Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini,
Sheikh Issa Ponda ameiomba Serikali kuunda Tume ya kushughulikia
matatizo ya Waislamu.
Ponda alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam
alipokuwa akitoa mawaidha ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, wilayani
Kinondoni.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja nje, baada ya
kupatikana na hatia ya kuingia isivyo halali katika eneo la Markazi
Chang’ombe.
Alisema kwa muda mrefu Waislamu nchini wamekuwa na madai ambayo Serikali haijaonyesha dhamira ya kuyashughulikia.
“Waislamu wamekuwa wakinyanyasiki katika nchi yao
utadhani wakimbizi, tuna madai ya msingi ambayo hayahitaji watu kufungwa
au kuundiwa kesi kwa hiyo sasa ni wakati wa Serikali kuunda tume
tutakayokwenda kuwaeleza matatizo yetu na vithibitisho vyake,” alisema
Ponda.
Ponda alisema atahakikisha kuwa anawatetea
Waislamu ili wapate haki zao zinazopokwa na baadhi ya watu wasiowapenda
waumini wa dini hiyo.
“Wamekuwa wakinitungia njama za kuniondoa kwa
misingi ya kuwa mimi siyo Mtanzania, hakuna wa kuniondoa hapa nchini na
nitapambana hadi hatua ya mwisho na kuhakikisha kuwa Waislamu wanapata
uhuru wao,” alinena Sheikh Ponda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba alielezea kusikitishwa kwake juu ya kauli kwamba Sheikh
Ponda asingeweza kupata dhamana katika kesi iliyokuwa ikimkabili.
“Vyombo vyetu haviko makini, tuliambiwa Ponda
hawezi kupata dhamana lakini leo hii amefungwa kifungo cha nje, hii
inatia shaka na uamuzi uliokuwa ukiendelea,” alisema Profesa Lipumba.
Mtaalamu huyo wa uchumi, alitumia nafasi hiyo kuwataka Waislamu kuungana na kuhakikisha kuwa wanatetea haki zao.
“Tuache unafiki, tuungane na kumsikiliza Ponda kwa
kauli zake, matendo yake ili kufikia kile ambacho Waislamu wanakitaka,”
alinena Profesa Lipumba.
Umati mkubwa wa waumini wa Kiislamu walimiminika
kutaka kusikia mawaidha ya katibu huyo kwa mara ya kwanza baada ya
kutoka gerezani juzi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akitoka kuswali Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, jana
chanza:mwananchi
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akitoka kuswali Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, jana
chanza:mwananchi
No comments:
Post a Comment