WAKATI timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikishuka
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo kucheza pambano la kirafiki la
kimataifa dhidi ya Burundi, Kocha wa muda wa Stars, Salum Mayanga,
ameahidi kuwaanzisha kikosi cha kwanza nyota wawili au watatu ‘yoso’
waliozalishwa na programu ya maboresho ya Stars.
Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inawaalika
Burundi ‘Itamba Mu Rugamba’ ikiwa ni sehemu ya Sherehe za Miaka 50 ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maandalizi ya awali kwa mechi za
kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2015), zinazotarajiwa
kufanyika mwakani nchini Morocco.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
makocha na manahodha wa timu zote walitamba kuwa tayari kuonyesha
burudani ya uhakika kuzipamba sherehe za Muungano, huku Mayanga akisema
atawapa nafasi yoso wawili au watatu, kisha kuwaongeza zaidi katika
mabadiliko yake mchezoni.
“Najua Watanzania watataka kuona matunda ya kambi ya mafunzo ya
mpango wa maboresho ya Taifa Stars, ingawa hiyo haiwezi kunifanya
nikurupuke na kuwajaza kikosini, kwani bado ni wachanga na wanahitaji
muda. Nitawaanzisha wachache, kisha wataongezeka kupitia ‘sub’
nitakazofanya,” alisema Mayanga.
Kwa upande wake, Nahodha wa Stars, Aggrey Morris, aliahidi kikosi
chake kutowaangusha Watanzania katika sherehe hizo na kwamba, nyota wake
wako tayari kwa changamoto iliyo mbele yao, huku akiwataka Watanzania
kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti.
Morris anayekipiga Azam FC, aliwataka mashabiki wa soka na Watanzania
kuwa tayari kwa matokeo yoyote, kwani soka lina aina tatu za matokeo,
ambayo ni kushinda, kufungwa ama sare, hasa ukizingatia kikosi chake
kinajumuisha nyota waliozalishwa na programu maalumu ya maboresho ya
Stars.
“Watanzania wanapaswa kuwapa muda wa kuiva kisoka vijana hawa, kabla
ya kutarajia makubwa zaidi kutoka kwao. Naamini tuna kila sababu ya
kushinda mechi hii, ambayo kwangu mimi ni kipimo sahihi kabisa kuelekea
AFCON 2015,” alisisitiza Morris.
Kwa upande wake, Kocha wa Burundi, Niyungeko Alain Olivier, alisema
vijana wake wana ari kubwa ya kushinda mechi hiyo bila kujali matokeo
yaliyopita baina ya nchi hizo, huku akielekeza matumaini yake kwa
watikisa nyavu wawili wanaosakata kabumbu nchini, Amisi Tambwe na Didier
Kavumbagu.
Kavumbagu anayekipiga Yanga na nahodha wa Burundi, aliambatana na
kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Tambwe, katika
mkutano huo. Wakali hao wanampa matumaini makubwa Olivier, ingawa
hakutaka kubainisha hilo katika mkutano huo.
Nahodha huyo wa Burundi aliahidi burudani kwa kila shabiki
atakayehudhuria mechi hiyo, huku akitaka uwepo wa ‘fair play’ kutokana
na umuhimu wa mechi kwa sherehe za Muungano, lakini pia kudumisha undugu
na ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.
Viingilio katika mechi hiyo inayotarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi
Mkenya, Anthony Ogwayo, mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa
(FIFA), vitakuwa sh 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani.
Katika jukwaa la VIP A, kiingilio kitakuwa sh 20,000, wakati VIP B na C
ni sh 10,000.
No comments:
Post a Comment