Vijiji vilivyozua mapigano hayo ni vya Muleru na Lalage na inadaiwa kuwa chanzo chake ni kugombea msitu unaomilikiwa na kijiji kimojawapo.
Diwani wa Kata ya Balangdalalu, Paulo Tarimo, alisema jana kuwa ugomvi kati ya vijiji hivyo ni wa siku nyingi na ulikuwa ukitafutiwa ufumbuzi kupitia vikao mbalimbali.
Tarimo alisema kuwa kijiji cha Muleru ndicho kinadaiwa kumiliki msitu huo wa Tenga.
Habari zilizopatikana jana zilisema kuwa wakazi wa kijiji cha Lalage, walivamia msitu huo na kulima mazao mbalimbali kiasi cha ekari 200, hali ambayo wakazi wa kijiji cha Muleru haikuwapendeza.
Diwani Tarimo alisema kufuatia hali hiyo, wakazi wa kijiji cha Muleru mapema jana walijitokeza na kufyeka mazao hayo, hali ambayo ilizua mapigano kati yao.
Alisema katika mapigano hayo, mwanakijiji wa Muleru alichomwa mshale na amelazwa hospitalini na hali yake ni mbaya. Alisema katika hatua nyingine inayoonekana kama kulipiza kisasi, mwanakijiji mmoja wa Lalage, alichinjwa hadi kufa. Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, inasemekana kuwa mapigano yalikuwa yakiendelea.
Mapema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, alithibitisha kutokea kwa mapigano hayo na kwamba alikuwa njiani kuelekea eneo la tukio.
Alisema habari za awali alizokuwa amezipata zilidai kuwa mtu mmoja alikuwa amejeruhiwa katika mapigano hayo, lakini hakuwa na taarifa rasmi hadi hapo atakapowasili eneo la tukio.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Christine Mndeme, hakupokea simu wakati NIPASHE lilipokuwa likimtafuta kupata maelezo zaidi kuhusiana na mapigano hayo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment