Wednesday, April 24, 2013

Wakuu wa Kenya na Ethiopia wajadili bandari ya Lamu

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo amekutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Haile Dessalegn mjini Nairobi.
Kenyatta na Dessalegn wamejadili kuhusu njia za kutekeleza mradi wa Bandari ya Lamu na Ukanda wa Mawasiliano wa Sudan Kusini na Ethiopia LAPSSET. Mradi huo mkubwa unatazamiwa kugharimu shilingi trilioni 1.5 na utafungua njia za mawasiliano na biashara katika eneo hilo. Rais Kenyatta amesema mradi huo ni kwa manufaa ya nchi zote za eneo.
Akizungumza na waandishi habari katika Ikulu ya Rais mjini Nairobi, Kenyatta amesema mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Ethiopia pia yalihusu mchakato wa amani Somalia. Viongozi hao wawili pia wameahidi kuunga mkono juhudi za ujenzi mpya wa Somalia.
Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika amesema nchi yake inataka kuwa na uhusiano mzuri na nchi za eneo. Dessalegn ndio kiongozi kwa kwanza kutembelea rasmi Kenya baada ya kuapishwa Rais Kenyatta wiki mbili zilizopita. Kesho Alkhamisi Rais Kenyatta anatazamiwa kushiriki katika shughuli ya kwanza rasmi nje ya Kenya wakati atakapojiunga na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wa kilele mjini Arusha, Tanzania.


No comments: