dhahiri kuwa swala ni amri ya Mola
amuamrisha mja wake, je! Huoni kwamba kuacha swala ni kupinga na kuivunja amri
ya Muumba wako? Avunjaye na kupinga amri ya Bwana wake hufanywaje na Bwana
wake, hasa ukizingatia kwamba siku zote amri hutoka kwa Mkubwa aliye kuja juu
kwa mdogo aliye chini kama ambavyo ombi hutoka kwa aliye chini kuja kwa aliye
juu.
Hebu jaribu kuwa mkweli, mwanao au mkeo akivunja amri yako, unakuwaje na
unchukua hatua gani? Ukiukir ukweli huu ndipo utaiona nafasi yako mbele ya Mola
wako wewe usiyetaka kumsujudia Mola wako.
Naam, tumetangulia kusema huko nyuma
kwamba swala ni FARDHI /WAJIBU, hebu sasa tulitazame neno WAJIBU limeaanishwa
vipi na sheria ili uione nafasi yako wewe usiyeswali. Wataalamu wa fani ya
fiq-hi wamelianisha neno wajibukwa kusema (WAJIBU/FARDHI ni lile jambo ambalo
Allah ameliwajibisha juu yetu, hulipwa mtu aliye baleghe (mtu mzima),mwenye
akili timamu kwa kulitenda/kulitekeleza (hilo la wajibu)na huaadhibiwa kwa
kuwacha kulitenda, kama vile swala, funga na kuwatii wazazi). Hili ndilo
ainisho (definition) sahali la WAJIBU, hebu sasa lichukuwe aanisho hili
uliambatishe na swala, unafahamu nini? Ikiwa wewe ni mkweli, uliokulazimu kwa
amri ya Mola Muumba wako na kwamba ukiswali utakuwa umeikubali na kuipokea
kuitekeleza amri ya Mola wako kwa maslahi na faida ya nafsi yako, hivyo
utalipwa thawabu ambaazo ndizo "Dollar" za kuinunulia akhera. Kinyume
chake ni kwamba kama hukuswali utakuwa umeipuzana na kuivunja amri ya Molawako
kwa maangamivu na khasara ya nafsi yako mwenyewe, kwa hivyo utaaadhibiwa kwanza
hapa hapa duniani, kaburini na kesho akhera kama lilivyothibiti hilo katika
hadithi ya Mtume –Rehema na Amani zimshukie. Tusome kwa mazingatio: "… NA
BILA SHAKA ADHABU YA AKHERA NI KALI ZAIDI NA IENDELEAYO SANA"[20:127]
"ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA
(mwenye) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi) YAKE NAMOLA WAKO
SI DHALIMU KWA WAJA WAKE."[41:46]
B: NAFASI YA SWALA KATIKA UIISLAM
Katka kuonyesha umuhimu na nafasi ya
swala,Bwana Mtume- Rehema na Amani zimshukie –ameijaalia swala kuwa inashika
nafasi ya pili katika nguzo tano za uislam "uislamu umejengwa juu ya nguzo
tano: kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa ila Allah na Muhammad ni
Mtume wa Allah, kusimamisha swala, kutoazakah, kufunga ramadhani na kuhiji
Makkah-Mukaram" Bukhaariy.
Ukiitafakari hadithi hii utaona ya
kwamba Mtume –Rehema na Amani zimshukie –anaumathihsha uislamu na mfano wa
jengo kubwa, imara na madhubuti lililojengwa juu ya nguzo tano. Hapana hata
mmoja awezaye kupinga kwamba kuna jengo linaloweza kusimama bila ya nguzo. Kama
tunakiri ukweli huu, basi ni dhahiri kwamba hapana uislam pasipo na nguzo tano
hizi na pasipo na nguzo na uislam pana kufru tu si vinginevyo.
Eeh Mola wetu
tukinge na ukafiri kwa kutujulia kuisimamisha swala maisha yetu yote Aamiyn.
Inakupasa uelewe ewe nduguyangu mpenzi muislam kwamba swala ndio nguzo tukufu
kabisa ya dini na nafasi na umuhimu wa swala katika uislamu ni kama vile ilivyo
nafasi na umuhimu wa kichwa katika kiwiliwili. Basi kama ambavyo asivyokuwa na
uhai mtu asiye na kichwandivyo ambavyo hana uislamumtu asiye na swala. Bwana
Mtume –Rehema na Amani zimshukie anatuasa kwa kutuambia : "Ye yote
atakuyeicha swala kwa makusudi, bila ya shaka amekufuru" Twabraaniy.
Haya hebu jiulize ewe Ndugu yangu
Muislamu na uihurumie nafsi yako, mtu aliyekufuru ana Uislamu ?! Fahamu ewe
Ndugu yangu unayemuasi Mola wako kwa kuacha kuswali kwamba sala ndio nguzo ya
dini hii, dini haipo bila ya nguzo hii. Haya yanathibitishwa na kauli ya Bwana
Mtume – Rehema na Amani zimshukie – "Swala ndio nguzo ya dini,
atakayeisimamisha, hakika ameisimamisha dini na atakayeiacha, bila ya shaka
huyo ameivunja dini". Kwa mantiki hii, mtu atakayeihifadhi nguzo hii kwa
kuswali katika nyakati zake maalumu na akatimiza sharti na nguzo zote hali
kujinyenyekeza kwa Mola wake na huku akiamini kuwa ni wajibu wake kuswali, huyo
ndiye atakayefaulu duniani na akhera.
Tunasoma ndani ya Qur-ani Tukufu :
"KWA YAKINI WAMEFAULU WAUMINI AMBAO WAO NI WANYENYEKEVU KATIKA SWALA
ZAO" Al-Muuminun : 1-2. Kinyume chake yule atakayeipuuzia swala, akaacha
kuswali, huyo ndiye mtu muovu aliyepata khasara duniani na akhera kwa sababu ya
kuikhalifu amri ya Mola Muumba wake. Kwa mujibu wa kauli iliyotangulia ya Bwana
Mtume, wewe usiotaka kuliweka paji lako la uso ardhini kumsujudia Mola wako
umeichukua nyundo kubwa na nzito unaivunja na kuibomoa dini ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu.
Dini ambayo amewatuma mitume wake wote, tangu Nabii Adam mpaka Mtume
wa mwisho Muhammad – Rehema na Amani ziwashukie wote – kuja kuisimamisha katika
katika ardhi hii. Je, mbomoa dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu si mgomvi wa Allah,
na hivi mtu anaweza kugombana na Allah kisha akatazamia kupata salama ?! La
hasha.
Ewe mpenzi ndugu yangu, elewa na
ufahamu kwamba swala ndiyo ibada ya kwanza kabisa aliyoiwajibisha Mwenyezi
Mungu kwa waja wake. Amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie - :
"Cha mwanzo alichokifaradhisha Allah kwa umati wangu ni swala tano, na cha
mwanzo kinachorufaishwa (kinachopanda mbinguni) katika amali (matendo) yao ni
swala tano, na cha mwanzo watakachoulizwa katika amali zao ni swala tano
…." Ndugu yangu mpenzi usiotaka kumsujudia Mola wako aliyekuumba,
haikutoshi hadithi hii kuona ni jinsi gani ibada ya swala ilivyopewa umuhimu wa
kwanza katika Uislamu ?! Amali zako zote njema ni lazima zitanguliwe na swala
tano ndipo zikubaliwe, kinyume na hivyo amali hizo hazina maana bali ni sawa
sawa na mavumbi yapeperushwayo.
Ushahidi wa haya ni kauli ya Bwana Mtume –
Rehema na Amani zimshukie – "Cha mwanzo atakachokaguliwa/atakachohesabiwa
mja siku ya kiyama ni swala, ikitengenea zimetengenea baki ya amali zake
nyingine, ikifisidika (swala) zimefisidika (zimeharibika) baki ya amali zake
nyingine"
Ndugu mpenzi muislamu, ukiyakiri
maneno haya ya Bwana Mtume yatakufikisha katika ukweli na hakika kwamba swala
ndio ibada mama. Kadhalika ili kuonyesha utukufu wa ibada ya swala, utaikuta
swala ndio ibada pekee aliyoitiwa Bwana Mtume na kukabidhiwa na Mola wake mbinguni.
Ibada nyingine zote Bwana Mtume alikuwa akiletewa amri hapa hapa ardhini
kupitia kwa malaika Jibril – Amani imshukie – Allah alimkuhutubu Mtume wake juu
ya swala tano katika ule usiku wa Miraji pasina wasita wa Jibril. Amesema Anas
– Allah amridhie – Imefaradhishwa swala kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
usiku aliopelekwa mbinguni swala khamsini, kisha zikapunguzwa mpaka zikawa
tano, kisha (Mtume) akaitwa ewe Muhammad ! Hakika maneno yangu hayabadilishwi
na utapata wewe katika swala tano hizo ujira wa swala khamsini"
Ndugu yangu muislamu, hebu
yatafakari kwa makini maneno ya Mtume wako, utauona utukufu wa ibada ya swala.
Ni kwa ajili hiyo ndio tunaona Allah anatuamrisha kuhifadhi na kudumisha swala
na muislamu amewajibikiwa kuitekeleza swala muda wa kudumu roho yake katika
kiwiliwili chake.
Akiwa mzima wa afya njema au mgonjwa asojiweza kitandani kwa
sharti ya kuwa na fahamu za kujua alitendalo. Awapo vitani au katika hali ya
amani, akiwa safarini au la, swala imemlazimu tu. Mwanamume na mwanamke wote ni
sawa katika amri hii ya swala, ila mwanamke hatoswali akiwa katika hali ya
hedhi au nifasi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuamrisha swala
"HIFADHINI (angalieni sana) SWALA (zote kuziswali) NA (khasa) ILE SWALA YA
KATI NA KATI NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH NA MKIWA KHOFU
( mmo vitani, basi swalini) HALI YA KUWA MNAKWENDA KWA MIGUU AU MMEPANDA
(wanyama) NA MTAKAPOKUWA KATIKA AMANI BASI MKUMBUKENI ALLAH (swalini) KAMA
ALIVYOKUFUNZENI YALE MLIYOKUWA HAMYAJUI" [2:238-239]
Ndugu yangu mpenzi, utabainikiwa
kutokana na aya hii kwamba muislamu hana udhuru hata chembe unaomuhalalishia
kuacha swala. Hivyo basi muislamu atakayeitekeleza swala kama itakikanavyo,
swala hiyo itakuwa ni hoja (wakili wa kumtetea) itakayomuokoa siku ya Kiyama,
si hivyo tu bali itakuwa ni nuru itakayomuangazia na kumuongoza katika siku
hiyo ngumu na nzito kama ambavyo itakovyokuwa ni sababu ya kufutiwa madhambi
yake.
Imepokelewa kutoka kwa Sayyidna
Uthman – Allah amuwie Radhi – amesema : nimemsikia Mtume – Rehema na Amani
zimshukie – akisema : "Hatawadhi mtu udhu wake vizuri kisha akaswali ila
Allah humsamehe mtu huyo madhambi yaliyo baina ya swala hii na swala
ijayo".
Basi ni kheri na furaha iliyoje kwa
yule aliyeitekeleza swala kwa ukamilifu, ukamilifu na unyenyekevu mpaka
anamaliza muda wake wa kuishi hapa duniani (anakufa). Eh! Ole wake, tena ole
wake na majuto yake yule aliyefanya kibri, akaacha kuitekeleza swala hata
akaondoka duniani bila ya kumsujudia Mola wake.
Hebu itegee sikio la usikivu kauli
hii tukufu ya Allah asema nini juu ya watu hawa : "(Na wawalete) HIYO SIKU
KUTAKAYOKUWA NA MATESO MAKALI NA WATAITWA KUSUJUDU LAKINI HAWATAWEZA. MACHO YAO
YATAINAMIA CHINI; UNYONGE UTAWAFUNIKA NA HAKIKA WALIKUWA WAKIITWA KUSUJUDU
WALIPOKUWA SALAMA (na walikataa)" [68:42-43].
Watu wa peponi watawauliza watu wa
motoni : "NI KIPI KILICHOKUPELEKENI MOTONI ? WASEME : HATUKUWA MIONGONI
MWA WALIOKUWA WAKISWALI. HATUKUWA TUKILISHA MASIKINI. NA TULIKUWA TUKIZAMA
(katika maasia) PAMOJA NA WALIOKUWA WAKIZAMA" [74:42-45]. Khasara na
maangamivu yaliyoje, leo utawaona baadhi ya waislamu hawaswali na hoja yao
kubwa shughuli nyingi hawana nafasi, wametingwa na kazi na wengine huthubutu
hata kusema kwa kinywa kipana kabisa kwani ni lazima kuswali, kama ninafanya
mema mengine haitoshi ?! Hebu itegee sikio kauli hii ya Bwana Mtume – Rehema na
Amani zimshukie - : "Yeyote yule atakayeihifadhi swala, iatkuwa (swala
hiyo) ni nuru, hoja na uokovu kwa mtu huyo siku ya Kiyama, na yeyote yule
asiyeihifadhi swala, haitokuwa (swala) ni nuru, hoja na uokovu kwa mtu huyo,
bali atakuwa (motoni) siku ya Kiyama pamoja na akina Qaarun, Fir-aun, Haaman na
Ubayyi bin Khalaf".
Fahamu ewe ndugu yangu muislamu,
swala ina nafasi na utukufu wa pekee katika Uislamu ndio maana tunamkuta Bwana
Mtume mara nyingi anatuhimiza swala na swala ndio ulikuwa wasia wake wa mwisho
wakati anaondoka duniani : "Ninakuhimizeni na kukuusieni swala pamoja na
wamilikiwa wa mikono yenu ya kuume".
C. KHATARI YA KUACHA SWALA
Ndugu yangu Muislamu, bila shaka
unatambua au umewahi kusikia kwamba Allah aliwaamrisha malaika pamoja na Ibliis
wamsujudie baba yetu Nabii Adam – Amani imshukie – hali ya kumuamkia.
Iblisi kwa ushupavu na kibri
alichokuwa nacho alikataa kuitii na kuitekeleza amri ya Mola wake. Ni kwa
sababu hii tu Allah akamfukuza Iblis na kumtoa huko alikokuwa pamoja na Malaika
na akamlaani mpaka siku ya kiyama, na kesho akhera ataingia motoni.
Tusome kwa mazingatio : "(na
wakumbushe watu khabari hii) TULIPOWAAMBIA MALAIKA MSUJUDIENI ADAM ( yaani
mwadhimisheni kwa ile elimu yake aliyopewa) WAKAMSUJUDIA WOTE ISIPOKUWA IBLIS,
AKAKATAA NA AKAJIVUNA NA (toke hapo) ALIKUWA KATIKA MAKAFIRI (ila tu
alichanganyika tu na malaika)" [2:34].
Basi wewe ndugu yangu mpenzi
usiotaka kuswali, hujioni kuwa wewe ni mbaya zaidi kuliko Iblis ?! Iblis
alikataa kumsujudia Nabii Adam, wewe leo unakataa kumsujudia aliyemuumba Nabii
Adam.
Iblis alikataa kusujudu mara moja
tu, wewe leo unakataa kusujudu mara thelathini na nne (34) kila siku, mara 238
kila wiki, mara 1020 kila mwezi, mara 12,104 kwa mwaka, mara ….. katika umri
wako, jaza mwenyewe. Iblis alikataa kusujudu sijida ya heshima kwa Nabii Adam,
wewe unakataa kusujudu sijida ya ibada kwa Mola Muumba wako.
Hebu angalia tena adhabu aliyopewa
Iblis kwa kuacha sijida moja tu alilaaniwa na kutolewa peponi na huku
akisubiriwa kuliongoza kundi la watu wa motoni kuingia motoni.
Hii inamaanisha mwenye kuacha sijida
34 kila siku anastahiki kupata adhabu kali zaidi ya ile aliyopewa Iblis
mlaaniwa, sikwambii asioswali juma moja au zaidi. Ndugu yangu usioswali unatarajia
nini ikiwa hali ni hiyo ?! Unaona uzito gani kumsujudia Mola wako ?! Aletwe
Mtume mwingine ndio utasikia na kutii ?! Hebu ihurumie nafsi yako, huiwezi
adhabu ya Mola wako.
Ndugu yangu umepewa neema ya akili,
ishukuru neema hiyo kwa kuzingatia uambiwayo, umepewa masikio ili usikie,
isikie haki na kuifuata, usijitie upofu na uziwi wa bure ukajuta na kuangamia.
Zinduka, usiingie katika kauli ya
Allah isemayo : "NA BILA SHAKA TUMEWAUMBIA MOTO WA JAHANAMU WENGI KATIKA
MAJINI NA WANADAMU (kwa sababu hii): NYOYO WANAZO LAKINI HAWAFAHAMU KWAZO, NA
MACHI WANAYO LAKINI HAWAONI KWAYO, NA MASIKIO WANAYO LAKINI HAWASIKII KWAYO.
HAO NI KAMA WANYAMA, BALI WAO NI WAPOTOFU ZAIDI. HAO NDIO WALIOGHAFILIKA"
[7:179].
Tahadhari ewe
ndugu yangu, usiwe na sifa hizi zilizotajwa, kwani hizi ni sifa za watu wabaya,
watu wa motoni. Tumuombe Mola wetu Mtukufu asitujaalie kuwa miongoni mwa watu
wa motoni, wasiotaka kumsujudia – Amin.
RUSHWA:HATARI NA ATHARI ZAKE
KWA NINI UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI
RUSHWA:HATARI NA ATHARI ZAKE
RUSHWA:HATARI NA ATHARI ZAKE
Msemo
"Rushwa ni adui wa haki", kelele zinapopigwa ulimwenguni kote na
wanasiasa, viongozi na serikali na wale wa dini dhidi ya rushwa. Haya yote ni
ishara na dalili wazi juu na namna jamii inavyoathirika na kukerwa na mdudu
mbaya huyu, rushwa. Rushwa ni mdudu mwenye athari mbaya sana kwa jamii, mdudu
anayeua bila huruma haki za kimsingi na za kijamii.
Mwenyezi Mungu
Mtukufu anatuasa:
"WALA MSILIANE
MALI ZENU KWA BATILI NA KUZIPELEKA KWA MAHAKIMU ILI MPATE KULA SEHEMU YA MALI
YA WATU KWA DHAMBI NA HALI MNAJUA" [2:188]. Amesema swahaba wa Mtume-Ibn
Abbas-Allah amuwiye radhi-katika kuitafasiri aya hii: Katazo hili linamuhusu
mtu mwenye kumiliki mali bila ya uhalali wowote, kisha akamuendea hakimu kutaka
kupata uhalali wa kumiliki na ilhali anajua fika kuwa haki si yake. Huyo aelewe
kuwa anapata dhambi na anachokila ni haramu.
Aya
inafahamisha kuwa hukumu ya huyu hakimu kumuhalalishia dhalimu na kumpa haki
asiyoistahiki haibadilishi chochote hakika na ukweli. Hakika itabakia pale pale
mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa mali ile si haki yake na ukweli ni kuwa mali
itabakia kuwa ni haramu inayompatia dhambi za uovu wake huo.
Kwa mantiki
hii, hakimu muhalalishaji wa haramu hali anajua na dhalimu muhalalishiwa haramu
hali nafsi yake inakiri kuwa haramu wawili hawa watashirikiana katika dhambi za
uovu huu.
Mwenyezi Mungu
anatukataza na kutuonya katika aya hii kula au kuchukua mali ya mtu kwa njia ya
batili yaani kwa njia isiyo ya halali. Kula mali ya mtu katika njia ya batili
ni pamoja na kupokonya, kupora,kudhulumu,kupokea rushwa na kadhalika. Kwa nini
Mwenyezi Mungu amesema:" WALA MSILIANE MALI ZENU", akatumia neno KULA
badala ya KUCHUKUA. Neno KULA limetumika kwa kuwa ndio makusudi na lengo kuu la
kuchukua/kupata mali. Mporaji anapopora ili ale, dhalimu anadhulumu apate kula,
mpokea rushwa anapokea pia kwa ajili ya Tumbo.
Hili ndilo
lengo la kwanza, kisha ndio hufuatia mengine kama vile kuvaa,kujenga,kununua
gari,shamba na kadhalika. Ndio maana watu husikika wakisema (Fulani anakula
mali za watu) wakiimanisha: Anachukua mali za watu bila ya uhalali,kwa njia
batili.
Mwenyezi Mungu
amewaumba wanadamu na akawapangia na kuwawekea sheria zitakazoyatawala maisha yao
katika ulimwengu huu wa muda,ili waishi kwa amani,salama na utulivu. Mwenye
nguvu asimdhulumu mnyonge wala mkubwa asimuonee mdogo.
Basi mfanyakazi
anayepokea rushwa kwa ajili ya kutoa huduma,huyu anaivunja misingi ya amani
katika jamii, anavuruga nidhamu/utaratibu wa sheria. Huyu mbali ya kuwa ana
hatia mbele ya mahakama adilifu ya Mwenyezi Mungu pia anaikosea jamii nzima kwa
kuwa anapokea ujira kwa kuivunja amani.
Mtoaji wa
rushwa pia haiepuki hatia kwa kuwa kutoa anatoa ujira kufisidi/kuharibu
uadilifu. Mali anayoipokea mlaji rushwa ni moto na ataadhibiwa kwa uchukuaji wa
mali hiyo adhabu kali kabisa, kwa sababu ya kuvunja kwake sheria ambayo misingi
yake mikuu ni uadilifu na amani. Hebu uone ubaya na athari ya rushwa kwa jamii
kupitia mifano hali ifuatayo:
Serikali/Shirika
la umma limetangaza nafasi za kazi.
Wananchi wenye
sifa zinazotakiwa wakajitokeza kujaza nafasi hizo. Mtu aliyekabidhiwa na umma
dhamana ya kuhoji watu hawa na hatimaye kuwaajiri wanaostahiki.
Huyu anayapiga
teke maadili na muongozo wa kazi yake,badala ya kuwachagua watu kwa sifa
husika, yeye anawachagua watu kwa vigezo vya udugu, na kwa kupewa rushwa.
Natija ya
uchaguzi huu ni kuwapa ajira watu wasiostahili, jambo ambalo litasababisha
utendaji mbovu usio na ufanisi, utendaji utakaopelekea kufilisika na hatimaye
kufa kwa shirika ambalo ni mali ya umma. Uharibifu wa mtu mmoja huyu mwenye
maradhi hatari ya rushwa unasababisha kuathirika kwa jamii nzima ni kwa sababu
hii ndiyo Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie –akaikemea vikali rushwa
aliposema "Mtoaji na mpokeaaji rushwa (wataingia ) motoni".
At-twabraaniy.
Utamuona leo
daktari anayetupilia mbali maadili ya kazi yake, anavua utu wake na kuuvaa
unyama. Anamuacha mgonjwa kufa mbele ya macho yake eti tu kwa sababu hakupewa
chai (rushwa).
Huu ndio ukweli
na sote tunishuhudia hali hii kila leo. Mdudu rushwa ameiondosha kabisa huruma
ndani ya moyo wa daktari kiasi cha kuwa maisha ya binadamu mwenziwe hayana
thamani kama hakupewa rushwa.
Ni kutokana na
athari hii mbaya ya rushwa ndio Bwana Mtume –Allah amshushie Rehema na Amani
–akasema "Allah amemlaani mtoaji na mpokeaji rushwa na mkaa kati
yao". Ahmad
Hebu tuangalie
hakimu anayepewa dhamana ya kusimamia haki. Huyu kwa sababu ya kitu kidogo
alichopewa (rushwa) anampa haki mtu asiyestahiki na kumnyima mwenye haki au
anamfunga mtu kwa dhuluma kwa sababu tu kuna mtu anataka kumkomoa au anamuachia
huru mtuhumiwa aliyetiwa hatiani na sheria kwa ajili ya kupewa rushwa.
Hizi ni baadhi
tu za athari nyingi za rushwa kwa jamii. Rushwa ikienea katika jamii husika,
tabia za watu zitaharibika,utu na heshima vitatoweka na badala yake
unyama,chuki na uadui ndivyo vitaitawala jamii hiyo kama tulivyoona katika
mifano yetu hai. Mla rushwa ni mtu mbaya na hatari sana katika jamii.
Huyu hana utu,
hana haya wala huruma na ndio maana Bwana Mtume hakumuonea haya kumshushia
laana za Mwenyezi Mungu.
Ewe ndugu yangu
uliyelemazwa na maradhi ya rushwa hebu jiulize na kisha ujihurumie. Jee,
unaweza kuibeba laana ya Mola wako? Kulaaniwa na Mwenyezi Mungu maana yake ni
kutengwa na Rehema za Mola duniani na akhera , Je, utasalimika ikiwa hukupata
rehema za Mola wako? Kutokupata rehema kunaamaanisha kupata ghadhabu je ndugu
yangu unao ubavu wa kuhimili ghadhabu za Mola wako.
Ikemee nafsi yako, acha
kuanzia leo tabia mbaya ya kupenda na kupokea rushwa kwa huduma ambayo
unawajibika kuitoa huku ukiitafakari kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:-
"ANAYEFANYA
MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE,NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya
nafsi)YAKE (vilevile) NA MOLA WAKO SI DHALIMU (hata kidogo) KWA WAJA (wake).
[41:46]
Chagua
sasa,kuendelea kula rushwa kwa khasara na maangamivu ya nafsi yako mwenyewe au
kuacha kula rushwa kwa faida na maslahi ya nafsi yako. Kumbuka "Rushwa ni
adui wa haki" na mla rushwa ni "Adui wa Mungu, Mtume na watu wote"
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
YA KIISLAMU
Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – alipotumwa
na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuja ulimwenguni kuuhusisha Uislamu ulioasisiwa na
Mitume waliomtangulia, alimkuta mwanamke akiishi chini ya mazingira na kivuli
cha ukandamizaji. Katika ulimwengu ule, mwanamke hakuwa na haki yeyote ile
katika jamii yake bali alionekana kama ni bidhaa inayoweza kuuzwa wakati
wowote.
Mwanamke alichukuliwa kama ni chombo cha kumstarehesha na
kukidhi matamanio ya kimwili ya mwanamume.
Mwanamke alihesabika kuwa ni chombo cha uzalishaji na
hakuwa na uchaguzi/uhuru wa kupanga na kuamua. Haya kwa mukhtasari ndiyo
mazingira ambayo Uislamu ulimkuta mwanamke akiishi chini ya anga lake.
Mwenyezi Mungu kupitia mfumo sahihi wa maisha (Uislamu)
ambao dhamana ya uongozi wake alimpa Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie
– akamuondolea mwanamke unyonge, udhalili, dhulma, uonevu na unyanyasaji ule.
Uislamu ukamjengea mwanamke mazingira bora, kanuni na sheria ambazo
zitamuhakikishia uhuru, usalama, amani, haki na usawa katika jamii yake.
Uislamu ukamtayarishia mwanamke anga zuri, chini ya anga
hilo ataishi huku akijihisi kuwa ni binadamu kamili, mwenye haki sawa kama
mwanamume na ukamdhaminia kupata haki zote kama binadamu bila ya kuhitajia
upendeleo maalum kama tusikiavyo istilahi hii ikipigiwa kelele ulimwenguni kote
bila ya utekelezaji wowote.
Uislamu ukamuondoshea mwanamke tuhuma ya kumpotosha Baba
yetu Adam – amani iwashukie wote – peponi na kuwa yeye (mwanamke) ndiye asili
na chanzo cha uovu wote huu utendekao ulimwenguni. Uislamu ukabainisha kwamba
ni shetani mlaaniwa ndiye aliyewapoteza Nabii Adam na mama yetu Hawaa, kama
tunavyosoma katika kitabu cha Uislamu "(Lakini) SHETANI (yule Iblis adui
yao) ALIWATELEZESHA WOTE WAWILI (wakakhalifu amri ile, wakala katika mti huo
waliokatazwa) NA AKAWATOA KATIKA ILE (hali) WALIYOKUWA NAYO …[2:36].
Uislamu unakiri na kutangaza wazi kuwa watu wote bila ya
kujali rangi au hali zao kimaisha wameumbwa kutokana na nafsi moja tu. Tusome,
tuzingatie na tukubali : "ENYI WATU ! MCHENI MOLA WENU AMBAYE AMEKUUMBENI
KATIKA NAFSI (asili) MOJA …." [4:1]
Huu ni usawa wa binadamu katika mfumo adilifu wa maisha
(Uislamu). Chini ya kivuli cha mfumo huu, mwanamke na mwanamume wanaogelea
pamoja katika bahari moja ya usawa wa haki zote za msingi za binadamu bila ya
kubaliwa. Isitoshe ule utukufu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu aliompa mwanadamu
katika kauli yake : "NA HAKIKA TUMEWATUKUZA WANADAMU …" [17:70].
Huu
ni utukufu aliozawadiwa mwanadamu yoyote bila ya kuangalia ni mwanamume au
mwanamke, wote wanashirikiana kwa usawa katika utukufu huu. Qur-ani Tukufu
inapomzungumzia mtu au wanadamu, basi huwa inamkusudia mwanamume pamoja na
mwanamke. Ama inapotaka kumtaja mwanamume au mwanamke peke yake bila ya
kumhusisha mwenzake basi hutumia istilahi "wanamume" au
"wanawake".
Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anazidi kuudhihirisha
ulimwengu nafasi aliyonayo mwanamke katika mfumo huu sahihi wa maisha
(Uislamu).
Anatuonyesha uhusiano uliopo baina ya mwanamume na
mwanamke katika kauli yake: "Wanawake ni ndugu baba mmoja, mama mmoja na
wanamume, wanayo haki kwa sheria (kufanyiwa na wanamume) kama ile haki iliyo
juu yao kuwafanyia wanamume" Abu Dawoud. Istilahi ya ndugu baba mmoja,
mama mmoja aliyoitumia Bwana Mtume inatoa sura kamili ya usawa baina ya
mwanamke na mwanamume.
Kwa jicho la mfumo kamili huu wa maisha (Uislamu)
wanamume na wanawake kiasili ni sawa sawa bila tofauti yeyote mbele ya Mola
wao. Ila tofauti na ubora utajitokeza katika amali njema anazozifanya kila
mmoja wao, ni dhahiri kuwa mzuri na mwingi wa amali njema hawezi kulingana sawa
na mchache wa amali njema bila ya kuangalia ni mwanamume au mwanamke, hii ndio
mojawapo wa misingi na kanuni za Uislamu.
Tusome kwa mazingatio na kutafakari : "WAFANYAJI
MEMA, WANAMUME AU WANAWAKE, HALI YA KUWA NI WAISLAMU, TUTAWAHUISHA MAISHA MEMA
NA TUTAWAPA UJIRA WAO (Akhera) MKUBWA KABISA KWA SABABU YA YALE MEMA WALIYOKUWA
WAKIYATENDA" [16:97].
Uislamu unazidi kumthibitishia na kumuhakikishia mwanamke
nafasi ya usawa kwa kumpa fursa sawa ya kukubaliwa na kujibiwa dua sawa
sawa/sambamba na mwanamume bila ya kupoteza amali zake njema. Hili linathibitishwa
na Qur-ani Tukufu : "MOLA WAO AKAWAKUBALIA (maombi yao kwa kusema) HAKIKA
MIMI SITAPOTEZA JUHUDI (amali) YA MWANAMUME AU MWANAMKE (kwani nyinyi) NI
NYINYI KWA NYINYI …" [3:195].Muundo wa maelezo ya Qur-ani Tukufu NI NYINYI
KWA NYINYI unatufahamisha kuwa kuna hali ya kutegemeana baina ya mwanamume na
mwanamke na kwamba maisha ya kila mmoja wao hayakamiliki bila ya kushirikiana
na mwenziwe.
Uislamu unauthamini mchango wa mwanamke katika jamii,
ndio maana ukampa nafasi na haki sawa ya kushiriki katika vitakatifu vya kidini
"Jihadi" sambamba na mwanamume.
Katika medani ya vita kuna watakaokufa mashahidi, kuna
majeruhi, wapiganaji ni wanadamu wanahitaji huduma ya maji na chakula. Nani
atakayetoa huduma hizi ili kuipa ushindi dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ? Hapo
ndipo unapoonekana umuhimu wa mchango wa mwanamke katika kuipigania dini ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ni kutokana na sababu hii na nyinginezo ndio tunamkuta
Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa haendi katika vita vyovyote
ila ataambatana na wanawake.
Bibi Umayyah bint Qays ni mwanamke anayetajwa sana katika
vitabu vya historia ya Uislamu kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika
vita vya Khaybar. Kwa kuuona na kuuthamini mchango wa bibi huyu, baada ya
kumalizika vita hivi Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alimtunukia
kidani alichokivaa maisha yake.
Alipokurubia kufa aliusia azikwe pamoja na kidani chake –
Allah amuwie radhi -. Mwanamke huyu na wale wote watakaomuiga wanaingia katika
kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : "LAKINI MTUME NA WALE WALIOAMINI PAMOJA
WALIIPIGANIA (dini) KWA MALI ZAO NA NAFSI ZAO; NA HAO NDIO WATAKAOPATA KHERI;
NA HAO NDIO WENYE KUFUZU (kufaulu) . ALLAH AMEWATENGENEZEA MABUSTANI YAPITAYO
MITO MBELE YAKE, WAKAE HUMO. HUKO NDIKO KUFUZU KUKUBWA" [9:88-89]
Kadhalika Uislamu haukumuacha nyuma mwanamke katika
uwanja wa elimu bali umemshirikisha kikamilifu sambamba na mwanamke. Hili
linathibitishwa na kauli/agizo la Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie - :
"Utafutaji/Kutafuta elimu ni fardhi ya lazima kabisa kwa kila muislamu
mwanamume na muislamu mwanamke". Utaona kupitia agizo/kauli hii ya Bwana
Mtume, Uislamu umewajibisha mwanamke apate elimu.
Hivi baada ya haki hizi za msingi alizopewa mwanamke wa
Uislamu, haki ambazo zinalindwa na kusimamiwa na sheria madhubuti, kuna mtu
muadilifu atakayefunua kinywa kipana na kudai kuwa eti Uislamu unamdhulumu na
kumkandamiza mwanamke ?! Ndugu zanguni, ni lazima tukubali kuwa hapa kuna mambo
mawili; Uislamu kama dini na mfumo sahihi wa maisha unaotawaliwa na sheria ya Allah
na upande wa pili kuna wanaoitwa waislamu wanaitawaliwa na desturi/ada na
mwenendo mbaya dhidi ya mwanamke. Kwa hivyo ni lazima tutofautishe baina ya
vitu viwili hivi kama kweli tu waadilifu.
Kelele hizi na wimbo huu wa kunyanyaswa, kudhulumiwa na
kunyimwa haki mwanamke zilizoenea leo ulimwenguni kote ni kelele zipigwazo na
kambi za magharibi na mashariki.
Hawa hawana ushahidi wa kuyathibitisha madai yao haya
bali kwa makusudi mazima wanataka kuipaka matope dini ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu; hawa ndio Mwenyezi Mungu anataumbia : "WANATAKA KUZIMA NURU YA
ALLAH (Uislamu) KWA VINYWA VYAO; NA ALLAH ATAKAMILISHA NURU YAKE IJAPOKUWA
WASHIRIKINA WATACHUKUWA" [61:8].
Tukifanya uchunguzi wa kiadilifu tutagundua kuwa
ustaarabu wa kimagharibi ndio unaomnyima haki na kumdhulumu mwanamke. Ikiwa
mwanamke anapoolewa huko katika ulimwengu wa kwanza (Ulaya) kwa watu
walioendelea kama wanavyodai ananyimwa hata haki ya kuitwa kwa jina la baba
yake mzazi bali ananasibishwa na familia ya mume aliyemuoa.
Kwa mfano mwanamke anayeitwa Vicky James akiolewa na
Michael Brown anaitwa Mrs Vicky Brown.
Ikiwa mwanamke huyu hapati haki ya kuitwa kwa jina la
baba yake aliyemzaa vipi unamtazamia kupata haki nyingine katika jamii hiyo ?!
Katika Uislamu, mambo ni kinyume kabisa na hivyo. Wakeze Mtume, ambaye kwa
mujibu wa imani ya kiislamu ndiye kiumbe bora kuliko wote hawakupata kuitwa
mathalan Bibi Muhammad bin Abdillahi, bali waliitwa kwa majina ya baba zao,
kama Bibi Aysha binti AbuBakri, Hafsa binti Umar, Zaynab binti Jahshi na
kadhalika. Katika hali kama hii utawasikia na kuwaona watu wenye fikra lemavu
waliorogwa na ukoloni mamboleo wakisema : Tunataka kuwa kama watu wa Magharibi.
Huu ni udumavu wa fikra na mawazo.
Hivi kumvua nguo mwanamke na kumuacha uchi mbele ya
kadamnasi ya watu katika kile kinachoitwa mashindano ya urembo, ndiko kumpa
haki na uhuru mwanamke ? Huu ndio ustaarabu na maendeleo tunayotaka kuyaiga
kutoka Magharibi ?! Je, kuja nyumbani kijana wa kiume na kumpiga busu mtoto wa
kike mbele ya wazazi wake na kisha kumchukua kokote atakako na kumrudisha
wakati autakao kwa madai ya uchumba na hili likapewa baraka zote za wazazi wa
binti. Kijana akishamtia binti mimba amkimbie na kumuacha aubebe mzigo huo peke
yake na kwenda kwenda kumtafuta kimwana mwingine na kustarehe naye na
kuendeleza uchafu wake. Je, huu ndio usawa, haki na uhuru anaopewa mwanamke na
ulimwengu wa magharibi na sisi tukataga kuuiga kibubusabubusa ? Haya si
maendeleo bali maondoleo ya utu na maadili mema, na hizi ni tabia na silka za
kinyama si za kibinadamu hata kidogo.
Huu ndio ukweli, tukikubali au kukataa. Uislamu haukuja
kumdhulumu, kumuonea na kumkandamiza mwanamke, bali umekuja kumkomboa kutoka
katika jahilia na kumpa haki zote anazostahiki kuzipata kama binadamu.
Hebu
tuhitimishe makala yetu haya kwa kuangalia mfano hai huu ambao unatoa
sura/picha ya uhuru kamili ya kujieleza na kuchangia fikra aliopewa mwanamke
chini ya mfumo sahihi wa maisha (Uislamu). Zama za ukhalifa(utawala) wa
Sayyidna Umar – Allah amuwie radhi – wanawake walikuwa wakiwatoza wanamume
mahari kubwa sana. Hali iliyopelekea baadhi ya wanamume wenye kipato duni
kushindwa kuoa.
Sayyidna Umar kama kiongozi mkuu wa dola ile ya kiislamu
aliliona tatizo hili na kujiona kuwa anawajibika kulitafutia ufumbuzi wa
haraka.
Akaamua kuitisha mkutano wa hadhara na kupiga marufuku
utozaji mkubwa wa mahari na badala yake akaweka kiwango maalum cha mahari. Hapo
ndipo aliposimama mwanamke mmoja na kusema : " Ewe Umar, ikiwa Mwenyezi
Mungu mwenyewe ameturuhusu kuchukua mrundi wa mali (mali nyingi isiyo na idadi)
vipi leo wewe unatuzuia na kutupiga marufuku kuchukua mali kidogo tu ? Hebu
jaribu kufikiri huyu ni kiongozi wa dola, anaambiwa maneno hayo mbele ya watu
na anayemwambia ni mwanamke, unafikiri alichukua hatua gani ? Sayyidna Umar
aliuheshimu uhuru wa kujieleza na haki ya kusikilizwa ya mwanamke huyu.
Akasalimu amri na kusema : Umar amekosea na mwanamke amepatia. Je, ni haki gani
zaidi ya hizi tunataka apewe mwanamke ?! Hebu mchukue mwanamke huyu na umlete
katika jamii yetu ya leo.
Je, atathubutu kufungua kinywa chake na kumwambia
kiongozi/mtawala maneno hayo ya kumkosoa mbele ya hadhira tena bila ya kuanza
kwa kumuita mtukufu/mheshimiwa raisi, akamuita kwa jina lake tu, na kiongozi
huyo akakiri mbele ya watu kuwa kweli kakosea ?! Hebu tuache chuki zetu na
tujaribu kuwa waadilifu na wakweli ili tuweze kuiona haki kuwa ni haki na
kuifuata na kuiona batili kuwa ni batili na tuiepuke.
KWA NINI
UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI
Haukuwa Uislamu ndiyo dini ya kwanza kuruhusu kuoa wake
wengi na wala Uislamu haukuzua utaratibu huu. Bali Uislamu umekuwa ndiyo dini
ya kwanza kuratibisha na kuyawekea utaratibu mzuri masuala ya ndoa. Isitoshe
Uislamu ukaliwekea suala la kuoa wake wengi masharti madhubuti na magumu, ambayo
Mume analazimika kuyazingatia kabla ya kuongeza mke/wake.
Suala la kuoa wake wengi halikuwa tu ni ada na desturi za
waarabu zama za jahiliya, bali pia ilikuwa ni desturi ya mataifa mbalimbali kwa
namna moja au nyengine, kama historia inavyokiri ukweli huu. Historia
inaonyesha kuwa hata hapa kwetu Tanzania, watemi (machifu) wa makabila mbali
mbali bali watu wa kawaida wenye mali walikuwa na wake wengi, huu ni ukweli
usiopingika. Utaratibu huu wa kuoa wake wengi ulikuwemo pia katika vitabu
vilivyotangulia Qur-ani Tukufu. Mna ndani ya Taurati maandiko na matukio
yanayouthibitisha ukweli huu na wala hamna ndani ya Injili aya/maandiko
yanayoharimisha kuoa wake wengi. Bali kuoa wake wengi kulizuiliwa na kanisa
katika karne ya kati {karne ya 10-15 AD} na wakati mwingine waliruhusiwa na
kanisa baadhi ya wafalme wakubwa kuoa wake wengi. Rejea vitabu vya historia ya
kanisa.
Uislamu umeruhusu kuoa wake wengi kwa sharti
isizidi idadi
yao wake wanne
Kufanya
uadilifu baina yao.
Tunasoma ndani ya Qur-ani Tukufu juu ya ruhusa hii :
"…. BASI OENI MNAOWAPENDA KATIKA WANAWAKE (maadam mtafanya uadilifu)
WAWILI AU WATATU AU WANNE (tu). NA MKIOGOPA KUWA HAMWEZI KUFANYA UADILIFU, BASI
(oeni) MMOJA TU, AU (wawekeni masuria) WALE AMBAO MIKONO YENU YA KUUME IMEWAMILIKI.
KUFANYA HIVYO NDIKO KUTAPELEKEA KUTOFANYA UJEURI." [4:3]
Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alimwambia Ghaylan
At-thaqafiy, ambaye alisilimu akiwa na wake kumi "Kaa na wanne (tu)
miongoni mwao na waache (wataliki) waliosalia" At-tirmidhiy, An-nisaai na
Ibn Maajah. Ni vema ikafahamika kwamba huyu Ghaylan alikuwa ndiye mtemi
(mfalme) wa Twaif.
Suala hili la kuoa wake wengi ni suala lililofanywa na
mwenyewe Bwana Mtume, maswahaba na waliokuja baada yao na ni suala ambalo umma
mzima wa kiislamu umekongamana juu yake. Sheria hii inayomruhusu mwanamume kuoa
zaidi ya mke mmoja ina maslahi na manufaa kwa wote wawili; mwanamume na
mwanamke. Kwa upande wa mwanamume :
Inawezekana
kabisa mkewe akawa hamtoshelezei haja yake ya maumbile. Hili husababishwa na
uwezo mkubwa wa mume katika tendo la ndoa na udhaifu wa mke. Mume hataki
kumuacha mkewe, sasa ataitosheleza wapi kiu yake ? Hapo ndipo uislamu
ukamruhusu kuoa mke mwingine na yule wa mwanzo kubakia pale pale. Lau uislamu
usingemruhusu mume huyu kuongeza mke mwingine ni dhahiri kuwa ili kukidhi haja
yake angefanya moja kati ya mawili. Ima angemtaliki huyu aliye naye, asiyekidhi
haja na kuoa mwingine au angekuwa na nyumba ndogo (mwanamke wa pembeni/kimada)
Kadhalika
mwanamke anaweza kuwa tasa; hazai na mume anatamani kupata watoto, ambalo hili
la kupata watoto ni mojawapo ya malengo na madhumuni ya ndoa. Lakini mume
anampenda mkewe na kwa sababu moja au nyingine hataki kumuacha. Sasa huyu mume
afanyeje ili aweze kupata watoto kuendeleza kizazi cha binadamu ? Akazae nje ya
ndoa ? Hapana, hilo ni kosa. Hapa ndipo sheria ikaizingatia haki ya huyu mume kupata
watoto na ikamruhusu kuoa mke mwingine ajaribu bahati yake. Huenda Mola wake
akamruzuku watoto kwa mke huyu.
Haya ni baadhi tu ya maslahi ya sheria hii ya kuoa zaidi
ya mke mmoja kwa upande wa mume. Hebu tuangalie mwanamke naye, ananufaika vipi
na sheria hii :
Inawezekana
kabisa mke akapatwa na maradhi; yakamsababishia kushindwa kabisa kuitekeleza
haki ya unyumba kwa mumewe. Maskini mke huyu mgonjwa, aende wapi na il-hali
sasa katika kipindi kigumu cha ugonjwa ndio anahitajia zaidi huruma, mapenzi na
liwazo la mumewe. Mumewe amtaliki ? La, hapana, sheria inambana mume kuwa
katika mkataba wa ndoa alichukua ahadi kuishi naye katika raha/shida,
uzima/ugonjwa, basi amuuguze mkewe na ili kukidhi haja zake za kimaumbile basi
na aoe mke mwingine, Je hapo mwanamke hajanufaika?
Kadhalika kama
ambavyo binadamu anavyotofautiana katika sura, akili, tabia na kadhalika. Ni
kama hivyo pia tunatofautiana katika uwezo/nguvu ya kujamiiana. Inaweza uwezo
wa mume ukawa ni mkubwa sana kuliko mkewe, mume ni tembo na mke ni kondoo, vipi
kondoo atahimili vishindo vya tembo ? Sasa, ili mke huyu asiichukie ndoa na
hatimaye kukimbia, uislamu ukamruhusu mume kuongeza mke mwingine. Siku za zamu
ya mke mwingine, huyu asiyehimili vishindo atapata kupumzika. Hebu tuwe wakweli,
mwanamke huyu kanufaika au la?
Vile vile sheria hii ina maslahi makubwa kwa jamii.
Hakuna jamii isiyokuwa na wajane na mayatima; ambao hawa wanataka wapate
uangalizi na malezi. Nani basi atawalea wajane hawa waliofiwa na waume zao na
hawa walioachwa na baba zao ? Hapo ndipo Uislamu ukampa ruhusa mwanaume ambaye
tayari ana mke, kuongeza mke mwingine. Pengine huyu atakayemuoa ni huyo mjane,
mwenye mayatima. Je hapo mwanamke huyu hajasitirika na wanawe ? Kwani huyu mume
atakuwa anawajibika kumhudumia yeye na wanawe. Waswahili husema ukipenda boga
penda na maua yake. Je, hapa jamii imenufaika au haikunufaika ?
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake duniani ni
kubwa kuliko idadi ya wanaume, kadhalika idadi ya wanyama jike ni kubwa kuliko
ya wanyama dume. Haya ni matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi mbali mbali
ulimwenguni kote. Sasa itakuwa tunakubaliana na takwimu hizi na leo vita
vimetapakaa duniani kote na wahanga (victims) wa vita hivi, wengi wao ni
wanaume kwa kuwa wao ndio askari wanaopigana vita. Hebu tuchukulie/tukadirie
kuwa uwiano wa wanaume na wanawake duniani 1:5 yaani mwanaume mmoja kwa
wanawake watano. Sasa ikiwa kila mmoja akioa mke mmoja hawa waliobaki waende
wapi, wakaolewe na nani ? Hawa pia ni binadamu, wanayo haki yao ya msingi ya kupenda
na kupendwa katika jamii. Wanayo matakwa yao ya kimaumbile, wakakidhi wapi haja
na hamu zao za kimaumbile ? Ni kwa kuzingatia hili ndio uislamu ukamruhusu
mwanaume kuoa mke zaidi ya mke mmoja kwa sharti ya kuwa awe muadilifu baina
yao.
Ni lazima tukubali kuwa kila sheria aliyotuwekea Mola
wetu mtukufu ina faida,maslahi na manufaa kwetu sisi waja wake. Akiamrisha au
kukataza ni kwa maslahi na faida yetu sisi wenyewe. Ni mamoja tumeyajua na
kuyaona maslahi na faida za amri au katazo hilo au hapana. Kushindwa kwetu
kuyajua maslahi na kuziona faida, hakuziondoshi faida na maslahi hayo na
kuyafanya yasiwepo, bali yatabakia pale pale. Huu ndio ukweli usiopingika.
Waislamu tumekuwa tukiwacha mafundisho ya dini yetu na kufuata mafundisho ya
shetani yaliyopitia kwa wanaojiita wanamaendeleo. Leo matatizo yanayotukuta
yanatokana na kuacha mafundisho ya Uislamu. Tukodolee macho wakati wa Mtume na
masahaba na tuone nia zao katika kuoa wake wengi, jinsi mwanamke wa kiislamu
alivyohifadhika, wajane wa vita pia nao hawakutupwa mkono, na Mtume –Rehema na
Amani zimshukie – ndiye aliyeanza kuonyesha mfano.
Je, tuna mfano mkubwa kuliko
wa Mtume wakati Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuamrisha tumfuate ? Tunafuata mkumbo
wa maadui wa kiislamu unaodai haki za wanawake na kushikilia kuoa mke mmoja,
pamoja na kuweka vimada, kumvunjia mwanamke heshima yake kwa kumvua nguo na
kumtumia kwenye matangazo ya biashara, madansa, miss world na kadhalika. Leo
mwanamke akiolewa ananyang’anywa hata jina la mzazi wake na kujulikana kwa jina
la mumewe, Mrs fulani, sasa ni nani anayemtakia mema mwanamke, Mwenyezi Mungu
aliyemuumba au wakazi wa dunia hii wakiongozwa na mwanaume ambaye yuko tayari
kufanya lolote kutekeleza matashi ya nafsi yake ???
KWA
NINI UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI
KWA
NINI UKWKWA
NINI UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI A
NINI UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI ISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI
KWA NINI UISLAMU UMERUHUSU KUOA WAKE WENGI
No comments:
Post a Comment