RAIS Jakaya Kikwete ameonya kuwa mtu atakayechezea Muungano atakiona cha mtema kuni.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akilihutubia taifa kwenye
hafla ya kuwapongeza vijana wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),
waliozunguka nchini nzima kuunga mkono Muungano wa serikali mbili.
Rais Kikwete alitumia mkutano huo kulihutubia taifa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano inayoadhimishwa leo.
Rais Kikwete ambaye ametoa hotuba hiyo katika Ukumbi wa PTA jijini
Dar es Salaam, alisema kuwa leo si siku ya kuzungumza bali ni siku ya
jeshi kuonyesha umahili wao.
“Sherehe za kesho ni sherehe za jeshi ambao wamepania kuonyesha
watakavyoulinda Muungano na atakayeuchezea atakiona cha mtema kuni,”
alisema Rais Kikwete.
Bila kutaja majina, Rais Kikwete alisema kuna kundi la watu ambao
viongozi wake wanatumia milango ya VIP kusafiri, linataka kuvunja
Muungano na kusisitiza kwamba serikali itapambana kwa gharama yoyote ile
kuulinda Muungano.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja majina, lakini alikuwa akiwalenga
viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao pamoja na wajumbe
wao wameamua kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Viongozi hao, Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia na
wajumbe wao, wametoka bungeni kwa madai ya kutoridhishwa na namna Bunge
hilo linavyoendeshwa, huku baadhi ya mawaziri wa serikali wakiingia
ndani ya makanisa kuwatisha wananchi kwamba serikali tatu zikipitishwa
jeshi litapindua nchi.
UKAWA wanaeleza kuwa wametoka baada ya kuona kuwa CCM imeamua
kujadili rasimu yao badala ya ile iliyotokana na maoni ya wananchi
yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji
Joseph Warioba.
Viongozi wa UKAWA, wamekuwa wakieleza bayana kwamba hakuna mwenye nia
ya kuvunja Muungano, lakini wajumbe wanaotokana na CCM wamekuwa wakidai
kwamba UKAWA wanataka kuvunja Muungano.
Rais Kikwete alitetea dhamira yake ya kuanzisha mchakato wa Katiba
kwamba ilikuwa na nia ya kujadili kwa uwazi na mapana yale yanayotakiwa
yaingizwe au kuondolewa ndani ya Katiba ili kuondoa kero za Muungano.
“Niliwaambia siku ya kuzindua Bunge kuwa wajumbe watumie fursa hii
kutuletea katiba nzuri, fursa ambayo itaondoa matatizo ya Muungano.
“Lazima nikiri kwamba sikufurahishwa hata kidogo na baadhi ya wajumbe
kususia vikao, eti wanazunguka kwenda kushitaki kwa wananchi, sijui
wanakwenda wapi na kumshitaki nani, huko nje waendako siko, wakati wake
bado. Nawasihi warudi bungeni, hawawatendei haki wananchi wao,” alisema
Kikwete.
Rais Kikwete aliungana na viongozi wengine wanaowataka UKAWA warejee
bungeni badala ya kubaki nje ili kufanikisha upatikanaji wa Katiba.
Alisema wajumbe wa Bunge la Katiba wana matatizo na matatizo yao ni
ya mahusiano na kamwe hawawezi kupata jawabu kwa wananchi wanakokwenda
kwani watakachofanya wananchi hao ni kusikitika pamoja nao tu.
Alisema majawabu ya matatizo yao hayawezi kutatuliwa kwa wananchi
bali ndani ya Bunge ambalo wameliwekea kanuni ya namna ya kumaliza
matatizo yao.
Rais Kikwete pia alielezea lugha iliyokuwa ikitumiwa na wajumbe hao
kwamba si nzuri kwani haina staha, hivyo aliwataka wajue kuwa haiba na
vitendo vyao viendane na hadhi yao.
Kuhusu hati ya Muungano ambayo ilikuwa gumzo ndani ya Bunge, Rais
Kikwete alisema aliamua kuitoa hati hiyo hadharani baada ya kuona Bunge
linataka kupoteza mwelekeo.
“Nilipoona mjadala unapoteza mwelekeo, nikamwita Katibu Mkuu
Kiongozi, nikamwambia itoe hadharani, tumeitoa, kelele zikaanza kwamba
saini ya Karume imeghushiwa,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment