CHAMA cha Albino Tanzania (TAS) kimesema maadhimisho ya tisa ya Siku
ya Albino kitaifa yatafanyika Mei 4 na itakuwa siku ya kudai haki ya
afya na uhai.
Pia kimesema kutokutekelezwa kwa haki hiyo ni sawa na kutokukidhi haki ya kuishi na kubagua sehemu ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Ofisa
Habari wa TAS, Josephat Torner, alisema maadhimisho hayo yanalenga
kuongeza ufahamu wa jamii juu ya masuala ya ualbino na utekelezaji wa
mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu.
“Mkataba huu wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu nchi yetu
imekwishausaini na kuridhia, utekelezaji wake upo katika hatua
mbalimbali, hivyo maadhimisho haya yataongeza ufahamu kwa jamii kuhusu
mikataba hii,” alisema Torner.
Alisema maadhimisho hayo yatawashirikisha wadau wa ualbino toka
mataifa mbalimbali ulimwenguni ikiwa ni pamoja na nchi za Afrika
Mashariki na Kusini, Marekani na Ulaya.
“Wageni hawa watashiriki katika mkutano wa siku moja wa kimataifa
utakaozungumzia masuala ya albino na changamoto zinazowakabili, pia
matarajio ya mkutano huu ni kupata sauti pana itakayotangaza siku hii
kimataifa,” alisema.
Alitoa rai kwa watu wote wenye ualbino, wazazi, walezi pamoja na
wadau mbalimbali kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho
hayo.
No comments:
Post a Comment