Sunday, May 5, 2013

Moto wamwakia Dk Kawambwa

Siku moja baada ya Serikali kuchukua uamuzi mgumu wa kuyafuta matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 na kuamua yaandaliwe upya, wasomi, wanaharakati, wanasiasa na wanasheria wameitupia lawama Serikali wakitaka wote waliosababisha uzembe huo kushtakiwa kwa kusababisha vifo na udhalilishaji.
Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera (Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wakati akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne alisema kuwa, wameagiza Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuweka viwango ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi zao.
Uamuzi huo wa Serikali umetokana na matokeo mabaya ya mitihani ya mwaka jana, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi walipata alama sifuri.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti jana, wadau hao walisema kuwa licha ya wahusika kujiuzulu wanatakiwa pia kushtakiwa kutokana na uzembe wa makusudi.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anatakiwa kufukuzwa kazi na kushtakiwa kutokana na matokeo hayo mabaya.
Alisema haitoshi Dk Kawambwa kujiuzulu au kufukuzwa kazi, bali pia anatakiwa kushtakiwa kwa matokeo hayo, yaliyosababisha pia mauaji ya wanafunzi wanne, aliyosema hayakutokea kwa bahati mbaya, bali ni mpango maalumu ulioandaliwa na watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
“Kwa maneno aliyoyatoa, Waziri (Dk Kawambwa) wakati wa kukataa hoja yangu, haitoshi kujiuzulu tu, angekuwa anajificha asionekane hadharani kwa sababu ni aibu,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Kuna watu wanatakiwa washtakiwe kwa kusababisha maafa haya. Matokeo haya hayakutokea kwa bahati mbaya yaliandaliwa kwa makusudi, ni wauaji hawa!”
Aliionya Serikali kutochezea akili za Watanzania na kwamba familia za waliopoteza maisha kwa matokeo hayo zipewe kifuta jacho.
Mbatia aliongeza kuwa, taarifa alizonazo ni kwamba kutokana na matokeo hayo mabaya ya mtihani, baadhi ya wasichana wamekata tamaa na kuolewa.
Februari mwaka huu, mbunge huyo aliwasilisha hoja binafsi bungeni, akitaka kuundwa kamati teule kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya elimu nchini akieleza sababu kuwa hakuna mitalaa tangu Tanzania ipate uhuru na ipitie sera za elimu nchini. Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na Serikali ikidai kuwa kuna mitalaa inayokidhi viwango.
Alisema wanafunzi wanafahamishwa shuleni kuwa daraja D ni kuanzia alama 21 hadi 40; C kuanzia alama 41 hadi 60; B kuanzia 61 hadi 80 na A kuanzia 81 hadi 100, lakini Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilibadili mfumo huo bila waraka wowote.

1 comment:

Anonymous said...

KWANN IWE KAWAMBWA WAKATI BARAZA LA MITIHANI LIPO KWANN ISIWE NDALICHAKO