Thursday, May 2, 2013

Tandau afariki dunia, JK amlilia

Waziri wa zamani, Mjumbe wa halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na Mweka Hazina wa Taifa wa chama hicho, Alfred Tandau, amefariki dunia.
 
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa CCM, Tandau alifariki dunia juzi jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam alikokuwa  amelazwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya tumbo. 
 
Kufuatia msiba huo, Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, na kueleza  kushtushwa na kifo cha Tandau ambaye alikuwa waziri wa siku nyingi.
 
Rais Kikwete alisema alimfahamu Mzee Tandau kwa miaka mingi na alikuwa kiongozi hodari na mwaminifu ambaye katika nafasi zote alizozishikilia katika utumishi wake wa umma alithibitisha uadilifu na uzalendo wa kiwango cha juu.
 
Alisema katika uongozi wa Chama cha Wafanyakazi cha Nuta na baadaye Juwata, Mzee Tandau alijipembenua kama mtetezi halisi na mkweli wa maslahi ya wafanyakazi.    
 

No comments: