Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ametangaza Tume mpya ya
Uchaguzi itakayoratibu na kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi
na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi huo unaanzia
Aprili 30, mwaka huu.
Taarifa ilisema Kamishna mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, Jecha Salim Jecha, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo.
Aidha, wajumbe pekee walioteuliwa kwa mara nyingine katika tume hiyo ni
Nassor Khamis Mohamed na Ayoub Bakari Hamad, kutoka Chama cha Wananchi
(CUF).
Wajumbe wapya walioteuliwa katika tume hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Mambo
ya Ndani, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Katibu Mkuu mstaafu wa iliyokuwa
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Salmin Senga Salmin, Makamu
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Haji Ramadhan Haji na
Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Abdulhakim Ameir Issa.
Mwenyekiti pamoja na wasaidizi wake, wanatarajiwa kuapishwa Mei 4, mwaka
huu na tume hiyo ya uchaguzi inakabiliwa na zoezi la kusajili wapiga
kura wa kudumu waliofikisha umri wa miaka 18 baada ya zoezi hilo kukwama
kufanyika tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Aidha, tume hiyo itakuwa na kazi kubwa ya kuratibu na kusimamia uchaguzi
mkuu wa kwanza ukiwa chini ya mfumo mpya wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa inayoundwa na vyama vya CCM na CUF.
Wakati huo huo, Dk. Shein amefanya mabadiliko madogo kwa kumuondoa
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Mustapha Ibrahim na kumteua Dk. Idrisa
Muslim Hija kuwa Mkuu wa Mkoa huo wa Kusini Unguja.
No comments:
Post a Comment