Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina hivi karibuni
ataanzisha mazungumzo na pande husika kwa minajili ya kuunda serikali ya
umoja wa kitaifa huko Palestina. Taarifa zinasema kuwa, Mahmoud Abbas
anakusudia kukutana na makundi na shakhsia mbalimbali huru ili
kujadiliana nao kuhusu mchakato wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Taarifa zinasema kuwa, Abbas atajadiliana na makundi na shakhsia hao
kuhusiana na mawaziri watakaounda serikali ya umoja wa kitaifa, na kisha
kuandaa mazingira ya kuitishwa uchaguzi wa rais na bunge. Duru za
kisiasa zinaeleza kuwa, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ana mpango
wa kuunda serikali itakayowashirikisha shakhsia huru na wasiofungamana
na mirengo ya kisiasa, akihofia radiamali itakayotolewa na utawala wa
Kizayuni wa Israel na Marekani. Inafaa kuashiria hapa kuwa, hivi
karibuni harakati za Fat–h na Hamas zilitiliana saini makubaliano ya
kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa katika kipindi cha wiki tano
zijazo, ambayo itasaidia kuondoa mivutano na mifarakano kati ya pande
hizo mbili.
No comments:
Post a Comment