Sunday, April 27, 2014

WAISLAMU 1300 WAUKIMBIA MJI WA BANGUI, CAR

Televisheni ya al Alam imetangaza leo kuwa, karibu Waislamu 1300 waliokuwa wamejificha katika eneo moja la pambizoni mwa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, wamelazimika kulikimbia eneo hili kwa kuhofia kushambuliwa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka.
Taarifa zinasema kuwa Waislamu hao leo wameonekana wakiingia kwenye malori madogo 18 wakielekea maeneo ya kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya usimamizi wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, AU.
Televisheni ya al Alam imelinukuu shirika la habari la AFP likisema kuwa, mara baada ya malori yaliyowabeba Waislamu kuondoka sehemu hiyo, mamia ya wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka waliokuwa wanasubiri kwa hamu mita chache tu, wamelivamia eneo hilo ili kufanya wizi na uporaji dhidi ya mali za Waislamu hao.
Waislamu hao waliokuwa wamekimbia maeneo yao na kujificha katika eneo hilo, hawakusalimika na ukatili wa wanamgambo hao wa Kikristo ambao waliwazingira Waislamu hao hadi askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika walipofika na kuamua kuwahamisha katika eneo hilo.

No comments: