Mamilioni
ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam huenda wakakabiliwa na uhaba wa
kitoweo kufuatia hatua ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
(Nemc) kuyafunga machinjio ya Ukonga.
Nemc
imeyafunga machinjio hayo yaliyoko eneo la Ukonga Mazizini katika
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, baada ya kubaini kuwa yanaendesha
shughuli zake katika mazingira machafu yanayohatarisha afya za walaji wa
nyama.
Machinjio
hayo ambayo ng’ombe kati ya 350 hadi 500 huchinjiwa hapo, yamefungwa
baada ya maofisa wa Nemc wakiongozwa na Afisa Mwandamizi Mkuu wa baraza
hilo, Lucy Lugusha, kufanya ziara ya ukaguzi wa kushtukiza katika eneo
hilo.
Maofisa
hao walifika katika machinjio hayo jana majira ya asubuhi na kumkuta
Afisa Mfawidhi wa Machinjio ya Ukonga, Pradisius Mbita, ambaye pia ni
mtumishi wa Manispaa ya Ilala akiwa katika ofisi za wamiliki wa
machinjio hayo.
Kabla
ya kuanza ukaguzi, Mbita aliulizwa na maofisa wa Nemc kuna mahusiano
gani kati ya Manispaa ya Ilala na machinjio hayo na kueleza kuwa
manispaa imekuwa ikikusanya ushuru tu na kwamba kuna watumishi ambao
wameteuliwa rasmi kufanya kazi katika machinjio hayo.
Mbita
alisema watumishi wa manispaa ambao wanafanya kazi katika machinjio
hayo yaliyoanzishwa tangu mwaka 1972, ni pamoja na yeye mwenyewe (Mbita)
kama mkaguzi wa nyama, afisa afya, mhasibu na mlinzi.
Alipoulizwa
kama machinjio hayo yana leseni, Mbita alisema manispaa haina uhakika
kama kuna leseni yoyote iliyokatwa kwa ajili ya kuendesha machinjio
hayo.
Baada
ya maofisa hao wa Nemc kuendelea kumhoji Mbita, alijitetea kuwa masuala
mengine ni ya ndani zaidi, hivyo ni bora akamwita mmoja wa wamiliki wa
machinjio hayo ayajibu.
Baada
ya nusu saa, mmoja wamiliki wa machinjio hayo, Philemon Bereko,
aliwasili eneo hilo na kueleza kuwa machinjio hayo yanamilikiwa na watu
watatu ambao ni Philemon Bilia, Anthony Bilia na yeye mwenyewe (Bereko).
Bereko
ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa wachinja Nyama, alisema
kama ilivyo kwa Nemc, nao wamekuwa wakipata malalamiko kutoka kwa
wananchi kuhusu mazingira machafu ya machinjio hayo.
Alisema
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alishawahi kufika katika machinjio hayo
baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi na aliahidi kuwa
halmashauri itatoa fedha zinazotokana na ushuru unaotozwa katika
machinjio hayo kwa ajili ya kusaidia kuboresha mazingira.
Bereko
alisema tangu Mkurugenzi wa Manispaa alipondolewa, ahadi hiyo imekwama
kutekelezwa badala yake halmashauri hiyo imekuwa ikiendelea kukusanya
ushuru wake wa Sh. 2,500 kwa kila ng’ombe mmoja anayechinjwa katika
machinjio hayo.
“Halmashauri
wameweka hadi mhasibu wao hapa, kila ng’ombe anayechinjwa ushuru
unaotozwa ni Sh. 2,000 na Sh. 500 ni za mkaguzi wa nyama ambaye anatoka
halmashauri, mazingira haya wanayaona na mvua ikinyesha hali inakuwa
mbaya sana,” alisema Bereko.
Hata
hivyo, alipoulizwa inakuwaje machinjio hayo yaendeshwe na watu binafsi
halafu halmashauri ichangie kuyaboresha, alisema hayo ni katika
makubaliano yao na kwamba kinachomsikitisha ni hatua ya halmashauri
kuweka mhasibu katika machinjio hayo wakati katika maeneo mengine hakuna
utaratibu kama huo.
Baada
ya kikao hicho, maofisa wa Nemc walianza ukaguzi wa machinjio hayo na
kujionea hali ya kutisha ya uchafu wa mazingira katika eneo hilo ambayo
yanahatarisha usalama kwa mlaji wa nyama inayochinjwa.
Miongoni
mwa mambo yaliyobainika ni mamia ya tani za kinyesi cha ng’ombe ambacho
kimerundikana, mifereji ya kupitishia maji yaliyochanganyika na damu
kutitirika katika mtaro wa maji unaounganishwa katika mto ambao
unaingiza maji kwenye Bahari ya Hindi na kupita kando kando ya makazi ya
watu.
Pia
mazizi ya kuhifadhi ng’ombe kabla hazijachinjwa yamejaa maji machafu
yaliyochanganyika na kinyesi kiasi kwamba ng’ombe akiwa humo huzama
miguu.
Maofisa
wa Nemc walipofika eneo la machinjio na kufanya ukaguzi saa 5:45
asubuhi, hapakuwapo na nyama, lakini nzi na funza walionekana kutokana
kukithiri kwa uchafu.
Baada
ya kujionea hali hiyo, Afisa Mwandamizi Mkuu wa Nemc, Lugusha, alitoa
agizo la kusitisha shughuli za uchinjaji nyama katika machinjio hayo
hadi hapo mazingira ya usafi yatakapoboreshwa.
“Mchana
wa leo (jana), tutakuletea barua rasmi ya kukutaka usitishe shughuli za
kuchinja nyama katika machinjio haya na nakala tutapeleka Halmashauri
ya Manispaa ya Ilala,” alisema Lugusha.
Hata
hivyo, Bereko alijitetea kwamba apewe muda wa mwezi mmoja au wiki moja
arekebishe mazingira hayo, lakini ombi lake lilikataliwa na maofisa wa
Nemc ambao walimweleza kuwa aanze kazi ya kuboresha mazingira na
akimaliza ndipo ataruhusiwa kuendelea na uchinjaji.
No comments:
Post a Comment