Shirika la Ugavi Umeme Nchini (Tanesco), limetoa zabuni yenye thamani
ya zaidi ya Sh. bilioni1.9 kwa kampuni ya McDonald Live Line Technology
inayomilikiwa kwa ubia na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo na
mfanyakazi aliyefukuzwa.
Mtumishi huyo wa Tanesco alifukuzwa kazi kwa tuhuma za upotevu wa zaidi
ya Sh milioni 100, kuharibu gari la ofisi, kutowajibika kazini na utoro.
a
Mbia huyo alitimuliwa Julai 1999 akihusishwa na kashfa kadhaa ikiwamo
ya kuharibu gari la Tanesco namba TZD 2944. Hata hivyo aliiingia kwenye
ubia wa makubaliano na mmojawapo wa wakurugenzi wa Tanesco Julai 17,
2008 ambaye baadaye aliteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo.
Taarifa hizo zimo kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma ya mwaka wa fedha
2011/2012 iliyotolewa bungeni na pia kusambazwa kwa wadau mbalimbali.
Ukaguzi wa CAG unaeleza kuwa kuanzia 2009 hadi 2011 McDonald Live
Technology, kampuni ya mfanyakazi wa Tanesco aliyefukuzwa ambaye
haikumtaja, ilipewa mikataba mitano ya zabuni kadhaa zilizohusu:
UKARABATI, KUTENGENEZA NJIA YA UMEME
Mkataba ulitolewa Desemba 2008 wa kujenga njia ya umeme hai wenye
kilometa 35 huko Mtibwa kwa gharama ya milioni 73.0, lakini hata hivyo
wakaguzi wa CAG hawakuonyeshwa nyaraka za zabuni hiyo.
KUKARABATI NJIA YA UMEME
Mei 2009 McDonald alipewa zabuni ya Sh milioni 110 ya kukarabati njia ya
Nordic ya msongo kilovolti 33. “Mkataba ulitekelezwa bila kuwepo
dhamana ya benki kama zabuni zinavyoelekeza.”
UKARABATI MSONGO WA KV 66
Mnamo Machi 11, 2010 kampuni hiyo ilikuwa na zabuni ya kukarabati njia
ya umeme ya Kiyungi-Arusha yenye msongo wa kilovolti 66 kwa gharama ya
Sh bilioni 1.4
“Kazi ilitakiwa kukamilika Machi 2011 lakini haikumalizika ikaongezewa
muda hadi Julai 2011 lakini ilikwama na kuongezewa muda hadi Novemba
2011 lakini bila mafanikio “
Ilisema ripoti ya CAG na kuongeza kuwa Juni mwaka jana Tanesco ilivunja
mkataba na McDonald wakati ambao ilikuwa imevuna zaidi ya milioni 475 za
malipo ya awali.
Ripoti iliongeza kuwa Tanesco ilifanya uthamini na kuitaka kampuni hiyo
kuirejeshea zaidi ya Sh milioni 504 faini, fidia na dhamana lakini hadi
taarifa hii inawasilishwa bungeni fedha hiyo ilikuwa haijalipwa.
Zabuni nyingine ni ukarabati wa njia ya umeme ya Ifakara ya kilovolti 33
kuanzia Kidato hadi Mahenge na njia ya Mtibwa kutoka Mkundi hadi
Mvomero yenye kilovolti 33 pia kwa gharama ya Sh milioni 338.2 .
CAG anabainisha mkataba mwingine kuwa ni wa matengenezo na ukarabati wa
njia za umeme wa moto za Mzakwe Dodoma zenye kilovolti 33 kila moja.
“Kutokana na ukaguzi ni wazi kuwa McDonald alipewa kazi mikataba na
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco kulingana na ubia kati yake na mmiliki wa
kampuni hiyo kama sehemu ya pili ya makubaliano iliyompa jukumu la
kutafuta kazi za kampuni hiyo” ilisema ripoti ya CAG.
UKAGUZI WA RUSHWA
“Tanesco imegubikwa na ukiukaji uliokithiri wa sheria na kanuni za
manunuzi unaosababishwa na viongozi wa juu na wa kati wa shirika,
Mkurugenzi Mkuu akiwa ndiye mwenye mamlaka ya juu ya manunuzi kushindwa
kuzuia ukiukwaji wa sheria kwani mara nyingi aliidhinisha manunuzi ya
zabuni ya chanzo kimoja ama yaliyozuia ushindanishaji wa kizabuni.”
WIZI WA UMEME
CAG anasema Tanesco haina kumbukumbu za kuaminika na taarifa sahihi za
mita za umeme zinazotumika na mashine za kuuzia umeme zilizosambazwa
nchi nzima .
Mkaguzi anataja pia kuwa shirika hilo halina pia kumbukumbu za kuonyesha
kiasi cha uniti za umeme kilichotolewa kwa mawakala wauza umeme sehemu
mbalimbali. Tena halina kumbukumbu ya idadi za uniti za umeme
ilizokusanya kutoka kwa wauzaji.
“Ni udhihirisho wa kuwepo ukiukwaji wa usimamizi wa mifumo ya fedha ,
kanuni na udhibiti mapato wa ndani” alisema mkazi na mdhibiti katika
ripoti yake.
No comments:
Post a Comment