Friday, March 25, 2016

MUFTI WA TANZANIA AMUOMBEA DUA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM


MUFTI wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubery amemuombea dua, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Rais Dk. John Magufuli ili waweze kulitumikia vema taifa na kuliletea maendeleo.

Zubery alimfanyia dua hiyo Makonda Dar es Salaam leo asubuhi alipofika nyumbani kwake kujitambulisha na kumjulia hali pamoja na kumueleza mambo kadhaa ya maendeleo yaliyofanyika.

"Tunakuomba mola wetu kuwapa moyo wa imani na uzalendo na kuwaepusha na mabaya yote  Mkuu wetu wa Mkoa Paul Makonda, Rais wetu Magufuli pamoja na viongozi wote ili waliongoze taifa letu kwa amani" alisema Mufti Zubery"  wakati akiomba dua hiyo.

Makonda akizungumza na Mufti Zubery nyumbani kwake Mikocheni alimwambia kuwa kuna mambo kadhaa ameyafanya kwa kushirikiana na watendaji wenzake kwa kukutana na waendesha boda boda ili kuwawezesha kupata mkopo utakaowasaidia kupata vitendelea kazi zao kama kupata kofia ngumu mbili za kuvaa dereva na abiria wake ili kuwasaidia katika shughuli zao za kusafirisha abiria.

Makonda alitaja mambo mengine kuwa ni suala nzima la kupambana na uhalifu ambao bado unaonesha kupamba moto hasa ujambazi wa kutumia silaha za moto.

Alitaja mambo mengine kuwa ni mkutano alioufanya hivi karibuni wa kukutana na wenyeviti wa mitaa na maofisa watendaji ili kuzungumzia suala la utunzaji wa mazingira na mambo mengine ambapo alisema ameandaa mpango wa kumzawadia mwenyekiti atakayefanya vizuri kwenye mtaa wake.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum alisema jambo alilofanya Makonda la kumtembea Mufti ni jambo zuri na kuwa kumuona mufti ni sawa kama amewaona waislam wote nchini.

Alisema wanamuombea Makonda mungu amzidishie wepesi katika kazi zake kwani ni viongozi wachache wanaopata madaraka ambao uwakumbuka viongozi wa dini kama alivyofanya Makonda.

Katika hatua nyingine Makonda alifanya ukaguzi wa barabara kadhaa za Manispaa ya Kinondoni ambazo hivi karibuni aliagiza zifanyiwe marekebisho ikiwa ni pamoja na kuchimba mifereji baada ya kuharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

HISTORIA YA PASAKA

JE NI KWELI PASAKA NI SIKUKUU YA KUFUFUKA KWA YESU?



JE, NI KWELI PASAKA NI SIKUKUUYA  KUFUFUKA KWA YESU?
     Adhuhuri moja wakati nikiwa nyumbani alikuja jamaa yangu mmoja ambaye aliniletea bakuli maalum la kuhifadhia chakula. Ndani ya bakuli lile kulikuwa na wali na nyama ya kuku ambavyo kwa hakika vilinitamanisha sana hasa ukizingatia nilikuwa na njaa kali. Nikaona ule ndiyo wakati haswaa wa kujifaidia kile nilicholetewa.

      Baada ya kuutwanga wali ule ndipo nilipopatwa na shauku ya kujua Yule jamaa yangu alipata wapi ujuzi wa kupika wali mtamu namna ile na kumtayarisha kitaalamu, kuku yule wa kienyeji. Ndipo jamaa yangu aliponiambia kuwa chakula kile amekipika maalum kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya kufufuliwa kwa Yesu Kristo maarufu kwa jina la Pasaka.

       Kwa miaka mingi nimekuwa nikisikia kuhusu siku hiyo na ndipo baada ya kuambiwa vile na jamaa yangu, nilipoamua kuandika makala haya ili kuuelezea umma juu ya historia ya sikukuu hiyo na mwanzilishi wake na lengo la kuwepo kwake.

Historia ya pasaka
    Pasaka ni sikukuu iliyoanza kwa nabii Mussa, kumbuka kuwa wana wa Israel walikuwa utumwani nchini Misri chini ya utawala wa mfalme Firauni(Farao) takribani miaka 400 walikuwa wanateswa na mfalme Farao.

    Baada ya mateso ya muda mrefu mungu akamtoa Mussa na kumfanya kwa Nabii na akaamrishwa kwenda kupambanana na Farao ili awakomboe wana wa Israel na wawe huru.Ndipo Mussa akaenda kwa firauni na akafanikiwa kumshinda Farao.

     Baada ya Mussa kumshinda farao  akaondoka na wana wa Israel (wayahudi) akavuka nao katika bahari ya Shamu,Firauni naye alipojaribu kuvuka pamoja na jeshi lake aliangamizwa baharini.

      Baada ya mussa kuvuka salama na wana wa Israel mungu akawapa amri ya kufurahia kutoka utumwani na ndipo sikuku hiyo ya pasaka ilipoanzia hapo rejea katika kitabu cha kumbukumbu la torati 16:1-6)

“1 Utunzwe mwezi wa Abibu ukamfanyie pasaka Bwana mungu wako kwa kuwa ilikuwa mwezi wa Abibu alipokutoa misri usiku Bwana Mungu wako, 2 Nawe umchinjie pasaka Bwana Mungu wako katika kundi la kondoo na la ng’ombe mahali atakapochagua bwana apakalishe jina lake,3 Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu ,siku saba unakula naye mikate isiyotiwa chachu nayo ni mikate ya mateso kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka ili upate kukumbuka siku iliyotoka nchi ya Misri siku zote za maisha yako, 4 Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni kisilale chochote usiku kucha hata asubuhi,5 Usimchinjie pasaka ndani ya malango yako yote akupayo Bwana Mungu wako ,6 Ila mahali atakapochagua Bwana mungu wako apakalishe jina lake ndipo mtakapomchinjia pasaka jioni katika machweo ya jua kwa wakatika kama uliotoka misri”

    Baada ya kuangalia maandiko kutoka katika kitabu cha kumbukumbu la torati sasa tuangalie tena katika kitabu cha pili cha Nabii Musa kiitwacho “KUTOKA”

    Katika kitabu cha kutoka pia tunaona kuwa asili ya sikukuu ya pasaka ilianza kwa Nabii Mussa baada ya kutoka misri na wana wa Israel rejea Kutoka 12:42-51

“42 Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana kwasababu ya kawatoka katika nchi ya Misri ,huu ndio usiku wa bwana ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israel wote katika vizazi vyao, 43 Bwana akawaambia Mussa na Haruni Amri ya pasaka ni hii, mtu mgeni asimle 44 Lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha,ukiisha kutahiri ndipo hapo atamla pasaka.45 Akaaye kwenu hali ya ugeni na mtumishi aliyeajiliwa wasimle pasaka, 45 Akaaye kwenu hali ya ugeni na mtumishi aliyeajiliwa wasimle pasaka, 46 Na aliwe ndani ya nyumba moja ,usiichukue nje ya nyumba nyama yake yoyote wala msifunje mfupa wake uwao wote. 47 Na wafanye jambo hili mkutano wa Israel wote. 48 Na mgeni atakapoketi pamoja nawe na kupenda kumfanyia Bwana pasaka waume wake wote na watahiriwe ndipo hapo akaribie na kufanya pasaka ,naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi lakini mtu yeyote asiyetahiriwa asimle. 49 Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini. 50 Ndivyo walivyofanya wana wa Israel wote kama Bwana alivyowaagiza Mussa na haruni ndivyo walivyofanya. 51 Ilikuwa siku ile ile moja,Bwana akawatoa wana wa Israel katika nchi ya Misri kwa majeshi yao”(KUTOKA 12:42-51)

    Kwa maelekezo hayo hapo juu kutoka katika kitabu cha tano cha Mussa kiitwacho “KUMBUKUMBU LA TORATI” na kitabu cha pili cha Mussa kiitwacho “KUTOKA” moja kwa moja tunaona kuwa pasaka ni sikukuu iliyoanza wakati wa Nabii Mussa baada ya kuamriwa na Mungu wake kusheherekea pasaka pamoja na wana wa Israel kwa kuchinja Kondoo na Ng’ombe baada ya Mussa kufanikiwa kuwatoa wana wa Israel kutoka katika mikono ya mateso ya mfalme Firauni(Farao),Hivyo kwa maneno hayo moja kwa moja tunaona kuwa sikukuu ya pasaka si  kufufuka bwana Yesu kama baadhi ya wakristo wanavyodai 

    Jambo la kushangaza na kustaajabisha ni kuona baadhi ya watu hususani jamii ya Wakristo wakidai kuwa pasaka ni sikukuu ya kufufuka kwa Yesu wakati kwa mujibu wa vitabu vyao wanavyoviamini na kuvitumia kila siku vinakanusha suala la pasaka kuwa ni sikukuu ya kufufuka Bwana yesu.

     Baada ya kuona maandiko hayo hebu tuangalie je kweli bwana yesu alikufa na kufufua na je wanaosheherekea pasaka kuwa ni sikukuu ya kufufuka yesu wako sahihi?

LUKA 2:41-45  “Basi wazee wake huenda yerusalemu kila mwaka wakati wa sikuku ya pasaka.Na alipopata umri wa miaka kumi na miwili walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuuu.Na walipokwisha kutimiza siku wakati wa kurudi kwao,Yule mtoto yesu alibaki nyuma huko yerusalemu na wazee wake walikuwa hawana habari.Na wakadhani ya kuwa yumo katika msafara wakaenenda mwendo wa kutwa wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao.Na walipomkosa wakarejea Yerusalemu huku wakimtafuta”

     Kwa maelezo hayo hapo juu tunaona kuwa hata yeye mwenyewe yesu alikula sikukuu ya pasaka wakati akiwa mdogo na umri wake ulikuwa ni miaka kumi na miwili akiwa na wazee wake ambao walikuwa wakienda Yerusalemu kama ilivyokuwa desturi yao.

     Swali la kujiuliza hapo je ni nani alikufa na kufufuka ikiwa Yesu mwenyewe alikula pasaka akiwa na umri wa miaka kumi na miwili je kusema kuwa sikukuu ya pasaka ni kufufuka kwa Yesu je huyo ni yesu gani?
    Ukweli ni kwamba kusheherekea sikukuu ya pasaka ni kupoteza mwelekeo kwani sikukuu hiyo ya pasaka ni sikukuu ya wayahudi.

    Ushahidi unaothibitisha kuwa pasaka ni sikukuu ya wayahudi ni YOHANA 6:4 “Na pasaka sikuku ya wayahudi ilikuwa karibu”

     Nihitimishe makala hii fupi ya UKWELI KUHUSU PASAKA kwa maneno ya kitabu kitukifi cha QUR’AN pale ambapo ALLAH S W aliposema katika sura ya 4:157-158

    “Na kwaajili ya kusema kwao sisi tumemuua Masihi Isa mwana wa Mariamu mtume wa mungu hali hawakumuua wala hawakumsulubu bali walibabaishiwa (mtu mwingine wakamdhani Nabii Isa) Na kwa hakika wale waliokhitalifiana katika hiyo(ya kumuua Isa)wako katika shaka nalo (jambo hilo la kusema kauawa)wao hawana yakini juu ya jambo hili isipokuwa wanafuata dhana tu.Na kwa yakini hawakumwua. Bali Mwenyezimungu alimnyanyua kwake na Mwenyezimungu ni mwenye nguvu na mwenye hikima.

      Kwa aya hiyo ndipo ambapo tunaona kuwa Nabii ISSA(a.s) au YESU hakufa wala hakusulubiwa ila walifananishiwa tu hao mayahudi waliotaka kumsulubu na kumuua bwana Yesu.

    Hivyo kusheherekea sikukuu ya pasaka ni kufuata mila za wayahudi na watu wasio na dini.

Kwa kifupi huo ndio ukweli kuhusu pasaka na historia yake ambapo tumeona kuwa pasaka ilianza kwa Nabii Mussa pale alipoambia na Mungu wake aende kwa Firauni(Farao) akawaokoe wana wa Israel kutokana na mateso waliyokuwa wanayapata kutoka kwa mfalme Firauni(Farao) lakini pia tumeona kuwa pasaka ni sikukuu ya iliyokuwa inasheherekewa na mayahudi wa kipindi hicho.

     Nakuacha na swali hili; Kusema kuwa pasaka ni siku ya kufufuka kwa Yesu je ni Yesu gani huyo aliyekufa na kufufuka wakati yeye mwenyewe amekula pasaka?

Makala hii imeandaliwa na 
Adinani  H chorobi 0753-733217