Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, amesema serikali ina mpango
wa kuanzisha mahakama ndogo zitakazoshughulikia kesi ndogo pekee kama
vile matatizo ya wamachinga na wizi mdogo, ili kutoa kupunguza
mlundikano wa kesi.
Aidha, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, imeshauri Serikali iangalie
uwezekano wa kubadili mfumo wa uandishi wa Sheria zake na kuziandika
katika lugha nyepesi inayoeleweka kiurahisi kiwa ni pamoja na kuondokana
na maneno magumu ili kuwawezesha wananchi kuzielewa kiurahisi.
Waziri Chikawe aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akikabidhiwa
taarifa ya mapitio ya mfumo wa madai Tanzania na tamko la Sheria za
Kimila.
Kuhusu ripoti alizokabidhiwa, Chikawe alisema atazisoma kwa kina na
kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotokea kwa kuzingatia maslahi ya
Watanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa tume hiyo, Aloybius Mujuliz, alisema
wakati wakifanyia kazi marekebisho ya mfumo huo wa madai na tamko la
sheria za mila walipata fursa ya kuhusisha wananchi ambao walianzisha
mapungufu yanayogusa mfumo wa usimamizi wa haki katika kesi za madai
nchini na kutoa mapendekezo.
Alisema kati ya mapendekezo hayo ni pamoja na wananchi hao kutaka mfumo
wa uandishi wa sheria hizo ubadilishwe ili wapate fursa ya kuzisoma na
kuzielewa sheria zote zinazogusa haki na maslahi yao.
Aidha, alisema wananchi wengi walilalamika kuwa Sheria nyingi
zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza, lugha ambayo inazungumzwa na
wachache hivyo wengi wao wanashindwa kuzielewa.
No comments:
Post a Comment