Friday, April 25, 2014

Bunge la Bajeti kuanza Mei 6

MKUTANO wa Bunge la Bajeti ya mwaka 2014/2015 utaanza Mei 6 hadi Juni 27, mwaka huu mjini Dodoma huku bajeti kuu ya Serikali ikitarajiwa kusomwa Juni 12.
Hayo yalielezwa bungeni mjini hapa jana na Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa Bunge la Katiba.
Alisema ratiba hiyo imepangwa kutokana na mabadiliko ya mzunguko wa bunge hilo yaliyofanywa mwaka jana ili kuendana na mabunge mengine ya Afrika Mashariki.
Mwandumbya alisema kwa ratiba hiyo kamati za kudumu za bunge hilo, zinaanza kukutana Aprili 28 hadi Mei  4 jijini Dar es Salaam ambapo kamati zote za kisekta na majukumu mengine zitapitia masuala yote yaliyojitokeza wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Alieleza kuwa wabunge wote watakutana Aprili 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea mapendekezo ya mpango, kiwango na ukomo wa Bajeti ya serikali ya mwaka 2014/15 kwa mujibu wa Kanuni ya 97 ya kanuni za Kudumu za Bunge mwaka za 2013.
Mwandubya alisema kamati zisizo za kisekta zikiwemo Kamati ya Bajeti, Ukimwi, Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zitaendelea na utekelezaji wa majukumu yao kama yalivyoainishwa katika kanuni za Kudumu za Bunge.
Aliongeza kuwa tofauti na kamati nyingine, Kamati za LAAC zitaanza kazi mapema ambapo zilitakiwa  kuwasili Dar es Salaam jana na kuanza kazi zake kesho.
“Kazi za kamati zitamalizika Mei 4, mwaka huu  na kwamba Bunge la Bajeti litakapoanza linatarajia pia kupitisha mapendekezo kwamba liwe linakutana kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana, kisha kuendelea jioni saa 10 hadi saa 2 usiku ikiwemo Jumamosi.
“Hata hivyo pamoja na siku hizo, bunge litakuwa likikutana siku ya Ijumaa kuanzia saa 3 asubuhi  hadi saa 6 mchana kisha kuendelea saa 10 jioni hadi saa 2 usiku, utaratibu huu ukifikiwa utawezesha muda wa kujadili bajeti kuongeka zaidi licha ya siku kupungua,” alisema Mwandumbya.

No comments: