WAKATI Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku
ya Malaria, Kampuni ya RTI International ya jijini Dar es Salaam,
imesema vita dhidi ya ugonjwa huo inahitaji ushirikiano, hivyo kuzitaka
taasisi na kampuni zaidi kuungana.
Akizungumza katika kilele cha Siku ya Malaria jijini Dar es Salaam
jana, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Wadudu Waenezao Magonjwa wa RTI
International, Stephen Magesa, alikiri vita dhidi ya malaria ni ngumu,
hivyo inahitaji umoja.
Alisema kutokana na hali hiyo, alizishauri taasisi na kampuni
kushiriki katika makongamano ya vita dhidi ya malaria, yakiwamo
maadhimisho hayo ya kila mwaka na kwamba uzoefu walionao unawapa uhakika
wa kutoa msaada stahili kwa watakaohitaji.
“RTI International ina miaka 15 ya ushiriki wa maadhimisho haya,
hivyo tuna uzoefu mkubwa katika kuziongoza taasisi na kampuni mbalimbali
nchini ili kuunganisha nguvu ya kutokomeza malaria, ugonjwa unaoua
zaidi,” alisema Magesa.
Aliongeza kuwa licha ya bajeti ya serikali kwa vita dhidi ya ugonjwa
huo kuwa ndogo, ushirikiano baina ya taasisi, kampuni na wadau wa sekta
ya afya nchini ni kitu muhimu ili kuondoa tatizo hilo katika jamii.
Aliitaka serikali kwa upande wake kuzisaidia taasisi na kampuni
zilizojikita katika vita hiyo, kwa kuhakikisha inaondoa miundombinu
rafiki kwa mbu waenezao malaria, kwa kumaliza tatizo la mitaro, mabwawa,
mkusanyiko wa maji ambayo ndiyo mazalia ya mbu.
No comments:
Post a Comment