Uongozi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TAN/Met) umetaja sababu mbalimbali
zinazowafanya baadhi ya walimu kuacha kazi pamoja na kutoripoti kwenye
vituo wanavyopangiwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao huo, Mary Soko, alisema
hayo jana alipokuwa akitoa salam kwenye Maadhimisho ya Wiki ya
Uhamasishaji Elimu Duniani, ambayo kitaifa yanafanyika kwa juma moja
mkoani Lindi.
Akiwasilisha salamu za mtandao huo, Soko alisema baadhi ya walimu
wanalazimika kuacha kazi na kutafuta ajira zingine kutokana changamoto
mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo maslahi duni na mazingira duni, na
kutothaminiwa kwa kazi wanazozifanya.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni, kutopatiwa motisha na vifaa na zana
muhimu za kufundishia na kujifunzia na kukosekana kwa mazingira mazuri
ya kuishi.
Aliwasisitiza Watanzania wakiwemo wa mkoa wa Lindi kuendeleza mijadala
na makongamano kuhusu elimu ili kubaini matatizo yanayoikabili sekta
hiyo hapa nchini.
Akizindua maadhimisho hayo kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk, Shukuru Kawambwa, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Dk. Nassoro
Hamidi, alisema kwa mwaka 2012 na 2013 serikali imeajiri walimu 26,460,
kati yao 13,527 ni wa shule za awali na msingi, wakati 12,933 ni wa
shule za sekondari.
Hata hivyo, alisema kati ya walimu 743 waliopangwa mkoani Lindi katika
kipindi cha mwaka 2012 na 2013 walioripoti kwenye vituo vyao vya kazi ni
509 tu, huku 234 wakiwa hawajulikani walipo.
No comments:
Post a Comment