Tuesday, April 30, 2013

Polisi watoana kafara Liwale

Vurugu za kuchomeana nyumba zilizowakumba wakazi wa Wilaya ya Liwale, zimemtoa kafara aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani humo (OCD), Lucian Ngoromela, habari zikisema kuwa ameng’olewa na kurudishwa makao makuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi.

Mbali na hatua hiyo, kuna madai kuwa huenda akahojiwa ili aeleze kwa nini athari za tukio hilo zimekuwa kubwa kiasi hicho.

Hatua ya kumuondoa OCD Ngoromela Liwale imechukuliwa baada ya kubainika kuwa siku ya tukio (usiku wa kuamkia Aprili 24, mwaka huu), simu yake ya mkononi haikupatikana hadi kesho yake, kitendo ambacho kinadaiwa kilitoa mwanya kwa wahalifu kuchoma nyumba 20 ikiwamo ofisi ya serikali iliyokuwa ikitumiwa na Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo (CCM).

Mbali na nyumba hizo, katika tukio hilo pia maduka 11 yalivunjwa na mali kuporwa huku trekta ndogo tano aina ya Powertiller zikiteketezwa kwa moto.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE lililokuwa limepiga kambi mjini humo, unaonyesha kuwa hatua ya kumng’oa OCD Ngoromela inalenga kurudisha imani ya wananchi wa wilaya hiyo kwa Jeshi la Polisi.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kikao cha pamoja kati ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga; Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulega; Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Ephreim Mbaga na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mungulu.

Uchunguzi umeonyesha kuwa, wavamizi walianza kuchoma nyumba ya mbunge iliyopo kijiji cha Kingolowira Kata ya Nangando saa 2:30 usiku na waliendelea hadi alfajiri ya Aprili 24 bila hatua zozote kuchukuliwa na Jeshi la Polisi.

Habari zinasema kuwa wachomaji hao walikuwa wakisikika wakisema ‘tukimaliza kuchoma nyumba hii twende katika nyumba ya fulani’ na kwamba walifanya hivyo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa kukosekana kwa mawasiliano kulisababisha polisi kurundikana kituo cha polisi ili kulinda fedha zilizowasilishwa hapo na viongozi wa vyama vya ushirika baada ya wakulima wa korosho kukataa kupokea malipo ya nyongeza ya Sh. 200 badala ya Sh. 600 yaliyoahidiwa kutolewa awali.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulega, alipoulizwa na NIPASHE kuhusu taarifa za uhamisho wa ghafla wa OCD Ngoromela, alithibitisha na kusisitiza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kwa nia njema ikiwamo kutafuta amani ya kudumu wilayani humo.

Mapema akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mji wa Liwale, Ulega alisema pamoja na kasoro mbalimbali zilizobainika katika mfumo wa stakabadhi ghalani, pia uasi umechangiwa na baadhi ya viongozi wa serikali kushindwa kuwajibika kwa wakati.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Mwakajinga, alithibitisha kwa kuwa OCD Ngoromela, amehamishiwa makao makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi.

No comments: