Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu
Amiri Manento, amelituhumu Jeshi la Polisi nchini kuwa linawabambikiza
kesi wananchi na kutumia nguvu nyingi kupita kiasi zinazosababisha vifo
vya raia wasiokuwa na kosa.
Alisema jeshi hilo limeshindwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na
taratibu katika utendaji wa kazi wa kila siku na kwamba hatua hiyo
inayochangia kuwapo kwa matukio ya mauaji ya raia katika maeneo
mbalimbali nchini.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye Jukwaa la Asasi za
Kiraia zinazopinga adhabu ya kifo na kusisitiza kuwa polisi wanakiuka
maadili katika utendaji wao wa kazi. Alisema polisi wanaokiuka maadili
ya kazi, lakini hawajawahi kuchukuliwa hatua zinazostahili na kwamba
hali hiyo imekuwapo kwa kipindi kirefu.
Jaji Manento alilitaka jeshi hilo kufanya kazi kwa kufuata sheria za
nchi na kwamba yeye na tume yake kazi yao ni kuhubiri amani na kwamba
hawana mamlaka kisheria ya kukamata mtu yeyote.
Kuhusu Tanzania kufuta adhabu ya kifo, Jaji Manento alisema jambo hilo
linahitaji muda na kwamba haiwezekani likafanyika kwa mara moja na
kumalizika.
“Huwezi kuamka asubuhi na kusema umefuta adhabu ya kifo, badala yake uwe
ni mchakato wa muda mrefu ambao mwisho wake utasaidia kuifuta na
kuondokana nayo,” alisema.
Akizungumzia mauaji yanayofanywa na wananchi dhidi ya wenzao, Jaji
Manento alisema tatizo hilo linatokana na watu kutokuwa na kazi maalum
za kufanya na kwamba vijijini zinapofanyika shughuli za kilimo takwimu
za mauji zipo chini ikilinganishwa na mijini.
Aliitaka jamii kujisikia vibaya mtu mmoja anapopoteza maisha kwa namna
yoyote ile na kwamba ikifikia hapo inaweza kupunguza mauaji yanayofanywa
na raia wenye hasira.
Kuhusu jamii kubadilika na kutii sheria, Jaji Manento alisema tume yake
kwa kipindi kirefu imekuwa ikizunguka nchi nzima kutoa elimu ya namna
hiyo ingawa bado vitendo viovu vinaendelea kufanyika maeneo mbalimbali
nchini.
Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Harold Sungusia, alisema adhabu ya kifo imeendelea
kutolewa nchini licha ya kuwa tangu mwaka 1994, marais hawajawahi kutia
saini ili waliohukumiwa wanyongwe.
Alisema hukumu ya kifo ni miongoni mwa sheria mbaya zinazotakiwa kufutwa
kwa kuwa haitoi fundisho kwa mhusika badala yake inaongeza maumivu.
Aliongeza kuwa umefika wakati serikali kuwa na adhabu mbadala badala ya
kifo kwa kuwa tangu imeanza kutolewa tatizo halijaweza kumalizika katika
jamii na kwamba matukio ya mauaji yameendelea.
Mmoja wa mtu aliyehukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama Kuu na kuachiwa
huru na Mahakama ya Rufaa, Michael Lembeli, alisema alikamatwa na polisi
akiwa kidato cha nne mwaka 1994 na kubambikwa kesi ya mauaji. Alisema
siku aliyokamatwa polisi walifika nyumbani kwao wakimsaka mpangaji wao
waliyedai kamba aliiba mito ya makochi na baada ya kumkosa wakamkamata
yeye, lakini cha kushangaza alipofika kituoni aliambiwa ameua ofisa wa
Jeshi.
Alisema licha ya kubambikiwa kesi hiyo, lakini pia alipigwa na
kulazimishwa kukubali kuandika maelezo polisi kwamba ameua ili aachiwe
huru. Alisema baada ya kuyaandika, yalitumika mahakamani kama ushahidi
na hivyo kumfanya atiwe hatiani na kuhumiwa kifo na Mahakama Kuu Kanda
ya Tabora.
No comments:
Post a Comment