Makundi mbalimbali ya Palestina yaliyokutana na Rais wa Mamlaka ya Ndani yamepinga pendekezo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry la kuanza tena mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mazungumzo hayo ambayo yalianzishwa tena mwaka 2010 chini ya upatanishi wa Marekani, yalikwa muda mfupi baada ya kuanza kutokana na uamuzi wa Israel wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina.
Viongozi wa makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina walitangaza baada ya kikao cha jana mjini Ramallah kwamba mpango wa amani uliopendekezwa na John Kerry haukubaliwi na Wapalestina kwa sababu umebuniwa kwa maslahi ya Israel.
Mwakilishi wa kujitegemea katika bunge la Palestina Mustafa Barghuthi amesema makundi mengi yaliyoshiriki kwenye mkutano huo yamepinga pendekezo la Kerry kwa ajili ya kuanza tena mazungumzo ya mapatano. Ameongeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alishindwa kutoa dhamana ya kusimamishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina wala kueleza msingi wa mazungumzo hayo.
Amesema mpango wa Kerry haukuashiria hata kidogo suala la kuundwa dola huru la Palestina katika mipaka ya mwaka 1967.
Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya PLO Wasil Abu Yusuf ambaye pia ameshiriki katika mkutano huo amesema, mazungumzo ya mapatano kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni hayawezi kuwa na faida yoyote maadamu Israel inakataa kutambua rasmi haki za taifa la Palestina. Amesema viongozi wa makundi ya mapambano ya Palestina wameunda kamati maalumu itakayotayarisha mependekezo mbadala na kuyakabidhi kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Msemaji wa Harakati ya Hamas Sami Abu Zuhri pia amesema, kuanza tena mazungumzo eti ya mapatano kutainufaisha Israel na kuficha uhalifu na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala huo haramu dhidi ya wananchi wa Palestina. Msemaji wa Hamas amezitaka nchi za Magharibi ziunge mkono mapambano ya ukombozi ya wananchi wanaokandamizwa wa Palestina badala ya kuishinikiza serikali ya Mamlaka ya Ndani ili irejee katika meza ya mazungumzo yasiyo na tija.
Wakati huo huo Ali Faisal ambaye ni mjumbe wa ofisi ya harakati ya Kidemokrasia kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina amesema safari ya sasa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mashariki ya Kati ni katika juhudi za kuishinikiza zaidi Mamlaka ya Ndani ya Palestina ili ikubali masharti ya Wazayuni. Faisal ameongeza kuwa, katika safari zake zote kwenye eneo hili, John Kerry amekuwa akiwashinikiza Wapalestina na Waarabu kwa ujumla ili wakubali kushirikiana na Israel.
Katika muda wote wa safari yake huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu Kerry hakulaani au hata kukemea jinai zinazoendelea kufanya na Israel dhidi ya wananchi wa Palestina au ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina. Hii ni pamoja na kuwa sambamba na safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani huko Palestina, Israel imetoa kibali cha ujenzi wa nyumba 1200 katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki.
No comments:
Post a Comment