Friday, April 26, 2013

Waziri Maghembe hoi

                                                     Bajeti yake yaondolewa bungeni
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiteta na Waziri wa Maji, Profesa Jumann Maghembe kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma,Aprili 25,2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesitisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe, Jumatano wiki hii kutokana na karibu ya wabunge wote waliopata fursa ya kuchangia juzi na jana kutoiunga mkono.
 Kutokana na hali hiyo, Spika Makinda ameipa serikali siku tano, kuanzia jana kuhakikisha inapeleka bungeni majibu ya uhakika kuhusiana na tatizo la ufinyu wa bajeti hiyo lililosababisha wabunge kuipinga. Uamuzi wa Spika Makinda umechukuliwa saa chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kusema anaweza kuliomba Bunge
kupata fursa ya kuangalia namna serikali itakavyoweza kuboresha baadhi ya maeneo katika bajeti hiyo kutokana na maoni na ushauri uliotolewa na wabunge.
Pinda alisema hayo wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, bungeni jana.
 Katika swali lake la msingi, Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai, alisema wabunge walio wengi wamelalamika kuwa hazikukokotolewa fedha za kutosha katika kukabiliana na tatizo la maji nchini.
 Hivyo, akahoji kwanini serikali isiondoe bajeti hiyo na kwenda kuifumua upya ili kutafuta fedha kwa ajili ya kuwezesha Watanzania kupata maji?
 Wabunge hao, ambao wengi wao ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walipinga bajeti hiyo, wakisema ni finyu, ambayo haiwezi kukidhi mahitaji makubwa na ya muda mrefu ya maji yaliyoko nchini kote, hususan maeneo ya vijijini.
 Katika bajeti hiyo, Waziri Maghembe ameliomba Bunge liidhinishe Sh. 398,395,874,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka huo wa fedha.
 Mjadala huo ulitarajiwa kuhitimishwa jana jioni. Hata hivyo, kutokana na wabunge hao kuendelea kutoiunga mkono katika kikao cha Bunge cha jana asubuhi, Spika Makinda, aliamua kusitisha mjadala kuendelea, akisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona bajeti hiyo ikipingwa na wabunge wengi.
Aliiagiza Kamati ya Bajeti, Wizara na Maji na Hazina, kukutana ili kuangalia namna watakavyolipatia ufumbuzi tatizo la ufinyu wa bajeti hiyo linalolalamikiwa na wabunge.
 Pia aliitaka serikali kuhakikisha inapeleka majibu ya uhakika bungeni Jumatatu ijayo.
 Miongoni mwa wabunge waliochangia mjadala huo na kupinga ni  Gosbert Blandes (Karagwe-CCM) akipinga kutotekelezwa kwa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kupeleka maji Karagwe.
 Alisema anasikitishwa kuona Sh. bilioni 30 zimetengwa kwa ajili ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Mwanga anakotoka Waziri Maghembe, lakini ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kupeleka maji katika Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera, ambayo haihitaji fedha nyingi, hadi sasa haijatekelezwa.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama limesababisha watoto katika baadhi ya Kata za jimboni mwake; kama Ndeisinyai na Shambalai, kupinda miguu.
 Kutokana na hali hiyo, alishauri fedha za posho zilizotengwa kwa ajili ya vinywaji katika wizara hiyo ziondolewe na kupelekwa kusaidia katika miradi ya maji.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugola, alisema bajeti ya wizara hiyo ni sawa na mchezo wa karata tatu, ambao Watanzania wanaliwa kwa kutumia karata ya rangi nyekundu, hivyo haoni sababu ya kuiunga mkono, kwani imesheheni miradi isiyotekelezeka.
 Alisema kuna upendeleo unaofanywa na serikali kwa mawaziri katika masuala ya maendeleo, hivyo akaomba pia wabunge nao wapewe upendeleo huo.
 Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Clara Mwituka, alisema kama kuna upendeleo, ambao mawaziri wanafanyiana, basi anaomba pia ufanywe katika Jimbo la Newala linalowakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, kwani kuna tatizo kubwa la ukosefu wa maji.
 “Kuna maeneo hakuna maji hata ya kunawa uso,” alisema Mwituka.
 Mbunge wa Longido (CCM), Michael Lekule Laizer, alisema kutokana na tatizo la ukosefu wa maji, katika Wilaya ya Longido imefikia hatua baadhi ya familia wanapotaka kuoga wanapeana zamu.
 “Leo baba akioga kesho mama,” alisema Laizer na kuonya kuwa kama itafika mwaka 2015 maji yakaendelea kukosekana hajui nini kitakachotokea. Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nywangwine, alisema haungi mkono bajeti hiyo kwa sababu jimboni kwake wananchi hawaogi kabisa kutokana na kutokuwa na maji.
 Alisema ni aibu  kwa nchi kama Tanzania, ambayo imesheheni mito na maziwa, lakini bado inakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji, hivyo akamtaka Pinda kuhakikisha usiku wa kuamkia jana anatafuta fedha ili kupatia ufumbuzi.
Nywangwine alisema ni aibu kuona nchini Kenya maji yanamwagika na Tanzania ikiambulia aibu ya kuyakosa.
  Alisema maji yanayopatikana na kutumiwa na wananchi ni yale yanayofanana na ugoro au juisi, huku wakiwa wamesheheni maziwa na mito, lakini hayawanufaishi hata kidogo.
 Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, alisema kama ambavyo mwaka jana hakuunga mkono bajeti ya wizara hiyo, mwaka huu pia hataiunga mkono na kwamba, atapeleka hoja binafsi bungeni kuhakikisha wataalamu wote katika Wizara ya Maji wanaondoka.
 “Kuna watu walithubutu wakafanikiwa kama Mheshimiwa Lowassa katika mradi wa Ziwa Victoria. Hivi kweli tunajali kuwa maji ni uhai?” alihoji Shabiby.
 Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrodi Mkono, alisema haungi mkono bajeti hiyo kwa kuwa ni muda mrefu sasa amekuwa akisimama bungeni na kupiga kelele kuhusu tatizo la maji katika maeneo mengi jimboni kwake, lakini hakuna linalotekelezwa.
 “Waasisi wa taifa waliweka msingi wa kupata maji. Ahadi ya tangu mwaka 1974 haijatekelezwa na kila siku nasimama. Kwanini niunge mkono hoja?  Sioni sababu. Miaka 12 wananchi wangu wanalia kwa maji. Kwa nini niunge mkono hoja hii? Sioni sababu,” alisema Mkono.
 Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema anaungana na wabunge waliokataa kuunga mkono bajeti hiyo, kutokana na fedha zilizotengwa kutokidhi mahitaji ya upatikanaji wa maji.
 Alisema licha ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2005-2010 na 2010-2015 kuwaahidi Watanzania kuwa ifikapo 2010 asilimia 65 vijijini na asilimia 90 mijini watakuwa na maji safi na salama, hakuna lolote lililotekelezwa.
 Hivyo, akasema haamini kabisa kama ahadi iliyotolewa na Pinda, bungeni jana itatekelezwa.
 Alisema licha ya Rais Kikwete kuahidi tatizo la maji kwamba, litakuwa historia, hakuna lolote lililotekelezwa, hivyo akasema iwapo ufumbuzi hautapatikana, wananchi wa Dar es Salaam wataendelea kuandamana kwenda ofisini kwa Waziri Maghembe.
 Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Rose Kamili Sukum, ambaye naye alikataa kuunga mkono bajeti hiyo, alisema hawezi kusema maji yasipelekwe katika Wilaya ya Mwanga wala Same, lakini akasema utaratibu wa kuyapeleka katika wilaya hizo haukuwa sahihi, kwani fedha zilizopelekwa huko ni nyingi, hivyo akataka zigawanywe na kupelekwa katika maeneo mengine, ambako tatizo la maji pia lipo.
 Alisema kwenye hotuba ya Waziri Maghembe aliahidi kukamilika kwa visima vitano katika kila kijiji, lakini hadi sasa mradi huo haujakamilika.
 Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alisema atamshangaa mbunge atakayeunga mkono bajeti hiyo na kuwaomba wananchi kutomrudisha bungeni.
 Alisema Waziri Maghembe amelidanganya Bunge kwa kusema kuna Kijiji cha Kasanumba kilichopelekewa maji wakati hakipo, hivyo akawaomba wabunge wa CCM kuikataa bajeti hiyo.
 Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati, alisema anakubaliana na wabunge wengine kuhusu tatizo la maji kwamba, ni kubwa sana nchini, hivyo akashauri ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) kutotegemewa sana.
 Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji Luckson Mwanjale, alisema tatizo la maji ni kubwa na kwamba hakuna mbunge anayeweza kusema jimboni kwake ni salama.
 Dk. Christina Ishengoma (Viti Maalum-CCM) alisema maji safi na salama bado ni changamoto kubwa sana, hasa vijijini, hivyo akaishauri serikali ijipange kutatua tatizo hilo.
 Mbunge wa Nyang’hwale (CCM), Hussein Amar, alisema tatizo la maji limesababisha kifo jimboni kwake kufuatia ugomvi uliozuka baina ya wanawake wawili walipokuwa wakiyagombea.
 Alisema tatizo hilo pia limesababisha kukithiri kwa mimba, ndoa kuvunjika na wanafunzi kushindwa mitihani.
 Amar alisema kwa muda mrefu amekuwa akipigia kelele tatizo la maji bila ufumbuzi, na kwamba jimbo lake lina matatizo makubwa ya maji, huku maji yakiwa yamewazunguka, hivyo akasema haoni sababu ya kuunga mkono bajeti hiyo.
 Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Stella Manyanya, alisema hawezi kuwa kinyume cha wabunge waliopiga kelele kuhusu tatizo la maji.
Alisema hata ukiongea na wananchi nini kipaumbele chao, wanaume watakuambia elimu, lakini wanawake watakuambia maji na afya na kuwa katika maeneo ya vijijini, hata katika zahanati, ambako kinamama wanakojifungulia, hakuna maji safi na salama.
Mbunge wa Manyoni Magharibi (CCM), John Lwanji, alisema Tanzania imepata misaada mingi kutoka kwa wafadhili katika eneo la maji, lakini tatizo hilo bado ni sugu.
 Lwanji alisema tangu mwaka 1961 tatizo la upatikanaji wa maji bado limekuwa sugu, hivyo akasema haungi mkono bajeti hiyo.
 Mbunge wa Solwa (CCM), Ahmed Ali Salum, alisema haungi mkono bajeti hiyo na kushauri kuvunjwa kwa vyombo vyote vinavyosimamia maji na kuunda chombo kimoja, mkoani Shinyanga.

 WAZIRI MKUU ASINYWE MAJI YA CHUPA
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alisema kuanzia sasa katika ziara zote za viongozi wakuu wa serikali; akiwamo Waziri Mkuu, wasiandaliwe maji ya kunywa ya chupa, bali yale yanayotumiwa na wananchi wa kawaida na kusema haungi mkono bajeti hiyo.
 Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse, alisema miradi ya maji inayofadhiliwa na WB iko hoi na haiwezi kuwasaidia Watanzania, kwani sehemu yake kubwa imekuwa ikiliwa na baadhi ya wakandarasi, ambao alisema wanapaswa kuogopwa kama ukoma.
 AnnaMaryStella Mallac (Viti Maalum-Chadema), alisema anashangazwa kuona kufikia leo miaka 50 ya Uhuru, kinamama wanachota maji kwa kutumia kichwa, kwa kuinama na kutumia maji yanayofanana na togwa.
 Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka miwili, wabunge kukataa kuunga mkono bajeti za serikali zinazowasilishwa bungeni.
 Mara ya kwanza, wabunge waliikataa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, William Ngeleja, mwaka juzi, kwa maelezo kwamba, serikali ilikosa umakini katika kuiandaa.
 Wiki mbili baadaye, wabunge waliikataa pia bajeti ya Wizara ya Uchukuzi iliyowasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Omar Nundu, kwa maelezo kwamba, ilikuwa ni ndogo isiyokidhi mahitaji ya kukarabati miundombinu ya reli, ambayo hutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.

No comments: