Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, amemtaka Dk. Chami
kutambua kwamba Rais Jakaya Kikwete ni kiongozi wa Watanzania wote,
hivyo utekelezaji wa ahadi zake hauingiliani na matakwa ya kisiasa.
Gama akizungumza na NIPASHE jana alisema Rais anapotekeleza ahadi
alizoahidi haangalii jimbo fulani ni la mpizani au mbunge wa chama
tawala bali jambo la msingi linaloangaliwa ni umuhimu wa kuhudumia
wananchi wote.
“Siyo kweli kwamba kuna barabara zinazopendelewa, nasema habari ya
kuingiza masuala ya siasa katika mambo haya siyo sahihi, barabara zote
zilizoahidiwa na Rais zitajengwa kwa utaratibu ambao umepangwa na
serikali,” alisema Gama.
Alisema wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wasiwe na wasiwasi kwani
barabara zikishatengenezwa hata kama zipo katika jimbo linaloongozwa na
mbunge wa Chadema, lakini watapita wananchi wa vyama vyote.
Gama alisema mwaka 2010 Rais aliahidi barabara sita katika
majimbo yaliyopo Mkoa wa Kilimanjaro ambazo baadhi zimeanza kutengenezwa
na nyingine zipo katika mchakato.
Alisema barabara ya Rau madukani-Mamboleo hadi Kishumundu
inayolalamikiwa na mbunge kwamba imekuwa ikikarabatiwa kwa kuwekwa
kifusi licha ya kwamba ilijengwa kwa lami ipo chini ya Halmashauri na
mafungu ya kuitengeneza yamekuwa yakitolewa na halmashauri husika.
“Mbunge (Dk. Chami) ni mjumbe wa Bodi ya Barabara ya mkoa, hivyo
masuala mengine yanatakiwa yazungumzwe kwenye vikao, na katika suala la
utekelezaji wa ahadi hatuangalii miaka, mfano zipo barabara ambazo
ziliahidiwa wa Rais mstaafu, Benjamini Mkapa, ambazo zinatekelezwa na
Rais Kikwete,” alisema Gama.
Hatua ya serikali kutoa kauli hiyo imefuatia Dk. Chami kuandika
barua kwenda Wizara ya Ujenzi akilalamikia ujenzi wa barabara ya lami
katika Jimbo la Hai.
Katika barua yake kwenda kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge
ya Febrauari 4, mwaka huu, Chami anatoa mfano wa barabara ya Rau
Madukani-Mamboleo-Kishumundu iliyopo Kata ya Uru Mashariki ilijengwa kwa
kiwango cha lami mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Chami alisema barabara hiyo tangu wakati huo, ikiharibika
haikarabatiwi kwa kurudishia lami bali hujazwa kifusi kitu ambacho
anadai ni kinyume na taratibu za ukarabati wa barabara za kiwango cha
lami.
Alisema hali hiyo ni tofauti katika barabara ya Machine Tools
kwenda Machame iliyopo Hai iliyojengwa miaka ya 1950 ambayo Wakala wa
Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro kila inapoharibika
hukarabati kwa kurudishia lami.
Chami katika barua yake alisema kinachoongeza utata ni barabara ya
Machine Tools-Machame iko katika Jimbo la Hai ambalo linaongozwa na
Chadema.
Alisema viongozi wa Chadema wanawakejeli wananchi wa Moshi Vijijini
walioichagua CCM kuwa barabara yao (watu wa Hai) ya Machame
inakarabatiwa kwa lami kwa sababu wao waliichagua Chadema na kwamba
kinachoifanya barabara hii ya Moshi Vijijini ijazwe kifusi ni kwa sababu
waliichagua CCM.
Chami amebainisha kuwa kutokufanya hivyo ni kutoa kipaumbele zaidi kwa Chadema kuliko maeneo yanayoongozwa na CCM.
No comments:
Post a Comment