Serikali imelionya kundi la wapiganaji la waasi wa M23 wanaokinzana na
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia tishio lake
la kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa Tanzania, ikisema kama
kundi hilo litajaribu kufanya uchokozi wowote, itajibu mapigo.
Pia imesema Serikali ya Malawi imerejea kwenye mazungumzo na Tanzania ya
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa.
Tishio hilo la M23 lilitolewa na kundi hilo kupitia barua yao
waliyoiwasilisha kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
na kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, lisilaumiwe
litakapofanya mauaji hayo endapo serikali ya Tanzania itaendelea na
mpango wa kupeleka askari wake kujiunga na Mpango wa Umoja wa Mataifa
(UN) wa kulinda amani nchini DRC.
Onyo la Serikali ya Tanzania dhidi ya kundi hilo, lilitolewa na Waziri
wa Wizara hiyo, Bernard Membe, wakati akijibu hoja za wabunge
waliochangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, iliyowasilishwa
na Waziri wake, Shamsi Vuai Nahodha, bungeni, jana.
Membe alisema kundi hilo limepeleka barua hiyo bungeni na wizarani
kwake, likidai kwamba, wamesema na Mungu na saini ya Mungu na imepelekwa
kwake na Mungu.
Hata hivyo, Membe alisema amebaini kuwa kundi hilo linataka kutumia jina
la Mungu kuishinikiza Serikali ya Tanzania ili kuitisha isifanye
majukumu ya kitaifa.
Alisema matishio kama hayo si mapya, kwani yaliwahi kutolewa na Kanali
Mohamed Bakar aliyejitangaza kuwa ni mtawala wa Anjouan katika visiwa
vya Comoro.
Membe alisema katika tishio hilo, Kanali Bakar aliwahi kutamka kuwa
askari wa Tanzania wakienda huko watakuwa chakula cha mamba, lakini
walipokwenda badala ya kuliwa na mamba, wao ndiwo walikula samaki na
siku ya tatu Kanali Bakar akaikimbia Anjouan, huku akiwa maevaa baibui.
“...The rest is history. Ni vitisho vinavyokuja na mtu aliyekata tamaa,” alisema Membe.
Alisema M23 wanaua, wamebaka, wamedhalilisha wazee na kina mama,
wameleta wimbi la wakimbizi 220,000 na hata 30,000 kuingia Tanzania.
Kwa vitendo hivyo viovu, alisema kundi hilo la waasi kamwe haliwezi
kumnukuu Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyesema kuwa
binadamu wote ni sawa, kwani kufanya kwao hivyo ni kukufuru.
Alisema kama M23 wangekuwa wanathamini kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa
binadamu wote ni sawa, wasingeua, kubaka na kudhalilisha wazee wenzao.
Membe alisema badala yake, wameendelea kufanya vitendo hivyo viovu hadi
kusababisha kiongozi wao, John Bosco Ndagana, kujisalimisha mwenyewe.
“Na hivi ninavyozungumza, yupo kwenye Mahakama ICC The Heague kujibu
mashtaka ya uhaini na makosa ya jinai aliyoyafanya na wenzake hao M23,”
alisema Membe.
Kutokana na hali hiyo, alisema kamwe kundi hilo la waasi haliwezi
kuwafundisha Watanzania ubinadamu, amani na wala hawawezi kutumia jina
la Mwalimu Nyerere kuwaambia kitu.
Alisema nia ya Serikali ya Tanzania ni kupata askari 4,000 wakafanye
kazi tatu DRC; ya kwanza ikiwa ni kuhakikisha M23 hawajipanui na kuleta
madhara nchini humo, kwani wako 600 na wengine wameshaanza kujiondoa
katika kundi hilo.
Membe alisema kazi ya pili, ni lazima waidhoofishe hiyo M23 kwa kuondoa
silaha zao kutoka mikononi na kule walipozificha ili DRC ibaki kuwa nchi
ya amani.
Alisema kazi ya tatu ni kujenga uhusiano, kwani ni vizuri askari
watakaoonekana kuwa bora, waingie kwenye Jeshi la Taifa la DRC ili
kuleta amani nchini humo.
“Na tutalinda amani pale. Wakituchokoza tutajibu mapigo. Lakini lengo la
kwenda pale siyo kwenda kupigana vita. Na sisi tunaenda na mandate ya
Umoja wa Mataifa ya Chapter 7 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
linapopeleka vikosi maalum kama vya kwetu haviendi kule kwa ajili ya
vita. Inakwenda kulinda amani. Na inapokosekana kuitengeneza,” alisema
Membe na kuhoji:
“Mbona Pakistan ipo pale haiwaui? India, South Africa haiwaui? Kwa nini
wawaue Watanzania tu? Au wanawaogopa vijana wetu? Jibu ni moja, ni moja
tu. Kwamba, vijana wetu na jeshi letu ni imara sana lenyewe
halishindwi. Lipo Lebanon linafanya kazi nzuri na ya kusifiwa. Lipo
Darfur linafanya kazi nzuri ya kustahili kusifiwa”
Aliwafahamisha Watanzania kuwa Kiongozi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha
UN Darfur sasa kinaongozwa na Jenerali Mtanzania, kuanzia mwezi huu
kutokana na rekodi nzuri ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ).
Alilipongeza Bunge kwa uelewa mpana na kuungana kuwa kitu kimoja
serikali inapokabiliana na vitisho vya aina hiyo na kusema Tanzania ina
nguvu na historia.
Alisema kama M23 wakitaka askari wa Tanzania wasiende DRC, basi wafanye
mambo matatu; la kwanza ikiwa ni kuanza kujitoa kwenye jeshi lao na
kujisalimisha.
Membe alisema jambo la pili, kuna mazungumzo yanayofanywa na Rais wa
Uganda, Yoweri Museveni, jijini Kampala, ya kulitaka kundi hilo pamoja
na majeshi na serikali ya DRC kukaa na kumaliza tofauti, hivyo wamalize
tofauti zao na kuwapigia simu kwamba, wameshamaliza matatizo yote.
Alisema jambo la tatu, ambalo M23 wanatakiwa walifanye ni kuacha kubaka,
kuua, kuwatawanyisha watu kutoka katika majumba yao na kwenda maporini
na kuwafanya wakimbizi ndani ya nchi yao.
Alisema Tanzania ilifanikiwa kukomboa nchi nyingi sana, hivyo
kinachofanywa ni kwenda kuleta amani kwenye nyumba ya jirani na kwamba,
baada ya amani kupatikana ndiyo wanayaomba mashirika yasiyo ya
kiserikali yanayoweza kuchangamkia fursa za huko kuwekeza.
Alisema chimbuko la tatizo la M23, lilianzia kwa wao kupigana vita ya
wenyewe kwa wenyewe, hivyo Tanzania ikapata vibali vyote vya Baraza la
Usalama la UN, AU, nchi za maziwa makuu pamoja na nchi za SADC.
“M23 wasitutishe wala hakuna cha kututisha kuzuia majeshi yetu kwenda
kulinda amani. Na nawahakikishia tumezungumza na kamati mbili ya Nje na
ya Ulinzi kwa undani zaidi ili kuomba Baraka zao na wametoa baraka kwa
niaba yenu (wabunge) wote na muikubalie serikali kwenda kutimiza wajibu,
ambao nchi hii inaendelea kupata heshima yake,” alisema Membe.
Wakati huo huo, Membe aliliambia Bunge jana kuwa hatimaye Malawi
imerejea kwenye mazungumzo na Tanzania kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa
mpaka katika Ziwa Nyasa.
Membe alisema mazungumzo hayo yataanza rasmi kwa maana ya kuitwa
kuhojiwa wizara, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwishoni mwa
mwezi huu jijini Maputo, nchini Msumbiji.
Alisema mazungumzo hayo yatakuwa yanaendelea na kusema ni imani ya
Watanzania kwamba jopo la marais wastaafu linaloongozwa na Rasi mstaafu
wa wa Msumbiji, Joachim Chisano, litafikia uamuzi.
Hata hivyo, alisema iwapo jopo hilo litawashauri kwamba mgogoro huo
ubaki kama ulivyo na kwamba, uamuzi wa kudumu inabidi wasonge mbele
kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Tanzania haitasita kufanya
hivyo, kwani ina kila aina ya ushahidi wa kuhakikisha kwamba, wanashinda
kesi hiyo.
Kuhusu askari wanaokwenda DRC pamoja na kikosi cha Malawi, alisema ni
kweli katika nchi zilizochangia kupeleka askari wake nchini humo, Malawi
ipo.
Hata hivyo, alisema ni kweli kuwa vikosi hivyo vitakuwa vinaongozwa na
Mtanzania na kwamba, taarifa walizonazo hadi sasa ni kwamba, maeneo
watakayokuwapo Malawi na Watanzania ni umbali kilomita karibu 100.
HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI
Awali Bunge liliambiwa kuwa kiongozi wa Kikundi cha Waasi cha M23 cha
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimetuma barua inayotaka wasilaumiwe
kwa mauaji ya halaiki yatakayotokea nchini iwapo Tanzania itaingia
Kongo.
Hayo yalisemwa Mchungaji Israel Natse, wakati akisoma maoni ya kambi ya
upinzani bungeni mjini Dodoma jana kuhusiana na bajeti ya Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2013/2014.
Alisema kambi rasmi ya upinzani inatambua kwamba majeshi ya nchini ni
imara na kamwe hayawezi kuacha kutimiza wajibu wao kwa sababu ya barua
ya vitisho kwa kikundi cha M23.
Alisema pamoja na kutambua uimara na uhodari wa Jeshi, kambi hiyo
inaitaka serikali kutoa majibu ya maswali mbalimbali ya kambi hiyo.
“Kwa kuwa nchi ya Malawi nayo imepeleka vikosi vya jeshi kwenye Mpango
wa umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Kongo, serikali
inalihakikishiaje Bunge hili kwamba wanajeshi wetu watakuwa salama,
ikiwa kuna mvutano kati ya Malawi na Tanzania kuhusu mgogoro wa Mpaka wa
Ziwa Nyasa?” alihoji.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai
Nahodha, alisema serikali itaanza awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba
6,064 ili kupunguza tatizo la wanajeshi kuishi uraiani.
Akisoma bajeti yake kwa mwaka 2013/2014, Vuai alisema ujenzi huo utaanza mwezi huu.
Alisema lengo ni kujenga nyumba 10,000 kwa awamu mbili za mradi wa ujenzi huo.
Nahodha alisema kazi ya ujenzi wa nyumba hizo kwa gharama ya dola za
Marekani milioni 300 na utafanywa na mkandarasi wa Kichina, Shanghai
Construction (group) General Company.
Alisema nyumba hizo zitajengwa katika vikosi 37 vilivyopo katika mikoa
ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Pemba,
Pwani na Tanga.
Aidha, alisema mazungumzo ya kupata fedha za ujenzi wa nyumba takribani 4,000 katika awamu ya pili yanaendelea.
UWEKAJI WA MIPAKA
Nahodha alisema serikali katika mwaka huu wa fedha itanunua vifaa vya
kisasa vya kupimia ardhi ili kuongeza kasi ya upimaji wa maeneo ya
Jeshi na kuondokana na migogoro kati yake na raia ambao ndio majirani
zake.
Alisema kwa sasa kuna maeneo 80 yenye migogoro katika mikoa mbalimbali.
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama iliitaka Serikali
iandae mafunzo maalumu ya Jeshi la Kujenga taifa kwa watu maalumu kama
vile viongozi wa vyama vya siasa.
Akisoma maoni hayo, Omar Nundu, alisema kamati hiyo pia imeipongeza
Serikali kwa kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa baada ya kufuta
mwaka 1994.
Wizara hiyo imeidhinishiwa jumla ya shilingi 1,102,999,529,000 ambazo
kati yake shilingi 857,417,502,000 ni kwa matumizi ya kawaida na
shilingi 245,582,027,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, alisema
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment