KIMATAIFA

Mufti wa Libya aitaka serikali ipambane na vileo

Mufti wa Libya ameitaka serikali ya nchi hiyo kupiga marufuku vinywaji vyote vyenye kileo na madawa ya kulevya.
Sadiq Al-Ghiryani amewataka viongozi wa serikali ya Tripoli kukabiliana na uuzaji wa vileo hadharani na madawa ya kulevya nchi humo.

Al-Ghiryani amesisitiza juu ya ulazima wa serikali na viongozi wa Libya kupambana na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu na kuwataka Walibya wote wapambane na vitendo vilivyokinyume na mafundisho ya dini Tukufu ya Kiislamu, ukiwemo unywaji pombe na madawa ya kulevya.

Vilevile Mufti wa Libya amesema katika kuungana na familia dhidi ya vitendo viovu, serikali lazima ifunge mitandao yote ya internet ambayo inakinzana na maadili mema
.
Kwa mujibu wa sheria za Libya, ni marufuku kutumia vinywaji vyenye kileo na dawa za kulevya na adhabu kali inatolewa kwa makosa hayo.

Hata hivyo vileo na dawa za kulevya zimeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Libya kutokana na ukosefu wa usalama.

 

Hali ya tahadhari kati ya Lebanon na Israel

Jeshi la Lebanon limejiweka tayari kuanzia asubuhi ya leo kufuatia madai yaliyotolewa na utawala haramu wa Israel ya kudungua ndege isiyo na rubani katika anga ya mji wa Haifa inayodaiwa kumilikiwa na harakati ya Hizbullah.

Chanzo kimoja cha usalama katika jeshi la Lebanon kimesema kuwa, majeshi ya Lebanon yaliyoko katika mipaka ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo bandia yamewekwa katika hali ya tahadhari kubwa.

Chanzo hicho pia kimesisitiza kuwa, jeshi la Israel limeongeza idadi ya askari wake hususan katika maeneo ya mashariki ya Mazariu Shaba'a na karibu na lango la Fatwimah huko Kufru Kalaa na eneo la Ghajar na kando na eneo la Abbasiyyah nchini Lebanon.

Jeshi la utawala wa Kizayuni pia limeweka vifaru vya kivita aina ya Merkava katika maeneo kadhaa ya mpakani sambamba na kurusha idadi kadhaa ya ndege zake zizizo na rubani katika maeneo hayo.

Hapo jana jeshi la utawala haramu wa Israel lilitangaza kuwa, lilitungua ndege isiyo na rubani inayodaiwa kumilikiwa na harakati ya Hizbullah ya Lebanon karibu na bandari ya kaskazini mwa Haifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Hizbullah ya Lebanon imekanusha madai kuwa ilituma ndege isiyokuwa na rubani (drone) katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina huko Israel.

 

Misikiti yashambuliwa Iraq, wanne wauawa

Watu wanne wameuawa na makumi na wengine wakiwemo raia, askari polisi na wanajeshi wa Iraq kujeruhiwa hii leo Sambamba na kuendelea kwa mashambulizi ya kigaidi mjini Baghdad na maeneo mengine ya nchi hiyo.

Vyanzo vya usalama na hospitali nchini Iraq vimetangaza kuwa, mashambulizi hayo katika misikiti kadhaa mjini Baghdad yameua watu 4 na kujeruhi wengine 50.

Wakati huo huo, polisi ya Iraq pia imetangaza kutokea mlipuko mwingine katika msikiti ulio katika eneo la Al-Biyaau, kusini mwa mji mkuu Baghdad.

Weledi wa masuala ya kisiasa wameyataja mashambulizi hayo kuwa, yana lengo la kuzusha fitna za kimadhehebu kati ya Waislamu nchini humo

 

Al-Marzouqi: Hali ya hatari lazima ifutwe Tunisia

Rais Munsif Al Marzouqi wa Tunisia amesema kuwa, umewadia wakati wa kufutwa hali ya hatari liyoanza kutekelezwa mwaka 2011 nchini humo.

Akiashiria kwamba, kutekelezwa hali hiyo ya hatari nchini kumegharimu kiasi kikubwa cha nguvu kazi na fedha nyingi Rais wa Tunisia amesema, lazima hali hiyo ifutiliwe mbali ili askari waweze kutekeleza majukumu yao asili.

Itakumbukwa kuwa, mwanzoni mwa mwaka huu, Tunisia ilirefusha hali ya hatari kwa kipindi kingine cha miezi mitatu hadi mwezi Juni. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo,

kunapotokea hatari inayotishia usalama wa nchi au tukio lolote la hatari, kunapaswa kutangazwa hali ya hatari nchi nzima au katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

 

Watu 25 wauawa katika mapigano mapya Nigeria

 Mapigano mapya yaliyozuka kati ya askari usalama wa Nigeria na kundi la wanamgambo wa Boko Haram huko katika kijiji cha Jashwa kilichopo katika jimbo la Yobe kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, yamepelekea kuuawa watu wasiopungua 25. 

Mkuu wa polisi katika jimbo la Yobe Alhaji Sanusi Rufai amesema kuwa, kati ya watu hao waliouawa ni pamoja na wanamgambo 20 wa Boko Haram na askari 5 na kwamba, askari wengine wawali wamejeruhiwa na kulazwa hospitali.

Sanusi amesema kuwa, wanamgambo hao walivamia nyumba ya kiongozi wa benki moja iliyopo jimboni hapo na kuiba pesa zote zilizokuwemo.

Wakati huo huo, msemaji wa polisi ya Nigeria amesema kuwa, katika mapigano hayo askari usalama wa nchi hiyo wamefanikiwa kudhibiti aina mbalimbali za silaha na mabomu ya kurusha kwa mkono na magari matatu vilivyokuwa vikidhibitiwa na wanamgambo hao.

 

Hizbullah yakanusha madai ya kutuma 'drone' Israel 

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imekanusha madai kuwa imetuma ndege isiyokuwa na rubani (drone) katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina huko Israel. Jeshi la utawala haramu wa Kizayuni jana lilitangaza kuwa, limetungua ndege isiyo na rubani inayodaiwa kumilikiwa na harakati ya Hizbullah ya Lebanon karibu na bandari ya kaskazini mwa Haifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Msemaji wa Jeshi la utawala huo alisema kuwa, ndege hiyo ilitambuliwa ikiwa katika anga ya Lebanon katika umbali wa kilometa nane kutoka pwani ya magharibi mwa Haifa na kudondoshwa na jeshi la Israel.
Katika upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon amesema kuwa harakati ya Hizbullah haiingilii masuala ya Syria. Adnan Mansour amesema kwamba, askari wa Hizbullah wapo kwenye vijiji vya mpaka wa Lebanon kwa ajili ya kulinda Walebanoni wa eneo hilo na wala hawashiriki katika operesheni za kijeshi ndani ya Syria.

 

 

UN yaafiki kupelekewa vikosi vya kimataifa Mali

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura na kuafiki kupelekwa askari na polisi 12,600 wa kimataifa nchini Mali baada ya wanajeshi wa Ufaransa na wa nchi za Kiafrika kuondoka nchini humo ili kupambana na waasi.  Kikosi hicho kitajulikana kama Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kurejesha Uthabiti nchini Mali (MINUSMA) na unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Julai ambapo kikosi hicho kitakuwa na askari 11,200 na polisi 1,400.  Inatarajiwa kuwa Ufaransa itaanza kuondoa wanajeshi wake nchini Mali mwishoni mwa mwaka huu lakini askari 1,000 watabakia kwa madai ya kukabiliana na mashambulizi ya makundi yenye silaha.
Tieman Hubert Coulibali Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali amesema kupitishwa azimio hilo ni hatua muhimu katika mwenendo wa kupambana na harakati za makundi ya kigaidi  na waasi nchini humo

 

Mbeki: Sudan na waasi wa SPLM-N wanahitilafiana

Mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo kati ya Sudan na waasi wa SPLM tawi la Kaskazini amesema kuwa kuna hitiliafu baina ya pande hizo mbili. Thabo Mbeki rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye alifanya mazungumzo na pande hizo mbili katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa amesema kuwa, pande hizo zinahitilafiana kwa kiasi kikubwa. Mbeki ameongeza kuwa, ujumbe wa serikali ya Sudan unataka kuanza mazungumzo juu ya suala la usalama na kwamba suala hilo ndio msingi wa mwenendo wa amani, katika hali ambayo waasi wanataka kuanza kuzungumzia masuala ya kibinadamu na haki za binadamu. Hata hivyo Mbeki amesisitiza kufanya jitihada za kukurubisha mitazamo ya pande hizo mbili.
Hayo yalikuwa mazungumzo rasmi ya kwanza na ya moja kwa moja kati ya serikali ya Khartoum na waasi wa SPLM tawi la kaskazini, kwa lengo la kuhitimisha  migogoro katika majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kusini. 

 

Mawaziri wa EAC waidhinisha bajeti ya jumuiya hiyo

Jumla ya dola za Kimarekani milioni 117 zimetengwa kwa ajili ya bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha wa 2013-14 na kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri la jumuiya hiyo kwenye kikao chake kilichofanyika mjini Arusha, Tanzania.
 Mbali na bajeti hiyo mkutano huo ulioanza kwa kikao cha ngazi ya wataalamu na kufuatiwa na mkutano wa makatibu wakuu wa nchi wanachama ulijadili ajenda zitakazozungumziwa katika mkutano wa itifaki ya umoja wa fedha wa jumuiya hiyo utakaofanyika Novemba 15 mwaka huu. Katika mkutano huo kutajadiliwa pendekezo la kuongeza wigo wa mamlaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuiimarisha zaidi jumuiya hiyo na kuwafaidisha raia wa nchi wanachama.



Mholanzi aliyeuuzia silaha za kemikali utawala wa Saddam afungwa jela

 Mahakama ya Uholanzi imemuhukumu mfanyabiashara Frans van Anraat  raia wa Uholanzi adhabu ya kifungo cha miaka 16 jela na kumlipa kila mtu aliyefungua mashtaka dhidi yake wakiwemo raia wa Kiirani na Kiiraqi kiasi cha euro elfu ishirini na tano , baada ya kupatikana na hatia ya kuuzia utawala wa Iraq mada za kemikali. Taarifa zimeeleza kuwa, raia 13 wa Kiirani na wanne wa Kiiraqi ndio waliofungua mashtaka na kesi hiyo kusikilizwa kwa muda wa miaka miwili. Mfanyabiashara huyo wa Kidachi wa mada za kemikali alitiwa mbaroni mwaka 1989, na baada ya hapo alifanikiwa kutorokea  nchini Iraq na kuishi nchini humo kwa muda wa miaka 14  kwa kutumia jina la kubuni. Kwa mujibu wa sheria za Uholanzi, mfanyabiashara Frans van Anraat ana muda wa miezi mitatu ya kukata rufaa kama hakubaliani na  hukumu aliyopewa. Katika kipindi cha miaka ya 1985 hadi 1989, utawala wa Saddam Hussein wa Iraq ulipiga mabomu ya kemikali kwenye maeneo ya mpaka wa Iran na Iraq, ikiwemo mji ya Sardasht wa Iran na Halabcheh, ulioko nchini Iraq. Kwenye mashambulio hayo ya mabomu ya kemikali maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wasiokuwa na hatia waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa na baadhi yao hadi leo hii wanakabiliwa na machungu na mateso yaliyosababishwa na mabomu hayo. Inaonekana kuwa ni jambo la nadra kushuhudiwa tukio kama hili la kufunguliwa mashtaka na kupandishwa kizimbani mfanyabiashara wa Kiholanzi kwa kosa la kuuza silaha za kemikali kwa utawala wa Saddam Hussein. Lakini swali linaloulizwa hapa ni je, inatosha tu kuchukuliwa hatua kama hizo kwa jinai zilizofanywa dhidi ya binadamu, na kusema kwamba katika ulimwengu wa Magharibi unaojinasibu kuwa mtetezi wa haki za binadamu zinaweza kupatikana taasisi za kushughulikia ipasavayo jinai hizo? Lakini maafa hayo ni makubwa kwa kiasi ambacho hayawezi kufidiwa kwa kutolewa hukumu ya kulipwa fidia za kiasi fulani cha mamia ya maelfu ya euro kwa wahanga wachache tu wa silaha za kemikali. Taarifa zinasema kuwa, zaidi ya mashirika 400, mengi kati yao yakiwa ni ya Kimagharibi yaliupatia utawala wa Saddam Husssien silaha za kemikali katika vita vya miaka minane vya kulazimishwa, vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, na kupelekea zaidi ya watu laki moja kuuawa shahidi  au kujeruhiwa. Hadi sasa hakuna hatua zozote za kimataifa zilizochukuliwa dhidi ya mashirika hayo ambayo yamekuwa yakipata uungaji mkono wa nchi za Magharibi. Kadhia hiyo inaonyesha kuwa, serikali za Magharibi zimekuwa zikikwepa kumtuhumu mtu au kufungua mashtaka kwenye mahakama, huku zimekuwa zikionyesha kuwa zinapinga suala la uzalishaji na utumiaji wa silaha za mauaji ya halaiki, katika hali ambayo nchi hizo zenyewe ni wazalishaji na wauzaji wakubwa wa silaha hizo duniani na zimekuwa hazitekelezi  makubaliano ya kimataifa katika uwanja huo. Makubaliano ya kuzuia utumiwaji wa silaha za kemikali CWC yalipitishwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika tarehe 3 Septemba mwaka 1992 baada ya kupita miaka 20 ya mazungumzo, na baada ya hapo iliundwa Taasisi ya Kuzuia Silaha za Kemikali OPCW mwaka 1997 kwa lengo la kutekelezwa kipengee cha makubaliano ya The Hague nchini Uholanzi. Ilipangwa kuwa, tarehe 29 Aprili 2012 nchi hizo zitekeleze makubaliano yao kwa kuangamiza silaha zao; lakini kwa kitendo chao cha kukwepa kutekeleza makubaliano hayo itibari na makubaliano hayo yote pia yamekuwa hatarini. Kwa hakika madola yenye nguvu kwa kusaini makubaliano hayo au kwa kuendesha mahakama kama hizo, yenyewe yanataka kujionyesha kuwa ni yenye kupinga usambazaji wa silaha za mauaji ya halaiki, lakini wakati huohuo yamekuwa yakizalisha na kuuza silaha hizo katika maeneo yenye migogoro duniani, ili yaweze kujiimarisha kiuchumi na kufikia malengo ya siasa zao haramu.   

 

 

Uokoaji wa manusura waendelea Bagladesh

 Shughuli za uokoaji zinaendelea ili kuwatafuta mamia ya watu ambao bado hawajapatikana, baada ya jengo kuporomoka nchini Bagladesh na watu wasiopungua 273 kupoteza maisha yao. Maafisa wa nchi hiyo wanasema kwamba, watu 40 wameokolewa wakiwa hai tangu Jumatano baada ya jengo hilo kuporomoka karibu na mji mkuu Dhaka, mlimokuwa na karakana za ushoni wa nguo. Habari zaidi zinasema kuwa mamia ya watu bado wamekwama chini ya vifusi na huenda idadi ya vifo ikaongezeka. Waziri Mkuu wa Bagladesh Sheikh Hasina ametaka nchi nzima kuomba dua maalumu kwa ajili ya wahanga wa tukio hilo. Hii ni katika hali ambayo maelfu ya wananchi wameandamana nchini humo kupinga ujenzi holela wa majengo bila kuzingatiwa viwango vya usalama. Matukio ya kuporomoka au kushika moto majengo mjini Dhaka sio mageni.  Mwaka jana zaidi ya wafanyakazi 112 walifariki dunia baada ya kiwanda chao kushika moto na mwanzoni mwa mwaka huu takriban watu 10 walipoteza maisha baada ya jengo moja kuungua.

 

 

A. Kusini yapasisha sheria ya kulinda siri za Bunge

 Wabunge wa Afrika Kusini hatimaye wamepasisha muswada uliozusha ubishani kwa miaka mitatu kuhusiana  na kulindwa siri za Bunge.  Sheria hiyo imepigiwa kura za ndiyo na wabunge 187, wengi wao wakiwa wa chama tawala cha ANC na kupingwa na wabunge 74 pamoja na vyama vya upinzani.  Sheria hiyo inadhamiria kulinda taarifa muhimu kwa maslahi ya taifa na masuala ya biashara. Lakini wanaopinga wanasema kuwa, sheria hiyo hata hivyo haiwalindi watakaofichua baadhi ya machafu serikalini kama vile ubadhirifu wasifikishwe kwenye vyombo vya sheria. Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Democratic Alliance (DA) kimesema kupasishwa sheria hiyo ni kinyume cha katiba na kumtaka Rais Jacob Zuma airejeshe Bungeni ili ifanyiwe marekebisho.

 

No comments: