Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein amesema alipokea jina la Maalim
Seif Sharif Hamad kutoka Chama cha CUF ili kuliteua kuwa Makamu wa
kwanza wa Rais Zanzibar mwaka 2010 baada ya kuwa mshindi wa pili wa
nafasi ya urais.
Dk Shein ametoboa siri hiyo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa
CCM uliofanyika huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja juzi.
Alisema inashangaza wanapojitokeza baadhi ya watu wanaotaka kuwatisha
wenzao wakifikiri kuwa hata watakapovunja sheria serikali itawahofia,
kuchekea na kuwatazama kwa macho.
Alieleza kwamba kama Rais wa Zanzibar aliyechaguliwa na wananchi hana
mtu anaemuogopa ila hupenda kuongoza kwa kufuata na kuheshimu misingi ya
sheria za nchi na kufuata dhana ya utawala bora wa sheria.
Aidha, Dk. Shein alisema waliingia katika kinyang’anyiro cha kuwania
urais wa Zanzibar jumla ya wagombea watano lakini kwa bahati nzuri,
Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilimtangaza yeye ni mshindi kupitia CCM na
kula kiapo cha kulinda na kutetea katiba na sheria.
“Nilimwita Maalim Seif Sharif Hamad na kumtaka alete majina ya watu toka
chama chake walioteulwa ili kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais,akaniambia
ameteuliwa yeye, nikamwambia nenda kaniandikie uniletee kwa maandishi,
likaja jina lake tu nikamteua,” alisema Dk Shein.
Hata hivyo Rais huyo wa Zanzibar aliasa kuwa vyama vya hiari vya
kijamii, NGO na jumuiya nyingine zikiwamo za dini ambazo zimesajiliwa
kwa mujibu wa sheria zisimamie ipasavyo malengo ya kusajiliwa kwake.
Alisema si busara kwa jumuiya au chama cha kisiasa kufanya kazi za dini
au za dini zikafanywa ni za kisiasa na kuwataka wanaofanya hivyo kuacha
kufanya hivyo kabla mikono ya sheria haijawakamata.
Aliwataka wanachama wa CCM kujiandaa toka sasa ili kupata ushindi mwaka
2015 kwasababu wana kila sababu ya kushinda kutokana na kutekeleza
vizuri ahadi na kusimamia ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment