Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la
mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la
Olasiti Jijini Arusha. Tukio hilo la kigaidi limesababisha mtu
mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa. Rais Kikwete analaani
vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu katili, waovu na
wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu wake.
Rais Kikwete ameagiza vyombo vya
usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho kiovu na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.Vile vile Rais Kikwete
amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikalina vyombo
vyake inaendelea kufuatilia tukio hili. Tutawasaka popote walipo na
kupambana nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na aina yoyote ya
uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au
wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi
yetu. Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania
na watu wake. Rais anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa
wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi
za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao wamejeruhiwa katika
tukio hilo. Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia anawaombea
wote walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na
shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete vilevile anatoa
pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la
kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuliyao muhimu ya uzinduzi
wa Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment