Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera
(Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wakati akitoa kauli ya Serikali
bungeni kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo
ya Kidato cha Nne alisema kuwa, wameagiza Baraza la Mitihani Tanzania
(Necta) kuweka viwango ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi zao.
Uamuzi huo wa Serikali umetokana na matokeo mabaya
ya mitihani ya mwaka jana, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi
walipata alama sifuri.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati
tofauti jana, wadau hao walisema kuwa licha ya wahusika kujiuzulu
wanatakiwa pia kushtakiwa kutokana na uzembe wa makusudi.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema kuwa
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anatakiwa
kufukuzwa kazi na kushtakiwa kutokana na matokeo hayo mabaya.
Alisema haitoshi Dk Kawambwa kujiuzulu au
kufukuzwa kazi, bali pia anatakiwa kushtakiwa kwa matokeo hayo,
yaliyosababisha pia mauaji ya wanafunzi wanne, aliyosema hayakutokea kwa
bahati mbaya, bali ni mpango maalumu ulioandaliwa na watendaji wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
“Kwa maneno aliyoyatoa, Waziri (Dk Kawambwa)
wakati wa kukataa hoja yangu, haitoshi kujiuzulu tu, angekuwa anajificha
asionekane hadharani kwa sababu ni aibu,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Kuna watu wanatakiwa washtakiwe kwa kusababisha
maafa haya. Matokeo haya hayakutokea kwa bahati mbaya yaliandaliwa kwa
makusudi, ni wauaji hawa!”
Aliionya Serikali kutochezea akili za Watanzania na kwamba familia za waliopoteza maisha kwa matokeo hayo zipewe kifuta jacho.
Mbatia aliongeza kuwa, taarifa alizonazo ni kwamba
kutokana na matokeo hayo mabaya ya mtihani, baadhi ya wasichana
wamekata tamaa na kuolewa.
Februari mwaka huu, mbunge huyo aliwasilisha hoja
binafsi bungeni, akitaka kuundwa kamati teule kutafuta ufumbuzi wa
matatizo ya elimu nchini akieleza sababu kuwa hakuna mitalaa tangu
Tanzania ipate uhuru na ipitie sera za elimu nchini. Hata hivyo, hoja
hiyo ilipingwa na Serikali ikidai kuwa kuna mitalaa inayokidhi viwango.
Alisema wanafunzi wanafahamishwa shuleni kuwa
daraja D ni kuanzia alama 21 hadi 40; C kuanzia alama 41 hadi 60; B
kuanzia 61 hadi 80 na A kuanzia 81 hadi 100, lakini Baraza la Mitihani
Tanzania (Necta) lilibadili mfumo huo bila waraka wowote.
1 comment:
KWANN IWE KAWAMBWA WAKATI BARAZA LA MITIHANI LIPO KWANN ISIWE NDALICHAKO
Post a Comment