HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa imetenga sh milioni
115.5 kwa ajili ya kutekeleza pambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi kwa
mwaka wa fedha 2014/2015.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wilaya wa Kudhibiti Ukimwi, Peter Mbosa,
alieleza hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika
kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni.
Alisema fedha hizo zinatokana na chanzo cha mapato mengine na msaada
kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kwa lengo la
kutekeleza shughuli mbalimbali za mapambano dhidi ya ukimwi.
Mbosa alisema sh milioni 3.3 zitatumika katika kutoa huduma za dawa
za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika vijiji vya
Mawambala na Ipalamwa.
Wakichangia hoja wakati wa kujadili matumizi sahihi ya fedha hizo,
baadhi ya madiwani walisema huduma za upatikanaji wa dawa za kupunguza
makali ya VVU ziwafikie walengwa kwa wakati na zitolewe katika vituo
vyote vya afya.
Pia walisema kuna umuhimu wa kuhamasisha wananchi kwenda kupima afya
zao na kuishi maisha ya uaminifu ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
No comments:
Post a Comment