Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, linawashikilia raia sita kutoka Malawi wanaosadikiwa kuishi bila kibali nchini.
Kamanda wa polisi Kanda Maalumu, Suleima Kova, alisema Aprili 27 huko
Mbezi Beach Kinondoni, eneo la miti mirefu askari wakiwa katika doria
walifanikiwa kuwakamata raia hao wakiwa kwenye nyumba moja.
Aliwataja raia hao ni Sam Saka (24), Peter Jaston (29), Pres Magombe
(25), pamoja na ndugu watatu Musa, John, na Nesta Chilwa (30), ambao
taratibu za kisheria zinafanywa ili kuchukuliwa hatua stahiki.
Pia alisema watuhumiwa wengine 59, wanashikiliwa na jeshi hilo kwa
kosa la kukutwa na silaha mbili, bastola moja pamoja na risasi 26, Mei 2
huko eneo la Buza kwa Lulenge Ilala, baada ya askari wa kituo cha
StakiShari kufanya msako na kuwatia nguvuni.
Alisema watuhumiwa hao walikuwa wakifanya uhalifu wa ujambazi katikati
ya mji kwa kutumia pikipiki aina ya Boxer namba T992 CHZ, T 517 CCV,
na SUNLG namba T 801 CCW, pamoja na gari T200CAG.
“Majambazi hao wanatumia silaha kama SMG, Short GUN, zikiwemo zile za
kivita, kwa kufanya uhalifu, na idadi kubwa ya uhalifu wanaoufanya ni
kupora watu simu, fedha na komputa mpakato”alisema Kova.
Alisema katika hatua nyingine jeshi hilo limefanikiwa kukamata vitu
mbalimbali ikiwemo pombe haramu ya gongo lita 240 eneo la Kigamboni.
Pamoja na hayo alisema watuhumiwa wengine sita wanashikiliwa na jeshi
hilo kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu ambao ni Juma Ally (20),
Hamis Hassan (18) wakazi wa Tumbi, Mohamed Junga (21), Asha Hassan (30)
wakazi wa Ferry, pamoja na Silvestar Nailon (19) mkazi wa Magogoni.
No comments:
Post a Comment