Sunday, May 5, 2013

Ajali yaua saba Mufindi, 44 wajeruhiwa

Watu saba wamekufa papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Kampuni ya Taqwa lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda nchini Zimbabwe, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo. Ajali hiyo uliyohusisha magari matatu ilitokea juzi jioni katika Kijiji cha Nyololo,Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo ni  basi la Taqwa aina ya Nissan Diesel lenye namba za usajili T 273 CBR (Sniper), lori la mizigo aina ya Scania, mali ya Kampuni ya Nyati Transport Ltd lililokuwa limebeba shehena ya viazi na lori la mizigo lenye namba T 104 BZZ aina ya Scania, mali ya kampuni ya Sogea Satom.

Shuhuda wa ajali hiyo,Tsiesi Chipfupa ambaye ni raia wa Zimbabwe, alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni  juzi baada ya lori la mizigo la Sogea Satom kutaka kulipita basi hilo kwa kasi na kusababisha basi la Taqwa kugongana uso kwa uso na lori la kampuni ya Nyati Transport na kusababisha vifo vya watu hao.

"Sisi tulikuwa tunatoka Dar es Salaam kwenda Harare (Zimbabwe) na tulipofika karibu na eneo la tukio, lori la mizigo (Sogea Satom) lilikuwa likitaka kutupita na ghafla nilisikia
kishindo kikubwa na gari zima lilizizima kwa vilio. Nilijikuta nalia halafu wenzangu wanavuja damu nyingi lakini pia basi letu lilikuwa limefumuka lote sehemu ya mbele hadi katikati ambako huwezi kujua ni nini kimetokea kwa muda mfupi," alisema raia huyo wa Zimbabwe.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo alisema ilitokana na mwendo kasi, imetokea katika Kijiji cha Nyololo, kilomita 25 kutoka mji wa Mafinga.

Hadi jana mchana,  waokoaji na maofisa wa Polisi wa usalama barabarani mkoa wa Iringa walikuwa wakihangaika kuokoa mali za abiria hao, waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Zimbabwe, Uganda na Malawi.

Akizungumza kwa tabu akiwa wodini katika Hospitali ya Mafinga, majeruhi wa jali hiyo, Rehema  Gaifaro mkazi wa Mbeya aliyevunjika mguu  na mkono , alisema kuwa baada ya kutokea kwa ajali hiyo, dereva wa lori lililosababisha ajali ambalo  mali ya kampuni ya Sogea Satom, alikimbilia kusikojulikana.

"Nimevunjika mguu wa kushoto na mkono wa kushoto lakini  mume wangu (Gaifaro Kaziulaya) ameumia mguu wa kushoto na mtoto wangu wa kike (Asnati Limma) amejeruhiwa  mwili wake. Namshukuru Mungu kwa kutuepusha na kifo ingawa abiria wenzetu wametangulia mbele ya haki," alisema Rehema.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk.Erick Bakuza aliiambia NIPASHE kwamba hadi kufikia saa 1 jioni juzi alikuwa amepokea miili saba ya marehemu na majeruhi 44 ambao wawili kati yao wapo mahututi kutokana na kuumia vibaya kichwani.

Alisema hadi jana, majeruhi watatu kati ya 44 walikuwa wameruhusiwa  baada ya vipimo kubaini kuwa hawakupata majeraha makubwa yanayoweza kuwafanya waendelee kubaki wodini.

"Nimepokea majeuhi 44 na maiti saba wa ajali ya basi la Taqwa ambao walikuwa wakisafiri kuelekea nchi za Zimbabwe, Uganda na Malawi. Hali zao zinaendelea vizuri isipokuwa watu wawili ambao wako mahututi na wamelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali hii ya Wilaya ya Mufindi (Mafinga)...Lakini changamoto kubwa  tunayoipata ni hapa ni namna ya kuwahudumia majeruhi wa ajali zinazotokea umbali wa kilomita 200 katika barabara kuu ya Iringa-Mbeya," alisema Dk. Bakuza.

Aliwataja waliokufa kuwa ni dereva wa basi la Taqwa, Abrahaman Abduli (32), kondakta wa basi hilo, Nassoro Rashid (27), Omari Muhusin, Alli Mussa, Joseph Charles, Emmi Kafute na maiti moja haijafahamika jina.

No comments: