Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), amekabidhi uthibitisho wa takwimu
zinazoonyesha kuwa deni la Taifa linaongezeka kwa sababu matumizi ya
serikali yanazidi mapato ya ndani.
Mpina aliwasilisha takwimu hizo jana baada ya kipindi cha mwaswali na
majibu bungeni kwa kurejea bajeti ya mwaka jana wa fedha ambapo
alimuomba mwongozo Naibu Spika, Job Ndugai, aeleze kama majibu ya Naibu
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, kwamba matumizi ya serikali
hayazidi mapato ya ndani yanakidhi kanuni ya Bunge ya 46.
Kanuni ya 46 (1) inasema: “Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa
kujibu swali hilo kwa ukamilifu kama alivyoulizwa, isipokuwa kama jibu
linalohusika ni refu au lina takwimu nyingi, waziri atampa mbunge
muuliza swali nakala ya jibu mapema baada ya kikao kuanza kabla ya muda
wa kujibu swali hilo haujafikiwa.”
Alisema katika kipindi cha maswali na majibu, Aprili 16, mwaka huu,
alipouliza swali la nyongeza lililohusu deni la Taifa, alisema moja ya
sababu inayofanya deni la Taifa kuongezeka ni serikali kuwa na matumizi
makubwa kuliko mapato ya ndani.
“Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, alisema hatukopi fedha kwa ajili ya
matumizi ya ndani, tunakopa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo
akanitaka nihakikishe kama takwimu zangu ziko sawa sawa. Nataka
kukuhakikishia Mheshimiwa Naibu Spika kuwa takwimu zangu ni sahihi,”
alisema.
Aliongeza: “Leo nimekuja na kitabu cha waziri cha bajeti ya mwaka
2012/2013 ambapo mapato yetu ya ndani yalikuwa Shilingi trilioni 9.1
wakati matumizi yetu ya kawaida yalikuwa Shilingi trilioni 10.6 kulikuwa
na pungufu ya Shilingi trilioni 1.5.”
Alisema misaada iliyoipata nchi katika bajeti ya mwaka jana, ilikuwa ni
Sh. bilioni 878.4 na kwamba fedha zilizopungua katika bajeti hiyo
zilifidiwa na fedha za kukopa.
Alisema kwa msingi huo matumizi ya serikali ni makubwa kuliko mapato ya ndani.
No comments:
Post a Comment