Rais Jakaya Kikwete, ametangaza neema ya kupunguza kodi ya mishahara kwa
wafanyakazi nchini kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wa makato.
Kadhalika, Rais Kikwete amesema kuwa serikali itawaongezea kidogo
mishahara watumishi wa serikali. Hata hivyo, hakuweka wazi kiwango
hicho.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya akiwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya
Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kitaifa ilifanyika mkoani Mbeya.
Alisema kiwango cha chini cha kodi kutoka asilimia 14 ya sasa ya makato
yote wanayokatwa wafanyakazi wa umma katika mishahara yao, kitatangazwa
na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, wiki mbili zijazo
atakapowasilisha bajeti ya serikali katika Bunge la Bajeti linaloendelea
mjini Dodoma.
Rais Kikwete aliongeza kuwa, serikali imekuwa ikifanya jitihada za
makusudi katika kuboresha mazingira ya wafanyakazi yakiwamo kuwapunguzia
makato ya kodi kwenye mishahara yao hadi kufikia asilimia 14 mwaka huu
kutoka asilimia 18 zaidi ya miaka minne iliyopita.
Kutolewa kwa kauli hiyo kunafuatia kilio cha muda mrefu cha wanyakazi
nchini juu ya kuboreshewa mazingira yao ya kazi ikiwamo mzigo huo wa
makato ya kodi.
Wabunge kadhaa na wadau wengine wamekuwa wakipendekeza kwamba kiwango hicho kipinguzwe angalau kufikia asilimia tisa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kuongezwa kwa mishahara kwa watumishi wa
umma kunatokana na ukusanyaji mzuri wa mapato ya serikali na utendaji wa
kazi, na kwamba sehemu kubwa ya mapato hayo hutumika kulipa mishahara
kwa mfano, mwaka ujao zaidi ya asilimia 44.9 itatumika kwa ajili ya
mishahara.
Akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya Rais Kikwete, Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholaus
Mgaya, alieleza baadhi ya matatizo makubwa ambayo kwa sasa taifa
linakabiliana nayo kuwa ni pamoja mazingira magumu ya wafanyakazi
yakiwamo mishahara midogo, uhaba wa vitendea kazi, vurugu za kidini,
kufilisika kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na kushuka kwa kiwango cha elimu.
Kuhusu mishahara, Mgaya alisema kima cha chini kilichopendekezwa na
shirikisho hilo cha 315,000 mwaka 2009 hakimtoshelezi mfanyakazi kumudu
kupanda kwa gharama za maisha na kuiomba serikali kukiongeza kutoka
kiasi hicho hadi Sh.700,000 kwa mwezi.
Aidha, risala hiyo ilisikitishwa na kudidimia kwa kiwango cha elimu
nchini ikiwa ni pamoja na matokeo mabaya ya kihistoria ya kidato cha nne
ya mwaka jana ambayo zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya
mtihani huo walifeli.
Pia Tucta ilisikitishwa na hali ya ukata inayoikumba mifuko ya hifadhi
ya jamii ukiwamo Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Umma (PSPF), ambao
unadaiwa kuelekea kufilisika na kuwapa wasiwasi wafanyakazi wa umma
kuhusu fedha zao kwenye mfuko huo.
Pia Tucta imelaani hali ya vurugu za kidini zinazoendelea nchini huku
ikiwaasa viongozi wa madhehebu yote kukaa pamoja na kuzimaliza tofauti
za kidini kwa amani.
Akijibu risala hiyo iliyokuwa imesheheni changamoto lukuki
wanazokabiliana nazo wafanyakazi nchini, Rais Kikwete alisema kuwa
risala hiyo imejitosheleza na kwamba serikali imekubali kwa mikono
miwili kuzifanyia kazi.
“Nawahakikishia ushirikiano na msaada wangu pamoja na waliopo
serikalini. Risala imeandikwa vizuri ikiwa na ushauri, hoja na
imejitosheleza. Kama ingekuwa kwenye michezo ya mpira, tungesema
imekamilisha idara zote,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tumeipokea kwa mikono miwili, tunaahidi kuyatendea kazi na tutawaambia kuhusu maendeleo yote.”
Kuhusu ombi la kuongezewa kiwango cha mishahara kwa watumishi wa umma,
alisema kuwa serikali imepanga kuongeza kiasi kidogo na kuongeza kuwa
siyo kwamba serikali inapuuzia au kudharau pale maombi hayo yanapotolewa
bali ni kutokana na uwezo mdogo iliyokuwa nao.
Kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii, Rais Kikwete alisema serikali
imekuwa ikijitahidi katika kuhakikisha inaimarika na kwamba hakuna
mfanyakazi yeyote ambaye atakosa mafao yake pale atakapoyahitaji.
Aliongeza kuwa tangu aingie madarakani kumekuwapo na maboresho makubwa
katika mifuko hiyo ikiwa ni pamoja na kuiongezea uwezo wa kutoka Sh.
bilioni 10 hadi bilioni 50 kwa mwaka ili kuondoa mkanganyiko huo kwa
wafanyakazi.
Pia aliwaasa waajiri kote nchini, kuacha tabia ya kuwalazimisha
wafanyakazi wao kujiunga na mifuko wanayoipenda wao kwani kwa kufanya
hivyo wanavunja sheria na kuwataka kuwaacha wafanyakazi kujiunga na
mifuko wanayotaka wao wenyewe.
Aidha, aliahidi kushughulikia malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi
wa umma wapatao 50,000 kwa awamu ya kwanza na kufuatiwa waliobaki
takribani 27,000 kwa vipindi tofauti.
Akizungumzia kuhusu amani na utulivu wa nchi, Rais Kikwete alikemea
chokochoko za kidini kwa kusema kuwa vita ya dini haina mshindi na
kwamba suala la amani halina mbadala.
Kuhusu ajira, alisema tatizo kubwa nchini na kwamba mpaka sasa linafikia asilimia 12, kiwango ambacho alisema ni kikubwa.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali inakusudia kufungua
mianya ya ajira kwa vijana katika miaka miwili ya fedha ijayo na kwamba
zaidi ya ajira 600,000 zitapatikana.
“Kuanzia mwaka huu hadi kufikia mwaka 2016, serikali inaweza kuzalisha
ajira laki sita kwa kuweka fursa za upatikanaji wa ajira kwa vijana,
jambo ambalo litasaidia kukabiliana na tatizo hili,” alisema Rais
Kikwete.
Rais Kikwete aliongeza kuwa lengo la Serikali kujenga Uwanja wa Ndege wa
kimataifa mkoani Mbeya ni kufungua fursa za kiuchumi kwenye mikoa ya
Nyanda za Juu Kusini.
“Shabaha ya kujenga uwanja mkubwa wa ndege hapa Mbeya siyo kwa ajili ya
kushuhudia abiria na kuleta wageni, bali kuchochea maendeleo ya kiuchumi
kwenye maeneo ya kilimo kwa kuyaongezea thamani mazao kama maua, mboga
mboga na matunda,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wakuu wa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya kuanza maandalizi ya
kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na uwapo wa Uwanja wa Ndege
kama vile kuhamasisha kilimo cha maua, zao ambalo alisema kuwa tayari
alishalipatia soko la uhakika nchini Uholanzi.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ambayo huadhimishwa duniani kote
Mei Mosi, kila mwaka ilikuwa ‘katiba mpya izingatie usawa wa tabaka la
wafanyakazi’.
No comments:
Post a Comment