Sunday, May 5, 2013

Madiwani waunda timu kumwona Waziri Mkuu

Madiwani wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wameunda  timu  ya kukutana na Waziri Mkuu kutafuta muafaka wa wakazi wa Kigamboni zaidi ya 100 waliobomolewa nyumba zao na kusababisha familia zao kulala nje.

Azimio  hilo limefikiwa  kwenye kikao chao kilichofanyika juzi  baada ya kutolewa taarifa ya hali mbaya  inayowakabili wananchi hao wa mtaa wa Minondo kwa kukosa mahema ya kulala,chakula na maji.

Diwani wa Kata ya Somangila, Aisha Mpanjila wakati akitoa taarifa hiyo, alikiambia kikao hicho kuwa kama haijachukuliwa hatua za haraka ya misaada, maisha ya wananchi hao yatakuwa hatarini.

Kwa muda wa wiki tatu sasa, wananchi hao wanalala nje baada ya nyumba 37 kubomolewa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupisha ujenzi wa nyumba za wastaafu wa majeshi ya ulinzi na usalama na viongozi wa serikali.

Diwani wa Tandika, Zena Mgaya, alisema suala hilo limewaumiza watu wengi kutokana na bomoabomoa hiyo kutojali  utu wa mtu.

Alisema, timu hiyo itakuwa na majukumu ya kukutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa ajili ya kuwanusuru wananchi hao kufunguliwa njia ya kupatiwa misaada ya kibinadamu.

"Tuwe na chembe ya huruma kwa watu hawa wakiwamo wanawake na watoto wanaotaabika na kukosa mahema na chakula, tumueleze Waziri Mkuu kwamba tumechoka na atoe ruhusa ya kufikiwa kwa watu hawa haraka," alisema.

Hata hivyo, Aderson Chale, diwani wa Kijichi, alisema jeuri inayofanywa na wizara hiyo inasababisha wananchi kuchukia serikali yao, ambapo alishauri pamoja na kukutana na Pinda, time hiyo ijadili na kukataa kuachia kata tatu kuingizwa katika mradi wa mji mpya wa Kigamboni.

Baada ya kauli za madiwani hao, Meya wa Manispoaa hiyo, Maabad Hoja alitangaza kuundwa kwa timu hiyo itakayoongozwa na Naibu Meya na kuagiza kuanza kazi ya kutekeleza azimio hilo kuanzia Jumatatu (kesho).

Ubomoaji wa nyumba hizo ulifanyika Aprili 22 mwaka huu majira ya  saa 9 usiku hadi saa 12 alfajiri chini ya ulinzi wa polisi wa kutuliza ghasia (FFU) na askari mgambo wa jiji.

Toka tukio hilo litokee, hakuna kiongozi yoyote wa serikali aliyekwenda eneo hilo kuangalia athari iliyotokea, badala yake Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile ndiye kiongozi pekee aliyejitokeza kwenda kuwajulia hali.
 

No comments: