Tuesday, July 23, 2013

WAISLAMU NDIO WATU WAKARIMU ZAIDI UINGEREZA



Gazeti la Times linalochapishwa nchini Uingereza limeitaja dini tukufu ya Kiislamu kuwa ni dini yenye kutilia umuhimu mkubwa suala la  kuwalingania watu katika kutoa walichonacho na kwamba wafuasi wa dini hiyo tukufu ndio watu wakarimu zaidi kati ya wananchi wa Uingereza.
 
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na gazeti la Times kwa kushirikiana na kituo cha mawasiliano cha 'Just Giving' kwa watu elfu nne nchini Uingereza unaonyesha kuwa, Waislamu nchini humo ni wakarimu zaidi kuliko wafuasi wa dini nyingine. 

Imeelezwa kuwa, Waislamu wamekuwa wakitoa misaada yao ya kibinadamu kupitia taasisi  kama vile 'Islamic Relief'  na 'Muslim Aid' kwa watu wenye kuhitaji misaada na pia hupeleka misaada kwa taasisi zisizokuwa za Kiislamu kama vile taasisi za kusaidia wagonjwa wa  maradhi ya saratani nchini humo.

Friday, July 19, 2013

Makundi ya mapambano ya Palestina yapinga mazungumzo na Israel



Makundi mbalimbali ya Palestina yaliyokutana na Rais wa Mamlaka ya Ndani yamepinga pendekezo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry la kuanza tena mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mazungumzo hayo ambayo yalianzishwa tena mwaka 2010 chini ya upatanishi wa Marekani, yalikwa muda mfupi baada ya kuanza kutokana na uamuzi wa Israel wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina.
Viongozi wa makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina walitangaza  baada ya kikao cha jana mjini Ramallah kwamba mpango wa amani uliopendekezwa na John Kerry haukubaliwi na Wapalestina kwa sababu umebuniwa kwa maslahi ya Israel.
Mwakilishi wa kujitegemea katika bunge la Palestina Mustafa Barghuthi amesema makundi mengi yaliyoshiriki kwenye mkutano huo yamepinga pendekezo la Kerry kwa ajili ya kuanza tena mazungumzo ya mapatano. Ameongeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alishindwa kutoa dhamana ya kusimamishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina wala kueleza msingi wa mazungumzo hayo.
Amesema mpango wa Kerry haukuashiria hata kidogo suala la kuundwa dola huru la Palestina katika mipaka ya mwaka 1967.
Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya PLO Wasil Abu Yusuf ambaye pia ameshiriki katika mkutano huo amesema, mazungumzo ya mapatano kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni hayawezi kuwa na faida yoyote maadamu Israel inakataa kutambua rasmi haki za taifa la Palestina. Amesema viongozi wa makundi ya mapambano ya Palestina wameunda kamati maalumu itakayotayarisha mependekezo mbadala na kuyakabidhi kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Msemaji wa Harakati ya Hamas Sami Abu Zuhri pia amesema, kuanza tena mazungumzo eti ya mapatano kutainufaisha Israel na kuficha uhalifu na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala huo haramu dhidi ya wananchi wa Palestina. Msemaji wa Hamas amezitaka nchi za Magharibi ziunge mkono mapambano ya ukombozi ya wananchi wanaokandamizwa wa Palestina badala ya kuishinikiza serikali ya Mamlaka ya Ndani ili irejee katika meza ya mazungumzo yasiyo na tija.
Wakati huo huo Ali Faisal ambaye ni mjumbe wa ofisi ya harakati ya Kidemokrasia kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina amesema safari ya sasa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mashariki ya Kati ni katika juhudi za kuishinikiza zaidi Mamlaka ya Ndani ya Palestina ili ikubali masharti ya Wazayuni. Faisal ameongeza kuwa, katika safari zake zote kwenye eneo hili, John Kerry amekuwa akiwashinikiza Wapalestina na Waarabu kwa ujumla ili wakubali kushirikiana na Israel.
Katika muda wote wa safari yake huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu Kerry hakulaani au hata kukemea jinai zinazoendelea kufanya na Israel dhidi ya wananchi wa Palestina au ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina. Hii ni pamoja na kuwa sambamba na safari ya Waziri wa  Mambo ya Nje wa Marekani huko Palestina, Israel imetoa kibali cha ujenzi wa nyumba 1200 katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki.  

Ramadhani yapandisha bei za vyakula Tanzania

Bei za vyakula katika mwezi huu wa Ramadhani zinaripotiwa kupanda nchini Tanzania hususan katika jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya vyakula ambavyo hutumiwa na Waislamu kama futari zinaonekana kupanda mno katika masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Taarifa zaidi zinasema, maeneo ya Dar es Salaam kama Tabata Kimanga, Bima na hata Segerea yanashuhudia bidhaa za vyakula zikiwa juu ukilinganisha na maeneo ya Kariakoo, Vingunguti na hata Magomeni.
Bidhaa kama magimbi, viazi zinadaiwa kupanda kutokana na ugumu wa upatikanaji wake katika masoko. Baadhi ya wafanyabiashara wanasema, kwa kipindi hiki mahitaji ni makubwa kuliko upatikanaji wa bidhaa, na kwamba, hali hii imesababishwa na mvua kutokunyesha kwa wakati na kusababisha uhaba wa mavuno.
Aidha katika mikoa mingine ya Tanzania pia kumeripotiwa kupanda bei za vyakula vya mwezi wa Ramadhani kama mihogo, magimbi, viazi na maboga.
Baadhi ya wafanyabiashara pia wamekuwa wakilangua kwa makusudi vyakula wakifahamu kwamba, katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani bidhaa hizo zinahitajika sana.

Sunday, July 14, 2013

BAKWATA ARUSHA YALALAMIKIA UTENDAJI WA POLISI



Baraza Kuu la Waislamu nchini Tanzania BAKWATA limelalamikia jinsi wahusika wa mashambulizi yanayotokea mara kwa mara dhidi ya masheikh mkoani humo wasivyofuatiliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Malalamiko hayo yametolewa na Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Sheikh Abdallah Masoud kufuatia shambulio la juzi la mtu asiyejulikana dhidi ya Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Sheikh Said Juma Makamba aliyejeruhiwa vibaya kwa kumwagiwa maji yanayosadikiwa kuwa ni tindikali. 

Sheikh Makamba ameshambuliwa na mtu asiyejulikana akiwa nyumbani kwake jijini Arusha.

Akilaani tukio hilo, Sheik Abdallah Masoud amesema, ameshitushwa sana na tukio hilo na kusisitiza kuwa linafanana na shambulizi alilofanyiwa Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Abdulaziz Jonjo ambaye mwaka jana aliripuliwa kwa bomu akiwa amelala nyumbani kwake.

Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha amesema, matukio hayo yamekuwa yakijirudia huku wahusika wakishindwa kutiwa mbaroni na kusisitiza kwamba, pamoja na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, lakini wamekuwa hawapati taarifa za kukamatwa watuhumiwa licha ya kwamba amesema wanajulikana.

Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru baada ya kujeruhiwa vibaya maeneo ya usoni, kifuani, mkononi na mgongoni.

Naye  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amesema, polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo ingawa hadi sasa hakuna  mtu anayeshikiliwa kuhusishwa na shambulio hilo.