HAPO kitambo kidogo niliandika
makala katika gazeti la Raia Mwema nikiomba waumini wote wa kiislamu na
kikristo ‘wachinje’ imani zao ili Taifa libakie salama. Naona makala ile
haikueleweka kwani baada ya tukio la hivi karibuni la kulipuliwa kanisa huko
Arusha sasa wamejitokeza watu na hasa viongozi wa kidini na wa kisiasa wakidai
mihadhara ya wazi ipigwe marufuku kana kwamba mihadhara ndio sababu kuu ya watu
kumwagiana tindikali, kulipuana kwa mabomu, kugombea kuchinja, kuchinjana na
kupigana risasi!
Napenda awali ya yote niseme kuwa
mie ni mmoja wa waliokerwa sana pale Taifa lilipoanza kuruhusu mihadhara hadi
hata kufikia kuwaruhusu waumini wa dini mbalimbali kuanzisha ‘mashindano’ ya
kutumia viwanja vya michezo na sehemu nyingine za umma kwa mahubiri. Na
viongozi wetu wa serikali wakawa wageni mashuhuri kwenye mihadhara hiyo! Nao
sasa wanapiga kelele ‘mihadhara ifutwe’!
Kwa wale wa umri wangu watakumbuka
kwamba kabla ya ujio wa utawala wa Mzee Mwinyi mihadhara ilikuwa inafanywa na
waumini wa kikristo hasa pale Jangwani, mjini Dar es Salaam. Nyakati hizo
tulishuhudia ujio wa wahubiri wa kikristo toka nchi mbalimbali. Hizi zilikuwa
zile enzi za ‘November Crusades’ pale Jangwani.
Lazima tukiri kwamba; kama ni dhambi
ya mihadhara, basi, ilianza kabla ya utawala wa Mzee Mwinyi, na washiriki
wakubwa walikuwa wahubiri wa dini ya kikristo. Lakini lazima pia tukiri nyakati
hizo kebehi na matusi dhidi ya imani nyingine nayo haikuwa kubwa ingawaje
kulikuwa na malalamiko hapa na pale kutoka kwa waislamu. Waislamu nao wakadai
wapatiwe fursa ya kufanya mihadhara maeneo ya wazi.
Kwa vijana wa siku hizi na wale
ambao wanajifanya wamesahau, wakumbuke kuwa toka miaka ya mwanzoni mwa uhuru
hadi miaka ya 70 ilikuwa si rahisi kwa waumini wa kiislamu kupata kibali cha
kuendesha mihadhara kama tuliyoishuhudia kuanzia miaka ya themanini.
Ikumbukwe kuwa kwa miaka mingi tu
waislamu hawakuwa na TV, gazeti wala redio, na hata pale walipotaka kuanzisha
mambo hayakuwa rahisi sana kwao.
Nimeelezea hili ili tukumbuke ni
kina nani hasa walianzisha hili suala la mihadhara. Kabla ya utawala wa
Mzee Mwinyi mihadhara pekee ya dini ya kiislamu ilikuwa ni siku ya Maulidi.
Mihadhara hii ilikuwa inafanyika
usiku sehemu nyingi na ilikuwa inatawaliwa na masuala ya kiimani na ilikuwa
nadra kusikia kashfa dhidi ya dini nyingine. Kwa kumbukumbuku yangu, sikuwahi
kusikia malalamiko toka kwa ndugu zetu wa kikristo dhidi ya mihadhara ya
Maulidi.
Kwa hakika, malalamiko dhidi ya
mihadhara ya Maulid yalikuwa miongoni mwa wasilamu wenyewe, baadhi wakikubali
uwepo wa Maulid wengine wakidai Maulid ni bidaa!
Lakini dhambi ya kuruhusu mihadhara
ya nje ya nyumba za ibada ilianza kututafuna pale ambapo waislamu nao
walipoanza kuendesha mihadhara ya viwanjani, redioni, kwenye TV na magazeti.
Mara ghafla kukawa na ‘mashindano’
ya kuendesha mihadhara na aina nyingine ya mahubiri nje ya nyumba za ibada.
Ikaanza kuwa mazoea ukienda sokoni au ukipita barabarani unakuta mtu anahubiri
hadi sauti inamkauka!
Kukazuka vikundi vinapita majumbani
mwa watu eti kutoa neno hata kama mwenye nyumba au chumba si wa imani yao!
Ukipita barabarani unapewa kwa njia ya kulazimisha gazeti, maandiko au vitabu
vya imani isiyokuwa yako!
Ukiingia kwenye basi yupo mhubiri!
Anahubiria hata wasio wa imani yake eti kwa kuwa tu mwenye chombo cha usafiri
naye anaona ndio mchango wake kwa kumruhusu mhubiri yule ahubiri!
Ndani ya mabasi ya abiria ambao ni
wa imani tofauti tukaruhusu kanda na sinema za imani fulani zionyeshwe!
Akitokea abiria wa imani tofauti aseme kanda au video izimwe inakuwa mtafaruku!
Matendo haya yakitendwa zaidi na waumini wa dini za kikristo.
Waislamu nao tukaanza kuona vikundi
vya mahubiri (wao wanaita daawa). Vikundi hivi vikawa kashfa dhidi ya
wakristo (wao wakiwaita Wagalatia) mtindo mmoja! Vikundi hivi vikawa na
vyombo vya kisasa kabisa na vikaanza kuzunguka nchi nzima vikitoa kashfa dhidi
ya wakristo!
Kanda zikaandaliwa za kashfa tupu!
Hujifunzi lolote la maana katika imani ya kiislamu zaidi ya kwamba Yesu si
Mungu na ‘uongo’ wa Mtume Paulo! Mafundisho namna ya kusali,
kufunga, nk. wao hapana; bali kashfa tu!
Baadhi ya vikundi vya kikristo navyo
vikaingia mtegoni; maana vilikubali kuandaa mihadhara ya pamoja ili kuonyeshana
ufundi wa kukashifu imani ya wenzako! Mihadhara hii ya pamoja ikarekodiwa na
kanda zikasambazwa ndani na nje ya nchi!
Kwa vijana na watoto, hizi kanda ndo
zikawa kama vitabu rejea vya wanafunzi mashuleni! Mihadhara ikawa ndio ‘lecture
theatres’ zao! Sasa watoto wanakojolea quran eti tunashangaa!
Kama nilivyoeleza hapo juu, ni kweli
mihadhara imechangia kwa kiasi fulani katika mgawanyiko huu wa Taifa, lakini
je; mihadhara ndio kianzilishi (cause)?
Kwa wale waliochoka kufikiri au wale
wasioitakia mema nchi yetu, jibu lao litakuwa ‘ndio’! Lakini kwa wale
wanaousumbua bongo zao kufikiri, wazalendo na wenye nia njema na nchi yetu na
watu wake, jibu ni ‘hapana’.
Mihadhara, mabomu, tindikali, ugomvi
wa kuchinja, kuchinjana na kupigana risasi ni dalili (symptoms) za
ugonjwa. Taifa ‘linaumwa’ lakini kwa bahati mbaya ‘madaktari’ wake wanakimbilia
kuumwagia maji mwili wake eti kwa kuwa joto limepanda sana!
Ni kama kujaribu kumaliza malaria
kwa kufunga bandeji kichwani au kwa kununua klorokwini kwa wingi! Mgonjwa
hatapona, atakufa tu! Tunapaswa si kuangamiza mbu pekee bali kuangamiza
mazingira yanayosababisha mbu kuzaliana.
Labda nijaribu kuelezea sababu
zinazolifanya Taifa liwe gonjwa. Najua wengine wengi wameshagusia mambo haya,
lakini kwa kuwa ‘madaktari’ bado hawajazinduka, inapaswa tuendelee kukumbushana
ili siku moja wote tusiathirike. Au majaaliwa ya Mungu siku moja madaktari
wazinduke na kutupatia tiba muafaka.
Na katika kukumbushia, tunatakikana
tusimwonee yeyote haya; maana hata kama ni wa imani yako, anaweza kukudhuru!
Siasa za majitaka
Siasa za majitaka ambazo hata mmoja
wa viongozi wa CCM alipokuwa anajiuzulu alithibitisha ndio dira kuu ya chama
hicho, ndio chanzo kikuu cha mgawanyiko tulionao. Ukitaka kujua CCM imedumbukia
kwenye siasa majitaka rejea yafuatayo:
- Ilani ya uchaguzi ilipowahakikishia waislamu Mahakama ya Kadhi.
Binafsi
naamini bila kuwapatia waislamu Mahakama ya Kadhi tutaendelea na misuguano
isiyo lazima. Katika makala zangu za awali nimeshaeleza udhaifu wa hoja kwamba
hili ni suala la imani lisigharamiwe na serikali.
Tuna
masuala mengi ya kiimani ambayo yanagharamiwa na serikali ikiwa ni pamoja na
misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini, huduma kwa ubalozi wa Vatican, n.k. Na
huko hatusikii hoja hii ikijitokeza.
Pia
naamini tunaikuza mno Mahakama ya Kadhi. Mimi naamini kutakuwepo hata baadhi ya
waislamu wataopendelea kwenda mahakama za kawaida hata hiyo mahakama ikiwepo.
Huko nyuma
ilipokuwepo ilikuwa hivyo.
Binafsi,
naamini CCM ingeweza kuhakikisha Mahakama ya Kadhi inapatikana bila kuingiza
kwenye ilani yake ya uchaguzi. Si CCM ndiyo ilikuwa na uhakika wa kuunda
serikali?
Ubaya
ulikuwa ni kutumia hitajio la watu wa imani fulani ili kujipatia kura
kwenye uchaguzi. Kitendo hiki ndicho kiliweka mstari wa kwanza wa kutenganisha
Watanzania kwa msingi wa imani. Waliotayarisha, kuipitisha na kuighani ilani
ile ndio tunaopaswa kuwawajibisha au kuwarekebisha kama tunataka kuwa salama.
Hawa
hawakutoa mhadhara lakini dhambi yao ni kubwa kuliko ya watoa mihadhara.
Tukiwafumbia
macho watarudia tena kama si kwenye uchaguzi wa 2015 itakuwa chaguzi nyingine.
Si ndio mbinu iliyowapatia kura nyingi toka kwa waislamu?
- Mbinu za kupata kura kwa kubambikiza kuwa baadhi ya vyama au viongozi wa vyama hivyo ni vya / wa dini fulani.
Kauli za
wanasiasa hawa, hasa wa CCM, zilikuwa na madhara makubwa kuliko mihadhara
wanayotaka kuipiga marufuku. Hawa wanaweza kuendeleza kauli hizo mwaka 2015 kwa
kuwa wanaamini ndio njia ya kupata ushindi wa kishindo.
Kama ni
kupiga marufuku, tunapaswa kwanza kuwapiga hawa marufuku kabla ya kupiga
marufuku mihadhara. Tusipozinduka kwa hili tujiandae kwa vyama vya kisiasa
vitakavyokuwa kwa misingi ya kidini huko tuendako.
Kama si
vyama, basi, tujiandae watu kupiga kura kidini. Si tumeanza kuona dalili kwenye
uchaguzi wa mabaraza ya katiba? Au tunajifanya hatuoni?
- Uchaguzi wa Spika kwa msingi wa maumbile: ubaguzi wa aina moja huibua ubaguzi wa aina nyinginezo.
Huwezi
kuwa na jamii (hasa viongozi) inayoruhusu ubaguzi wa aina moja halafu ukadhani
ubaguzi huo utakomea hapo. Hii ndio falsafa ya ubaguzi; ubaguzi hausimami peke
yake.
Walioanza
kutuelekeza tutizamane kwa maumbile ndio waliopandikiza ubaguzi wa aina
nyingine. Ni kama ubaguzi umeruhusiwa rasmi! Itakuwa vipi uchaguzi ujao wa
Spika waislamu wakasema kwa kuwa maspika wengi waliotangulia walikuwa wakristo
sasa ni zamu ya waislamu kutoa spika? Si hao wanasiasa wa maji taka
wametuonyesha kuwa badala ya kuangalia viwango tunaweza kuangaliana kimaumbile,
kidini, kikabila nk?
- Uendeshaji wa bunge na lugha zinazotolewa ndani ya bungeni moja ya aina mbaya ya siasa za majitaka.
Kwa jinsi
uongozi wa bunge unavyoachia lugha za matusi zivurumishwe, hasa na wabunge wa
CCM, ipo siku lugha ya matusi haitakuwa dhidi ya wabunge wa upinzani bali
itakuwa dhidi ya imani ya kidini ya watu fulani au dhidi ya hoja iliyotolewa na
wabunge wa upinzani ambayo itakuwa inatetea maslahi ya waumini wa dini fulani.
Nchi italipuka!
Wanaoendeleza
mzaha huu pale bungeni lazima waelewe ipo siku wataitumbukiza nchi kwenye
matatizo makubwa ya kidini.
Kukosekana kwa haki
Haki ya mtu au kikundi cha watu ni
pamoja na kusikilizwa hata kama madai yao hayana hoja. Kwa miaka nenda rudi
waislamu wamekuwa wakitoa malalamiko kuhusu wasivyoridhishwa na BAKWATA, uwiano
wa wanafunzi kwenye taasisi za elimu, uwiano wa watumishi serikalini, kufutwa
kwa Mahakama ya Kadhi, nk.
Badala ya hoja hizi kusikilizwa na
kutolewa ufafanuzi au kutafutiwa ufumbuzi, serikali imekuwa aidha ikikaa kimya
au kutoa kauli tata au kuwaachia viongozi wa dini nyingine kujibu malalamiko
ambayo hawakupelekewa wao. Utadhani maaskofu ndio wamekuwa wasemaji wa
serikali!
Baadhi ya waislamu kwa kukosa majibu
murua toka kwa serikali, na kwa kuchukizwa na majibu yanayotolewa na viongozi
wa dini ambao hawakuwapelekea matatizo yao, wameamua kuonyesha hasira zao kwa
njia mbalimbali.
Ili tuwe salama, inapaswa Serikali
itoke na kuzungumza na waislamu kuhusu malalamiko yao. Kwa mfano kama BAKWATA
inalalamikiwa kwa nini Serikali kama ilivyoshughulikia uundwaji wa BAKWATA,
isisimamie mchakato wa kuunda chombo kitakachokubalika na waislamu kama sio
wote, basi, wengi wao?
Hivi hatuoni kuwa na chombo ambacho
tunajidanganya ndicho kinasimamia maslahi ya waislamu wote; ilhali kinapingwa
na idadi kubwa ya waislamu ni kujitakia balaa la bure?
Mbona Serikali inapotokea mgogoro wa
wakristo (kumbuka Arumeru) haraka inakwenda kusuluhisha? Wale wanaojidanganya
kwamba masuala ya waislamu waachiwe wenyewe hawaoni kwamba madhara wanapata
wote? Wasio na walio waislamu?
Jikoni hakuwezi kuwa panawaka moto
na walio sebuleni wakaendelea kutazama TV wakidhani masuala ya jikoni
hayawahusu! Angalia sasa, wanaolalamika au kuathirika zaidi ya wote ni waislamu
au wakristo?
Tunaishi nyumba moja, kama mmoja wa
wanafamilia ana malalamiko wanafamilia wanapaswa kukaa pamoja kusikiliza,
kushauri na ikibidi kuondosha visababishi vya malalamiko.
Baba wa familia anapaswa kuongoza
kikao hicho cha familia na si kuwaachia kila mtoto kumjibu mwenzio anavyoona
inafaa! Na hii isiwe tu kwa waislamu bali kwa dini zote ikiwepo na ya kikristo,
wahindu, nk.
Tukiendelea kutegemea eti Serikali
iwalete FBI au CIA na wengineo kama ndio suluhisho, tutaangamia! Ukishaona
nyumba inashindwa kutatua matatizo ya wanafamilia hadi wamwite jirani wa mbali,
ujue hiyo familia haiko salama!
Uongozi dhaifu
Uongozi ambao hautambui kuwa kauli
na vitendo vyake vinaweza kuchochoea ubaguzi ni uongozi dhaifu sana. Sasa
viongozi wetu wamefanya nyumba za ibada (hasa makanisa) ni maeneo yao ya kazi
au kuendesha kampeni.
Ukishakuwa kiongozi wewe ni kiongozi
wa wote; wa imani na wasiokuwa wa imani yako. Wewe nenda siku na saa yako ya
ibada kafanye ibada yako, full stop!
Kisingizio cha kuchangisha harambee
hakina mashiko. Ni udini tu! Hivi nani alikuwa Mkatoliki kama Mwalimu Nyerere?
Yeye mbona hatukumuona akizunguka toka kanisa moja kwenda jingine kwa kisingizo
cha kuchangisha mamilioni yeye na marafiki zake?
Hivi sasa mshiriki mkuu kwenye hizi harambee
ni Mkristo; hivi ingekuwaje au itakuwaje akijitokeza muislamu mwenye ndevu
akaanza kuzunguka nchi nzima misikitini akichangisha mamilioni? Hatutamwitia
CIA au FBI? Hatutamwita majina ya Al Shabaab, Al Qaeda?
Tusiwaonee haya viongozi wa aina
hii. Tuwaambie wao na wanaowakaribisha bila kubabwaja kuwa ‘MCHEZO WAO NI
MAUTI YETU’!
Uongozi imara pia hauwezi kuruhusu
nyumba za ibada zianzishwe kama uyoga hata kwenye mabanda ya kuku!
Tanzania ni nchi pekee unaweza
kuanzisha msikiti au kanisa kwenye nyumba yako bila kusajiliwa na serikali eti
tunajidanganya serikali haina dini!
Serikali yetu haina dini lakini ina
wajibu wa kuhakikisha wenye dini wanafuata sheria na wanaishi kwa amani na
upendo!
Serikali yenye kujua itendalo
haiwezi kuachia shughuli za imani moja ikaendeshwa ndani ya maeneo ya umma kama
mabasi, kumbi za mikutano nk.
Inakera, wewe umelipa nauli halafu
unaingia ndani ya basi mtu anaanza kwaya au kaswida? Na
tuambizane ukweli, wa kwaya ndio wamekubuhu! Au unaweka mkanda wenye maudhui ya
dini fulani ukiuliza unaambiwa kama hufurahishwi usitizame?
Serikali imara inapaswa kupiga
marufuku tabia hizi na hata za kuandika maandishi ya kiimani ubavuni mwa vyombo
vya usafiri.
Wakati wa Mwalimu Nyerere hata
hakupata taabu mzee wa watu; maana wenye vyombo vya usafiri hawakuthubutu kwa
kuwa walielimishwa ubaya wa udini!
Hivi inasaidia nini kuandika ‘gari
hili linalindwa na damu ya Yesu’? Au ‘Mwenye ezi Mungu ni Mmoja na Muhamad
(SAW) ni mtume wake’? Haitoshi kauli hizi kukaa moyoni mwako na ndani ya nyumba
yako au nyumba ya ibada yako?
Kama nilivyosema awali, haya mambo
hayakuwapo enzi zile za Mwalimu Nyerere lakini kwa kadri tulivyoyaruhusu sasa
yamepamba moto. Magazeti na vituo vya TV vimeanzishwa na kazi ni moja na wote
tunaijua ila tunajifanya hamnazo!
Serikali yenye kujua uzito wa kulea
udini haiwezi kuruhusu mtu aote ndoto kwa imani ya dini fulani na Serikali
imsaidie kutibu wananchi kutokana na ndoto!
Aidha, viongozi wa Serikali inayojua
wajibu wake hawawezi kuwa mstari wa mbele kuwaaminisha wananchi kuwa dawa hiyo
ya kiimani inatibu bila kufanyiwa utafiti na vyombo ilivyounda yenyewe!
Uongozi imara hauwezi kuruhusu maandishi
na vitabu vya dini kuingizwa kwenye ofisi zake. Sasa hapo Tanzania hakuna ofisi
ya umma utaingia usiweze kubaini mara moja mhusika ni wa dini gani!
Bila aibu wamebandika maadiko ya
imani zao kwenye kuta za ofisi za umma! Mathalani weye ni mkristo, unaingia
ofisi unakuta nyuma ya kiti alichokalia bosi kumeandikwa ‘ Ashadu Alla
illah Hai La Lah, wa ashadu anna Muhamadan Rasullulah’! Imani inakutoka
mara moja kama utaweza kupatiwa huduma ofisi ile.
Halikadhalika unaingia ofisi ya umma
unakuta maandishi ‘BWANA NDIYE KIMBILIO LANGU’! Unaanza kujiuliza sijui
nimwamkie ‘bwana asifiwe’ ndio nitahudumiwa?
Serikali tuondosheeni upuuzi huu
katika ofisi za umma. Wengine wamekubuhu kiasi wanaruhusu vikundi vya maombi
kutembelea ofisi za umma kutoa maombi!
Utasikia mtumishi anawaomba wenzie:
“Jamani watumishi wa mungu wametutembelea, karibuni tufanye maombi. Haitachukua
muda mrefu’! Jamani, kama mtu anataka kutumikia imani yake aende kanisani au
msikitini akaombe kazi huko!
Mahubiri ya chuki ndani ya nyumba za
ibada, majumbani mwetu, ofisi za serikali, taasisi za elimu na kwenye vyombo
vya habari.
Ukitaka kujua chuki haianzii kwenye
mihadhara bali inaanzia ndani ya nyumba za ibada wewe nenda kwenye nyumba zetu
za ibada hata kama hazina spika usikilize watoto wanavyofundishwa ubaya wa dini
nyingine!
Sasa ni mashindano ya kueleza ubaya
wa imani nyingine na si kutoa mafundisho ya kitabu cha imani husika.
Wajuzi wanasema ‘a child is the
reflection of the parents’. Ukitaka kujua watoto wanaelimishwa nini
majumbani jaribu kumuuliza mtoto ni nini mtazamo wake kwa watu wa imani
nyingine! Utasikia chuki na dharau.
Watoto wa aina hii ndio hao
wanaokojolea vitabu vitakatifu bila woga! Mie miaka ile japo nimetoka familia
ya kiislamu sikuwaza hata siku moja kumtukana mkristo au kukashifu Biblia!
Nilisoma shule ya msingi ya Waluteri
(Makuyuni Lutheran Primary School), na hakuna mchungaji au mwanafunzi wa
kikristo alinikashifu au kunitaka niache usilamu niwe Mluteri kwa miaka yote
saba niliyosoma pale!
Sikuwahi pia kusikia mtoto wa
kikristo akimtukana mwislamu au akikashifu uislamu. Sote tulihubiriwa vyema
kwenye nyumba za ibada na tulilelewa vyema na wazazi wetu.
Ilifika mahali tulivutiwa hadi kila
asubuhi wenzetu walipokuwa wanaenda kanisani kwa sala ya asubuhi tuliongozana
nao kuwalinda wasidhuriwe na wanyama!
Ndugu zangu, huu utamaduni wa
kupandikiza chuki ndani ya mioyo ya watoto na vijana utatugharimu! Si
kumtumikia mungu huku; bali ni kumtumikia shetani!
Ndugu zangu, hata tukifuta mihadhara
haitasaidia sana. Bila kutibu haya itakuwa sawa na nyumba inayovuja halafu
mwenye nyumba anaamua kuhamisha kitanda toka kona hii kwenda kona ile.
Ili tupone ugonjwa huu unaotutafuna,
lazima tutibu vyanzo na si dalili. Mihadhara, kuchinjana, kutukanana, kukashfiana,
kuchoma na kunajisi vitabu vitakatifu, kupigana risasi na kumwagiana tindikali
ni dalili (symptoms) tu!
Ukiondoa dalili bila kuondosha
vidudu viambukizi (infectious agents) ugonjwa hauponi ng’o! Tutapiga
marufuku mihadhara na tutaona chuki na matendo ya chuki yakishamiri.
Taifa linatakiwa lisimame na kutoa
ufumbuzi kwa niliyoeleza hapo juu. Lazima tupige marufuku siasa za maji taka,
tushughulikie malalamiko ya waumini kwa dhati, tusiruhusu dini moja kuchukua
jukumu la serikali kujibu malalamiko ya dini nyingine.
Aidha, tuzuie matendo,
maandishi, nyimbo, sinema na mahubiri sehemu za umma, uanzishwe utaratibu wa
kuanzisha nyumba za ibada na tuwahimize waalimu wa shule za madhehebu, wamiliki
wa vyombo vya habari, wazazi na viongozi wa dini kuacha mahubiri au malezi
yanayopandikiza chuki miongoni mwa watoto na vijana.
Aidha, uwekwe utaratibu wa
kufuatilia na pale inapobainika kuna ukiukwaji mhusika aadhibiwe mara moja.
Lakini jukumu hili lisiachiwe
Serikali peke yake. Viongozi wa dini, wazazi na kila moja wetu ajiulize hivi
kupalilia chuki dhidi ya dini au madhehebu nyingine inatusaidia nini? Je,
hatuvuni hasara badala ya faida?
Kwa nini tusihubiri yale yaliyo mema
kwenye imani zetu na kusisitiza umuhimu wa kuvumiliana?
Tunapaswa kujua hakuna aliye bora
mbele ya mwenye ezi Mungu zaidi ya yule aliye mwema miongoni mwetu. Na kamwe
haitatokea watu wote tukawa wa utakuwa unaota ndoto za alinancha.
chanzo:Raia mwema
No comments:
Post a Comment