Sunday, May 5, 2013

Mripuko wa bomu waua 11 nchini Somalia

Watu 11 wameripotiwa kuuawa na wengine watano kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa limetegwa bomu kuripuka katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Maafisa wa eneo hilo na watu walioshuhudia wamesema kukwa, sauti za risasi zilisikika pia baada ya kutokea miripuko hiyo katika eneo lililoko umbali wa kilomita 4 kutoka Mogadishu.
Shambulio hilo la bomu limetokea katika umbali wa mita 100 tu kutoka ulipo ubalozi wa Uturuki mjini Mogadishu.
Itakumbukuwa kuwa, tarehe 2 mwezi uliopita wa Aprili, mripuko wa bomu ulilenga benki ya Dahabshiil mjini Mogadishu. Mripuko huo ulitokea nje ya makao makuu ya benki, masaa machache tu baada ya wanamgambo wa ash Shabab kuiamuru benki hiyo kuacha kutoa huduma katika maeneo ambayo yako mikononi mwa wanamgambo hao.
Serikali dhaifu inayoungwa mkono na Magharibi inaendelea kupambana na wanamgambo wa ash Shabab kwa miaka mitano sasa nchini Somalia na inalindwa na vikosi vya Umoja wa Afrika kutoka nchi za Uganda, Burundi na Djribouti. Aidha Somalia ni nchi yenye wakimbizi wengi katika maeneo mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na watu wengi waliokimbia maeneo yao ndani ya Somalia kwenyewe.

No comments: