Sunday, April 27, 2014

MKAKATI WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA PALEST. WAANZA

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina hivi karibuni ataanzisha mazungumzo na pande husika kwa minajili ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa huko Palestina. Taarifa zinasema kuwa, Mahmoud Abbas anakusudia kukutana na makundi na shakhsia mbalimbali huru ili kujadiliana nao kuhusu mchakato wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Taarifa zinasema kuwa, Abbas atajadiliana na makundi na shakhsia hao kuhusiana na mawaziri watakaounda serikali ya umoja wa kitaifa, na kisha kuandaa mazingira ya kuitishwa uchaguzi wa rais na bunge. Duru za kisiasa zinaeleza kuwa, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ana mpango wa kuunda serikali itakayowashirikisha shakhsia huru na wasiofungamana na mirengo ya kisiasa, akihofia radiamali itakayotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani. Inafaa kuashiria hapa kuwa, hivi karibuni harakati za Fat–h na Hamas zilitiliana saini makubaliano ya  kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa katika kipindi cha wiki tano zijazo, ambayo itasaidia kuondoa mivutano na mifarakano kati ya pande hizo mbili.

WAISLAMU 1300 WAUKIMBIA MJI WA BANGUI, CAR

Televisheni ya al Alam imetangaza leo kuwa, karibu Waislamu 1300 waliokuwa wamejificha katika eneo moja la pambizoni mwa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, wamelazimika kulikimbia eneo hili kwa kuhofia kushambuliwa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka.
Taarifa zinasema kuwa Waislamu hao leo wameonekana wakiingia kwenye malori madogo 18 wakielekea maeneo ya kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya usimamizi wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, AU.
Televisheni ya al Alam imelinukuu shirika la habari la AFP likisema kuwa, mara baada ya malori yaliyowabeba Waislamu kuondoka sehemu hiyo, mamia ya wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka waliokuwa wanasubiri kwa hamu mita chache tu, wamelivamia eneo hilo ili kufanya wizi na uporaji dhidi ya mali za Waislamu hao.
Waislamu hao waliokuwa wamekimbia maeneo yao na kujificha katika eneo hilo, hawakusalimika na ukatili wa wanamgambo hao wa Kikristo ambao waliwazingira Waislamu hao hadi askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika walipofika na kuamua kuwahamisha katika eneo hilo.

TSVANGIRAI ASIMAMISHWA UONGOZI MDC

Chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change MDC kimesema kimemsimamisha kiongozi wake Morgan Tsvangirai kwa kukiuka kanuni za kidemokrasia.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa MDC Tendai Biti kufuatia mkutano wa chama hicho uliofanyika katika mji Mkuu Harare.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilifikia kikomo mwezi julai mwaka 2013 baada ya Rais Mugabe kushinda kwa wingi wa kura katika uchaguzi wa rais na Tsvangirai kususia uchaguzi kwa madai ya udanganyifu.
Kushindwa kwake kulipunguza nguvu yake kama kiongozi ambaye alikuwa mshindani mkuu wa Rais Mugabe.
Waangalizi wanasema ndani ya MDC kumekuwa na mgogoro wa kiuongozi kwa miezi kadhaa.
Viongozi wengine wa ngazi za juu wameripotiwa kusimamishwa katika mkutano huo uliofanyika siku ya jumamosi na wanachama wengine wa chama hicho watachukua nafasi zao.

WAFUASI 11 WA MORSI WAHUKUMIWA JELA

Mahakama moja nchini Misri imewahukumu wafuasi 11 wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Mohammed Morsi kifungo cha kati ya miaka mitano hadi minane jela kwa kufanya maandamano. Washtakiwa hao walikamatwa kufuatia msururu wa ghasia zilizozuka baada ya kundolewa madarakani kwa Mohammed Morsi mwaka uliopita.
Mnamo mwezi Machi, zaidi ya wafuasi 500 wa Mohammed Morsi walihukumiwa kifo katika mahakama hiyo hiyo.
kesi hiyo inajiri wakati ambapo kuna msako dhidi ya waislamu wenye itikadi kali wanaomuunga mkono Mohammed Morsi.

Waziri mkuu nchini Korea Kusini ajiuzulu

Waziri mkuu nchini Korea Kusini amejiuzulu kutokana na vile serikali yake ilivyolichukulia swala lote la ferry iliozama siku kumi na moja zilizopita. Chung Hong Won amesema kuwa kusalia afisini ni mzigo mkubwa kwake.
Bwana Chung alizomwa alipozitembelea familia za waathiriwa waliotoweka katika ferry hiyo ya Sewol,baada ya kuzama katika hali ya kutatanisha.
Takriban watu 200 wanadaiwa kufa maji katika tukio hilo huku zaidi ya mamia wengine wakiwa hawajulikani waliko,wengi wao wakiwa wanafunzi na walimu waliokuwa wakielekea katika ziara ya shule.
Wapiga mbizi bado wanaendelea kuwasaka waathiriwa chini ya ferry hiyo iliozama.
Ripoti za awali zimedai kuwa watu wote wametolewa katika boti hiyo.
(bbc)

VIONGOZI WA CCM SENGEREMA WAVURUGANA

 Sengerema
Katibu wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Bw Mohamed Shaaban Mohamed,  amekuwa na malumbano na viongozi  wa umoja wa vijana UVCCM  Bw Robert Madaha na Bw Benedicto Bujiku baada ya mwenyekiti wa umoja huo Bw Madaha kusema hatoshi katika nafasi yake ya ukatibu  kwa viongzi wa mkoa walipokuja kuhudhuria kwenye kikao cha kamati ya siasa wilaya sengerema kilichofanyika march 22, mwaka huu.
 
Wakiongea na mwandishi wa habari hizi  kwa nyakati tofauti viongozi hao wa  umoja wa vijana  walisema kuwa hawakuwahi kuwa na malumbano yoyote na katibu wa chama hicho Bw Mohamed isipokuwa malumbano yao yalianza march mwaka huu baada ya viongozi wa mkoa kuwasili sengerema march mwaka huu kwa lengo la kujadili watumishi wa chama katika mienendo yao ya kazi.
 
Aidha Madaha aliongeza kuwa baada ya kumaliza kikao baadhi ya wajumbe ambao sio waadilifu walivujisha siri na kumwambia Katibu wao kuwa hatoshi katika nafasi yake apelekwe mtu mwingine atakaeziba pengo lake ambapo tangu hapo Mohamed alianza ktafuta visa vya kumng’oa nafasi yake ili asiwe anahudhuria kamati ya siasa wilaya.
 
“Mimi Mohamed mambo yote anayoniundia ya vijana kunipiga mawe ni kwasababu tu walikuja katibu wa CCM Mkoa akiwa na baadhi ya viongozi wenzake kwenye kamati ya siasa ya mwezi wa tatu…… katika kujadili masuala ya watumishi baadhi walitoka nje ili tujadili na tukajadili vizuri na ilipofika zamu ya wengine nao walitoka wakajadiliwa ila sasa baada ya hapo kuna mwenzetu mmoja ambaye ni diwani mwenzangu sipendi kumtaja jina alimfuata katibu na kumwambia kuwa madaha amekuharibia kwa viongozi” alisema madaha.
 
Hata hivyo baada ya siku chache kupita inasadikiwa katibu wa CCM wilaya aliwahamasisha wajumbe na wasiokuwa wajumbe wa umoja wa vijana CCM  kwenda polisi kufungua kesi ya wizi wa pikipiki za umoja huo ambapo walifanikiwa kufika polisi na kufungua kesi ya wizi wa pikipiki na hadi sasa inaendelea.
 
Aidha upotevu wa pikipiki hizo pia kuna muhusisha katibu wake wa vijana ambapo baada ya kumuhoji katibu huo wa vijana kuhusiana na upotevu wa piki piki hizo alidai kuwa kweli pikipiki hizo waliziuza kwa watu watatu tofauti na bei tofauti kutokana na ubora wake na kuongeza kuwa waliziuza kisheria kwa kufuata utaratibu wa umoja wao, ambapo kamati nzima tendaji ilikaa kikao cha kuuza piki piki hizo na wajumbe waliohudhuria walisaini kitabu cha mahudhulio.
 
  Nashangaa kwanini Mohamedi ananing’ang’ania mimi wakati piki piki ziliuzwa tangu mwaka jana kabla hata hajaja alikuwepo Yule katibu mwingine Magdalena leo hii baada ya kukorofishana na madaha tu na mimi naingizwa katika mkumbo huo yeye alisema shida yake ni mwenyekiti wa vijana na sio mimi……. Ndugu mwandishi kinachogomba hapo ni mimi kuwa karibu na m/kiti wangu haaya yote ni majungu ya kisiasa tu hakuna ukweli wowote.” Alisema Bujiku.
 
Katibu wa chama hicho alipoulizwa kuhusu suala hilo alichojibu shida yake ni umwenyekiti wa umoja huo  na sio udiwani wa Madaha ambapo alisisitiza kuwa mwenyekiti huyo ajiuzuru wadhifa wake, na kuongeza kuwa ili Bujiku apone aachane na madaha na akiendelea kuwa nae pamoja ataharibikiwa.
 Na Dotto Mgaza

MWANZA WATAKIWA KUDUMISHA MUUNGANO

 
Wananchi mkoani Mwanza,  wametakiwa kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kuwaenzi waasisi wa taifa hili hayati Amani Karume na Mwl Julias kambarage Nyerere kwa kutenda mema waliyoyafanya.
 
Kauli hiyo ilitolewa na mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Ilemela Amina Masenza ambaye alikuwa akimwaakilisha mkuu waa mkoa wa Mwanza Eng Evarist Ndikillo alipokuwa akiwahutubia mamia ya watu  kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya muungano ambayo kimkoa yalifanyika katika  viwanja vya shule ya msingi Sengerema kata ya Nyampulukano wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
 
Bi Masenza alisema kuwa wananchi wote kwa ujumla wanatakiwa kudumisha muungano  wa Tanganyika na Zanzibar kwa  amani na utulivu na kuwaepuka wanasiasa wenye uchu wa madaraka na wapotoshaji ambao wanataka kuvuruga amani ya nchi  ya Tanzania kwa maslahi yao binafsi .
 
“Kuna kila sababu ya kuwakumbuka viongozi wetu hawa wawili Karume na Nyerere  kwani leo hii tunaadhimishaa miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa wao kutuonganisha, tumekuwa tukifanya biashara kwa pamoja na kuoleana” alisema Bi Masenza
 
Aidha aliongeza kuwa wananchi waliowengi walizoea serikali mbili ambapo muungano utakapovunjika wananchi wengine hawana pa kukimbilia.
 
Pia katika hotuba yake alikemea ubaguzi wa rangi na ukabila na kuwaasa wana Mwanza kudumisha muungano na kuonyesha mbegu bora walizopanda ambapo changamoto za muungano ni fursa na sio kuvuruga amani ya nchi.
 
“ Hatma ya muungano wetu ipo mikononi mwetu…… tuimarishe muungano wetu..” alisema Bi Masenza.
Na Dotto Mgaza- Sengerema

Friday, April 25, 2014

MEZA YA MAGEZETI LEO JUMAMOSI









Macho yote vipaji vipya Stars leo

WAKATI timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikishuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo kucheza pambano la kirafiki la kimataifa dhidi ya Burundi, Kocha wa muda wa Stars, Salum Mayanga, ameahidi kuwaanzisha kikosi cha kwanza nyota wawili au watatu ‘yoso’ waliozalishwa na programu ya maboresho ya Stars. Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inawaalika Burundi ‘Itamba Mu Rugamba’ ikiwa ni sehemu ya Sherehe za Miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maandalizi ya awali kwa mechi za kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2015), zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini Morocco.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, makocha na manahodha wa timu zote walitamba kuwa tayari kuonyesha burudani ya uhakika kuzipamba sherehe za Muungano, huku Mayanga akisema atawapa nafasi yoso wawili au watatu, kisha kuwaongeza zaidi katika mabadiliko yake mchezoni.
“Najua Watanzania watataka kuona matunda ya kambi ya mafunzo ya mpango wa maboresho ya Taifa Stars, ingawa hiyo haiwezi kunifanya nikurupuke na kuwajaza kikosini, kwani bado ni wachanga na wanahitaji muda. Nitawaanzisha wachache, kisha wataongezeka kupitia ‘sub’ nitakazofanya,” alisema Mayanga.
Kwa upande wake, Nahodha wa Stars, Aggrey Morris, aliahidi kikosi chake kutowaangusha Watanzania katika sherehe hizo na kwamba, nyota wake wako tayari kwa changamoto iliyo mbele yao, huku akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti.
Morris anayekipiga Azam FC, aliwataka mashabiki wa soka na Watanzania kuwa tayari kwa matokeo yoyote, kwani soka lina aina tatu za matokeo, ambayo ni kushinda, kufungwa ama sare, hasa ukizingatia kikosi chake kinajumuisha nyota waliozalishwa na programu maalumu ya maboresho ya Stars.
“Watanzania wanapaswa kuwapa muda wa kuiva kisoka vijana hawa, kabla ya kutarajia makubwa zaidi kutoka kwao. Naamini tuna kila sababu ya kushinda mechi hii, ambayo kwangu mimi ni kipimo sahihi kabisa kuelekea AFCON 2015,” alisisitiza Morris.
Kwa upande wake, Kocha wa Burundi, Niyungeko Alain Olivier, alisema vijana wake wana ari kubwa ya kushinda mechi hiyo bila kujali matokeo yaliyopita baina ya nchi hizo, huku akielekeza matumaini yake kwa watikisa nyavu wawili wanaosakata kabumbu nchini, Amisi Tambwe na Didier Kavumbagu.
Kavumbagu anayekipiga Yanga na nahodha wa Burundi, aliambatana na kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Tambwe, katika mkutano huo. Wakali hao wanampa matumaini makubwa Olivier, ingawa hakutaka kubainisha hilo katika mkutano huo.
Nahodha huyo wa Burundi aliahidi burudani kwa kila shabiki atakayehudhuria mechi hiyo, huku akitaka uwepo wa ‘fair play’ kutokana na umuhimu wa mechi kwa sherehe za Muungano, lakini pia kudumisha undugu na ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.
Viingilio katika mechi hiyo inayotarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi Mkenya, Anthony Ogwayo, mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), vitakuwa sh 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Katika jukwaa la VIP A, kiingilio kitakuwa sh 20,000, wakati VIP B na C ni sh 10,000.

Miradi ya TASAF yawainua wakazi Chamwino

WAKAZI wa Kijiji cha Ndogowe na Ng’ambaku katika Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, wamesema miradi inayosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imekuwa mkombozi wa kuwaondolea umaskini.
Aidha, walieleza miradi hiyo imewafanya kuondokana na hali ya kuwa ombaomba na badala yake wameweza kujenga utamaduni wa kujitegemea.
Wakazi hao walibainisha hayo kwa nyakati tofauti walipozungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalumu juu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TASAF kwa lengo la kuzinusuru familia lengwa katika hali ya umaskini.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Axa Mporo (78), ambaye ni mjane alisema kabla ya Tasaf kumuingiza katika mpango wa miradi ya kunusuru kaya maskini alikuwa ombaomba wa kutupwa.
Alisema alikuwa hawezi kufanya jambo lolote na wakati huo alikuwa ni mtu wa kuombaomba, kwani hakuwa na uwezo hata wa kununua chumvi.
“Nilikuwa siwezi kufanya jambo lolote na nilikuwa maskini kweli kweli, mume wangu alikuwa ni kibarua, lakini zaidi mimi nilikuwa siwezi kununua  hata chumvi. Mume wangu alipofariki dunia maisha ndiyo yakazidi kuwa mabaya,” alisema.
Alisema baada ya kuingizwa katika mradi huo na kupatiwa elimu na kisha kupatiwa fedha alinunua shamba kwa ajili ya kilimo na kwamba kwa sasa anaweza kupata chakula na hata huduma za matibabu.
“Tasaf wamekuwa mkombozi wa maisha yangu, kwani sasa napendeza tofauti na awali wakati nikiombaomba,” alisema Axa.
Katibu wa mpango wa uwahilishaji fedha kwa kunusuru kaya maskini, Mussa Mwendi, alisema miradi ya kunusuru kaya maskini ilianza mwaka 2010 ikiwa na walengwa 162 na kwa sasa wapo walengwa 276.
Alisema tangu kuanza kwa miradi ya maendeleo hadi sasa jumla ya sh milioni 59.3 zimewafikia familia lengwa ambazo ni maskini.
Mkurugenzi Mratibu wa Tasaf, Alphonce Kyaliga, aliwataka wanavikundi ambao ni kaya lengwa kuhakikisha wanajihusisha katika miradi ya maendeleo kwa lengo la kujinusuru katika dimbwi la umaskini.

Mil. 115/- kukabili ukimwi Kilolo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa imetenga sh milioni 115.5 kwa ajili ya kutekeleza pambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wilaya wa Kudhibiti Ukimwi, Peter Mbosa, alieleza hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni.
Alisema fedha hizo zinatokana na  chanzo cha mapato mengine na msaada kutoka  Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kwa lengo la kutekeleza shughuli mbalimbali za mapambano dhidi ya ukimwi.
Mbosa alisema sh milioni 3.3 zitatumika katika kutoa huduma za dawa za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika vijiji vya Mawambala na Ipalamwa.
Wakichangia hoja wakati wa kujadili matumizi sahihi ya fedha hizo, baadhi ya madiwani walisema huduma za upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU ziwafikie walengwa kwa wakati na zitolewe katika vituo vyote vya afya.
Pia walisema kuna umuhimu wa kuhamasisha wananchi kwenda kupima afya zao na kuishi maisha ya uaminifu ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

Siku ya Albino Mei 4

CHAMA cha Albino Tanzania (TAS) kimesema maadhimisho ya tisa ya Siku ya Albino kitaifa yatafanyika Mei 4 na itakuwa siku ya kudai haki ya afya na uhai.
Pia kimesema kutokutekelezwa kwa haki hiyo ni sawa na kutokukidhi haki ya kuishi na kubagua sehemu ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Ofisa Habari wa TAS, Josephat Torner, alisema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza ufahamu wa jamii juu ya masuala ya ualbino na utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu.
“Mkataba huu wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu nchi yetu imekwishausaini na kuridhia, utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali, hivyo maadhimisho haya yataongeza ufahamu kwa jamii kuhusu mikataba hii,” alisema Torner.
Alisema maadhimisho hayo yatawashirikisha wadau wa ualbino toka mataifa mbalimbali ulimwenguni ikiwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki na Kusini, Marekani na Ulaya.
“Wageni hawa watashiriki katika mkutano wa siku moja wa kimataifa utakaozungumzia masuala ya albino na changamoto zinazowakabili, pia matarajio ya mkutano huu ni kupata sauti pana itakayotangaza siku hii kimataifa,” alisema.
Alitoa rai kwa watu wote wenye ualbino, wazazi, walezi pamoja na wadau mbalimbali kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.

RTI yataka ushirikiano vita ya malaria

WAKATI Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Malaria, Kampuni ya RTI International ya jijini Dar es Salaam, imesema vita dhidi ya ugonjwa huo inahitaji ushirikiano, hivyo kuzitaka taasisi na kampuni zaidi kuungana. Akizungumza katika kilele cha Siku ya Malaria jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Wadudu Waenezao Magonjwa wa RTI International, Stephen Magesa, alikiri vita dhidi ya malaria ni ngumu, hivyo inahitaji umoja.
Alisema kutokana na hali hiyo, alizishauri taasisi na kampuni kushiriki katika makongamano ya vita dhidi ya malaria, yakiwamo maadhimisho hayo ya kila mwaka na kwamba uzoefu walionao unawapa uhakika wa kutoa msaada stahili kwa watakaohitaji.
“RTI International ina miaka 15 ya ushiriki wa maadhimisho haya, hivyo tuna uzoefu mkubwa katika kuziongoza taasisi na kampuni mbalimbali nchini ili kuunganisha nguvu ya kutokomeza malaria, ugonjwa unaoua zaidi,” alisema Magesa.
Aliongeza kuwa licha ya bajeti ya serikali kwa vita dhidi ya ugonjwa huo kuwa ndogo, ushirikiano baina ya taasisi, kampuni na wadau wa sekta ya afya nchini ni kitu muhimu ili kuondoa tatizo hilo katika jamii.
Aliitaka serikali kwa upande wake kuzisaidia taasisi na kampuni zilizojikita katika vita hiyo, kwa kuhakikisha inaondoa miundombinu rafiki kwa mbu waenezao malaria, kwa kumaliza tatizo la mitaro, mabwawa, mkusanyiko wa maji ambayo ndiyo mazalia ya mbu.

Bunge la Bajeti kuanza Mei 6

MKUTANO wa Bunge la Bajeti ya mwaka 2014/2015 utaanza Mei 6 hadi Juni 27, mwaka huu mjini Dodoma huku bajeti kuu ya Serikali ikitarajiwa kusomwa Juni 12.
Hayo yalielezwa bungeni mjini hapa jana na Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa Bunge la Katiba.
Alisema ratiba hiyo imepangwa kutokana na mabadiliko ya mzunguko wa bunge hilo yaliyofanywa mwaka jana ili kuendana na mabunge mengine ya Afrika Mashariki.
Mwandumbya alisema kwa ratiba hiyo kamati za kudumu za bunge hilo, zinaanza kukutana Aprili 28 hadi Mei  4 jijini Dar es Salaam ambapo kamati zote za kisekta na majukumu mengine zitapitia masuala yote yaliyojitokeza wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Alieleza kuwa wabunge wote watakutana Aprili 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea mapendekezo ya mpango, kiwango na ukomo wa Bajeti ya serikali ya mwaka 2014/15 kwa mujibu wa Kanuni ya 97 ya kanuni za Kudumu za Bunge mwaka za 2013.
Mwandubya alisema kamati zisizo za kisekta zikiwemo Kamati ya Bajeti, Ukimwi, Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zitaendelea na utekelezaji wa majukumu yao kama yalivyoainishwa katika kanuni za Kudumu za Bunge.
Aliongeza kuwa tofauti na kamati nyingine, Kamati za LAAC zitaanza kazi mapema ambapo zilitakiwa  kuwasili Dar es Salaam jana na kuanza kazi zake kesho.
“Kazi za kamati zitamalizika Mei 4, mwaka huu  na kwamba Bunge la Bajeti litakapoanza linatarajia pia kupitisha mapendekezo kwamba liwe linakutana kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana, kisha kuendelea jioni saa 10 hadi saa 2 usiku ikiwemo Jumamosi.
“Hata hivyo pamoja na siku hizo, bunge litakuwa likikutana siku ya Ijumaa kuanzia saa 3 asubuhi  hadi saa 6 mchana kisha kuendelea saa 10 jioni hadi saa 2 usiku, utaratibu huu ukifikiwa utawezesha muda wa kujadili bajeti kuongeka zaidi licha ya siku kupungua,” alisema Mwandumbya.

JK: Atakayechezea Muungano kukiona

RAIS Jakaya Kikwete ameonya kuwa mtu atakayechezea Muungano atakiona cha mtema kuni. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akilihutubia taifa kwenye hafla ya kuwapongeza vijana wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), waliozunguka nchini nzima kuunga mkono Muungano wa serikali mbili.
Rais Kikwete alitumia mkutano huo kulihutubia taifa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano inayoadhimishwa leo.
Rais Kikwete ambaye ametoa hotuba hiyo katika Ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam, alisema kuwa leo si siku ya kuzungumza bali ni siku ya jeshi kuonyesha umahili wao.
“Sherehe za kesho ni sherehe za jeshi ambao wamepania kuonyesha watakavyoulinda Muungano na atakayeuchezea atakiona cha mtema kuni,” alisema Rais Kikwete.
Bila kutaja majina, Rais Kikwete alisema kuna kundi la watu ambao viongozi wake wanatumia milango ya VIP kusafiri, linataka kuvunja Muungano na kusisitiza kwamba serikali itapambana kwa gharama yoyote ile kuulinda Muungano.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja majina, lakini alikuwa akiwalenga viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao pamoja na wajumbe wao wameamua kususia vikao  vya Bunge Maalumu la Katiba.
Viongozi hao, Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia na wajumbe wao, wametoka bungeni kwa madai ya kutoridhishwa na namna Bunge hilo linavyoendeshwa, huku baadhi ya mawaziri wa serikali wakiingia ndani ya makanisa kuwatisha wananchi kwamba serikali tatu zikipitishwa jeshi litapindua nchi.
UKAWA wanaeleza kuwa wametoka baada ya kuona kuwa CCM imeamua kujadili rasimu yao badala ya ile iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Viongozi wa UKAWA, wamekuwa wakieleza bayana kwamba hakuna mwenye nia ya kuvunja Muungano, lakini wajumbe wanaotokana na CCM wamekuwa wakidai kwamba UKAWA wanataka kuvunja Muungano.
Rais Kikwete alitetea dhamira yake ya kuanzisha mchakato wa Katiba kwamba ilikuwa na  nia ya kujadili kwa uwazi na mapana yale yanayotakiwa yaingizwe au kuondolewa ndani ya Katiba ili kuondoa kero za Muungano.
“Niliwaambia siku ya kuzindua Bunge kuwa wajumbe watumie fursa hii kutuletea katiba nzuri, fursa ambayo itaondoa matatizo ya Muungano.
“Lazima nikiri kwamba sikufurahishwa hata kidogo na baadhi ya wajumbe kususia vikao, eti wanazunguka kwenda kushitaki kwa wananchi, sijui wanakwenda wapi na kumshitaki nani, huko nje waendako siko, wakati wake bado. Nawasihi warudi bungeni, hawawatendei haki wananchi wao,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete aliungana na viongozi wengine wanaowataka UKAWA warejee bungeni badala ya kubaki nje ili kufanikisha upatikanaji wa Katiba.
Alisema  wajumbe wa Bunge la Katiba wana matatizo na matatizo yao ni ya mahusiano na kamwe hawawezi kupata jawabu kwa wananchi wanakokwenda kwani watakachofanya wananchi hao ni kusikitika pamoja nao tu.
Alisema majawabu ya matatizo yao hayawezi kutatuliwa kwa wananchi bali ndani ya Bunge ambalo wameliwekea kanuni ya namna ya kumaliza matatizo yao.
Rais Kikwete pia alielezea lugha iliyokuwa ikitumiwa na wajumbe hao kwamba si nzuri kwani haina staha, hivyo aliwataka wajue kuwa haiba na vitendo vyao viendane na hadhi yao.
Kuhusu hati ya Muungano ambayo ilikuwa gumzo ndani ya Bunge, Rais Kikwete alisema aliamua kuitoa hati hiyo hadharani baada ya kuona Bunge linataka kupoteza mwelekeo.
“Nilipoona mjadala unapoteza mwelekeo, nikamwita Katibu Mkuu Kiongozi, nikamwambia itoe hadharani, tumeitoa, kelele zikaanza kwamba saini ya Karume imeghushiwa,” alisema Rais Kikwete.

Jukata: Rais Kikwete si refa mzuri

JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata) limesema Rais Jakaya Kikwete, amepoteza urefa aliouvaa wakati anaanzisha mchakato wa kupata Katiba na kuvaa jezi ya chama kimoja. Jukata wameeleza kuwa kutokana na hali hiyo Bunge la Katiba limepata mpasuko huku Mwenyekiti wake, Samuel Sitta, akipwaya kiuamuzi kutokana na kutokemea mivutano na uhalalishaji wa kuvunja kanuni.
Aidha, Jukata wamemuomba Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta na Patrice Lumumba, kutoka Kenya kusaidia kusimamia unasuaji wa mchakato wa katiba unaoonekana kukwama baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba, alisema bila upatanisho mchakato huo utakwama na kuongeza kuwa kwa sasa Kikwete amepoteza uwezo wa kusuluhisha.
Kibamba alisema baada ya UKAWA kutoka nje ya Bunge na kugoma kurudi kumeleta pigo katika mchakato wa katiba na kutia dosari iliyosababisha matusi na mivutano.
“Rais lazima atambue kuwa si rais wa CCM pekee bali ni rais wa watu wote, hivyo kujionyesha kuegemea upande mmoja kunaleta mpasuko kwa taifa… rais alipaswa kujizuia katika kutamka misimamo yake ya nini anataka kwenye Katiba,” alisema Kibamba.
Katika tathmini iliyofanywa na jukwaa hilo imebaini kuwa kuingia moja kwa moja kwa wabunge na wawakilishi kwenye Bunge maalumu la Katiba ndiyo sababu ya mchakato huo kuwa hapo ulipo.
Alisema tathmini yao imebaini kuwapo na migongano ya kimasilahi kuhusu wanasiasa na masilahi yao ya vyeo na mapato.
“Ukiisoma rasimu ya pili ya katiba inaeleza kuwa kutakuwa na wabunge 75, sasa piga hesabu kutoka 360 hadi 75 hapo lazima viongozi wapate hofu,” alisisitiza.
Pia alisema sheria ya mabadiliko ya katiba sura ya 83 ya sheria za Tanzania imempa rais madaraka kwa hatua zote za mchakato huo.
Alisema mivutano iliyopo sasa imesababishwa na kupindishwa kwa sheria wakati wa ufunguzi wa bunge hilo hali iliyosababisha kuchochea kuligawa kivyama, kimisimamo na kiitikadi.
Aidha, alisema kuwa kitendo cha viongozi wa dini kuegemea pande kunaendeleza mivurugano na kuongeza kuwa viongozi hao wanapaswa kuongoza toba ya taifa na si kuongoza kulipasua taifa kwa kauli zao.
“Tusahihishe makosa katika mchakato wa katiba na hasa sheria ya mabadiliko ya katiba ili kuweka sawa mambo yenye utata yahusuyo elimu ya uraia, demokrasia ya mijadala na mamlaka ya wananchi katika mchakato huo,” alisema.
Kibamba aliongeza kuwa tangu kuanza kwa mchakato wa katiba Desemba 31, 2010 hadi jana bado imeshindikana kupatikana katiba mpya ambayo ilipangwa kuzinduliwa leo sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya  Muungano.

Kingunge awalipua CCM

MWANASIASA mkongwe na Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale – Mwiru, amesema makada wenzake wanaomshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wanakitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema kumtukana au kumshambulia Jaji Warioba, au wajumbe wengine wa tume hiyo ni sawa na kukitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza serikali.
Kingunge alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akichangia sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba, ambapo alisema wanaomshambulia Jaji Warioba wanaonyesha utovu wa adabu, kwa kuwa chama kina maadili na adabu katika kushughulikia masuala mbalimbali.
“Mimi sitakubali hata kidogo wajumbe watumie msimamo wa chama kumshambulia Warioba au wajumbe wengine wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, si halali kumshambulia Warioba au mjumbe yeyote yule binafsi.

“Mimi ni Mwana CCM niliyeondoka madarakani siku nyingi lakini naamini kuwa kumtukana mwenzetu ni sawa na kukitukana chama na sisi tuliopo hapa, wanaomshambulia Warioba wanakosea sana, hapa tuna  rasimu ya Katiba ambayo ina mawazo tu, hakuna watu ndani ya rasimu hiyo, hatupaswi kukiuka maadili kwa kuwatukana au kuwakashifu watu,” alisema.
Alisema kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba si uamuzi wa mwisho, hivyo wajumbe hawana sababu ya kumsema, kumtukana au kumkejeli mtu yeyote aliyekuwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kingunge pia alitumia fursa hiyo kukemea lugha za matusi, vijembe na kejeli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wajumbe kwenye mijadala mbalimbali.
“Hatuwezi kukaa hapa ndani kwa kudhalilishana, wale waliokuwa wakitumia lugha hizo walikuwa wanatudhalilisha wote. Wengine walitumia lugha hizo kwa waasisi wetu…Unyenyekevu ni sura moja ya msomi ambaye ametumia fedha za Watanzania kupata elimu yake,” alisema.
Alisema wajumbe wamekwenda bungeni kuwatafutia wananchi wenzeo Katiba mpya, iliyo bora na lazima izingatie miaka 50  ya muungano ambao umekuwa na mafanikio makubwa.
“Katiba bora lazima iimarishe yale mafanikio tuliyoyapata katika kipindi hicho ikiwemo muungano, umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na kuunda mazingira ya amani na utulivu, kama haiimarishi, haifai hata kidogo. Haya mafanikio yote yametokana na muundo wa serikali mbili ulioasisiwa na wazee wetu,” alisema.
Hakuna Katiba bila UKAWA
Kingunge alisema kuwa ili Tanzania ipate Katiba mpya iliyo bora, lazima kuwepo maelewano ya kuwashirikisha wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Alisema kitendo cha wajumbe wa UKAWA kususia vikao vya Bunge, kinaonyesha upungufu mkubwa walionao lakini Katiba mpya haitaweza kupatikana bila ya wao.
Kingunge aliwaomba wajumbe wa UKAWA warejee bungeni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa Katiba ya wananchi.
Alisema hata UKAWA wakirejea bungeni ni vema wajumbe wakatambua kuwa kupatikana kwa Katiba mpya kunahitaji maridhiano ya pande hizo mbili.
“Hatuwezi kupata theluthi mbili ya kura hasa kwa wajumbe wa kutoka Zanzibar watakaohalalisha maamuzi yetu bila kushirikiana na wenzetu, lazima tuzungumze, theluthi mbili ni takwa la kisheria, hatuwezi kulikwepa,” alisema.
Kingunge alisema kwa muda mrefu Zanzibar kulikuwa na mfarakano mkubwa kati ya CCM na CUF lakini yalifanyika mazungumzo yaliyodumu kwa takriban miaka 13.
“Tumezungumza kwa muda mrefu tangu 1998 lakini hatimaye tulibuni suala la kugawana madaraka…katika hali ya Zanzibar tulisema haiwezekani lazima tukubaliane, sasa Zanzibar imetulia. Ni kutokana na mazungumzo hayo.
“Suala la Katiba mpya si utani  ni lazima tukubali tuzungumze mpaka tuelewane….humu ndani sisi wajumbe tuzungumze lakini na wakubwa huko nje nao ni lazima wazungumze,” alisema.
UKAWA waliteka Bunge
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Alli Idd, wamewataka wajumbe wa UKAWA wabatilishe uamuzi wa kususia vikao vya Bunge Maalumu.
Kauli hizo walizitoa jana walipokuwa wakichangia sura ya kwanza na ya sita za rasimu ya Katiba, ambapo walisema Katiba inayotungwa ni ya Watanzania wote, hivyo ni vema UKAWA wakarejea bungeni.
Balozi Iddi alisema taifa limetumia fedha nyingi kugharimia ujenzi wa Bunge Maalumu pamoja na kuwagharimia posho wajumbe wake ambapo mpaka jana lilitumia zaidi ya sh bilioni 20, hivyo si busara kwa UKAWA kususia vikao.
Alisema UKAWA ni sehemu muhimu katika utungaji wa Katiba na wajumbe wake wametumwa na wananchi ambao wanataka matatizo yao yawekewe utaratibu wa kushughulikiwa kwenye Katiba.
Alisema kutokana na umuhimu wa kutunga Katiba, Rais Jakaya Kikwete, amekubali kuliongezea muda wa siku 60 zaidi Bunge hilo ambalo jana limeahirishwa hadi Agosti 5, mwaka huu.
Alisema kuongezewa siku huko kumetokana na kutokamilisha kazi yake kwa siku 70 zilizopangwa awali ambazo zimemalizika jana hivyo UKAWA wanapaswa kutambua unyeti wa vikao vya bunge na umuhimu wao.
“Pamoja na serikali kutumia fedha nyingi kutengeneza ukumbi na kulipana posho UKAWA wameamua kususia vikao vya Bunge. Nawasihi warudi tuendelee na kazi hii tuliyopewa na wananchi. Katiba haitungwi barabarani au kwenye mikutano ya hadhara bali bungeni.
“Nawasihi warejee bungeni tuifanye kazi hii tuliyotumwa na wananchi, tumetumia fedha nyingi na tutaendelea kutumia, kila mmoja wetu analipwa sh 300,000 kwa siku na serikali inatumia sh milioni 188 kwa siku kulipa posho.”
Naye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema anaamini katika umoja, hivyo kukosekana kwa wajumbe wa UKAWA ndani ya Bunge kumemsikitisha lakini ataendeleza jitihada za mazungumzo nao.
Pinda ametoa rai hiyo wakati ni takriban wiki moja imepita tangu alipokaririwa akitamba kuwa wanawafuata UKAWA huko huko kwa wananchi kwenda kusema ukweli.
Pinda aliwasihi wajumbe wa UKAWA warejee bungeni huku akiwasihi wajumbe wengine wajiepushe na lugha za kejeli na vijembe ambazo alidai zimechangia mijadala kuwa katika mazingira magumu.
‘Mimi kila siku huwa nasema kuwa yaliyopita si ndwele…tugange yajayo, naomba wenzetu UKAWA warejee bungeni, Katiba mpya inahitaji ushirikiano wetu sote,” alisema.
Pinda pia alisema Tume ya Jaji Warioba imefanya kazi nzuri kwa kuwa yapo mambo mengi ambayo hayamo kwenye Katiba ya sasa lakini yameorodhoshwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Alibainisha kuwa anapingana na rasimu hiyo katika eneo moja la muundo wa serikali tatu kwa kuwa anaamini ni mzigo mkubwa kwa taifa na litachangia kuvunja muungano.
Alisema kuwa wanaosema kuwa kutofuata mapendekezo ya tume ya Warioba kwa kuwa imetumia fedha nyingi, wanakosea kwani wajumbe wa Bunge Maalumu wamepewa fursa ya kuondoa, kuboresha na kuingiza mawazo wanayoona yanafaa kuwemo kwenye Katiba mpya.
Naye Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alisema kiti chake kiliamua kuwaacha wajumbe wajadili kwa uhuru zaidi na wananchi waamue kipi kinafaa.
‘Huko mitaani tunalaumiwa kwa kuwaachia wajumbe, sisi tulifanya hivyo pasipo kutumia nguvu, kanuni au askari ili wananchi wajue tabia za wajumbe wao na kuamua, tungebanana sana najua lazima tungepigana na kutoana ngeu,” alisema.

Friday, April 18, 2014

JE NI KWELI PASAKA NI SIKUKUU YA KUFUFUKA KWA YESU?



JE, NI KWELI PASAKA NI SIKUKUUYA  KUFUFUKA KWA YESU?
     Adhuhuri moja wakati nikiwa nyumbani alikuja jamaa yangu mmoja ambaye aliniletea bakuli maalum la kuhifadhia chakula. Ndani ya bakuli lile kulikuwa na wali na nyama ya kuku ambavyo kwa hakika vilinitamanisha sana hasa ukizingatia nilikuwa na njaa kali. Nikaona ule ndiyo wakati haswaa wa kujifaidia kile nilicholetewa.

      Baada ya kuutwanga wali ule ndipo nilipopatwa na shauku ya kujua Yule jamaa yangu alipata wapi ujuzi wa kupika wali mtamu namna ile na kumtayarisha kitaalamu, kuku yule wa kienyeji. Ndipo jamaa yangu aliponiambia kuwa chakula kile amekipika maalum kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya kufufuliwa kwa Yesu Kristo maarufu kwa jina la Pasaka.

       Kwa miaka mingi nimekuwa nikisikia kuhusu siku hiyo na ndipo baada ya kuambiwa vile na jamaa yangu, nilipoamua kuandika makala haya ili kuuelezea umma juu ya historia ya sikukuu hiyo na mwanzilishi wake na lengo la kuwepo kwake.

Historia ya pasaka
    Pasaka ni sikukuu iliyoanza kwa nabii Mussa, kumbuka kuwa wana wa Israel walikuwa utumwani nchini Misri chini ya utawala wa mfalme Firauni(Farao) takribani miaka 400 walikuwa wanateswa na mfalme Farao.

    Baada ya mateso ya muda mrefu mungu akamtoa Mussa na kumfanya kwa Nabii na akaamrishwa kwenda kupambanana na Farao ili awakomboe wana wa Israel na wawe huru.Ndipo Mussa akaenda kwa firauni na akafanikiwa kumshinda Farao.

     Baada ya Mussa kumshinda farao  akaondoka na wana wa Israel (wayahudi) akavuka nao katika bahari ya Shamu,Firauni naye alipojaribu kuvuka pamoja na jeshi lake aliangamizwa baharini.

      Baada ya mussa kuvuka salama na wana wa Israel mungu akawapa amri ya kufurahia kutoka utumwani na ndipo sikuku hiyo ya pasaka ilipoanzia hapo rejea katika kitabu cha kumbukumbu la torati 16:1-6)

“1 Utunzwe mwezi wa Abibu ukamfanyie pasaka Bwana mungu wako kwa kuwa ilikuwa mwezi wa Abibu alipokutoa misri usiku Bwana Mungu wako, 2 Nawe umchinjie pasaka Bwana Mungu wako katika kundi la kondoo na la ng’ombe mahali atakapochagua bwana apakalishe jina lake,3 Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu ,siku saba unakula naye mikate isiyotiwa chachu nayo ni mikate ya mateso kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka ili upate kukumbuka siku iliyotoka nchi ya Misri siku zote za maisha yako, 4 Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni kisilale chochote usiku kucha hata asubuhi,5 Usimchinjie pasaka ndani ya malango yako yote akupayo Bwana Mungu wako ,6 Ila mahali atakapochagua Bwana mungu wako apakalishe jina lake ndipo mtakapomchinjia pasaka jioni katika machweo ya jua kwa wakatika kama uliotoka misri”

    Baada ya kuangalia maandiko kutoka katika kitabu cha kumbukumbu la torati sasa tuangalie tena katika kitabu cha pili cha Nabii Musa kiitwacho “KUTOKA”

    Katika kitabu cha kutoka pia tunaona kuwa asili ya sikukuu ya pasaka ilianza kwa Nabii Mussa baada ya kutoka misri na wana wa Israel rejea Kutoka 12:42-51

“42 Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana kwasababu ya kawatoka katika nchi ya Misri ,huu ndio usiku wa bwana ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israel wote katika vizazi vyao, 43 Bwana akawaambia Mussa na Haruni Amri ya pasaka ni hii, mtu mgeni asimle 44 Lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha,ukiisha kutahiri ndipo hapo atamla pasaka.45 Akaaye kwenu hali ya ugeni na mtumishi aliyeajiliwa wasimle pasaka, 45 Akaaye kwenu hali ya ugeni na mtumishi aliyeajiliwa wasimle pasaka, 46 Na aliwe ndani ya nyumba moja ,usiichukue nje ya nyumba nyama yake yoyote wala msifunje mfupa wake uwao wote. 47 Na wafanye jambo hili mkutano wa Israel wote. 48 Na mgeni atakapoketi pamoja nawe na kupenda kumfanyia Bwana pasaka waume wake wote na watahiriwe ndipo hapo akaribie na kufanya pasaka ,naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi lakini mtu yeyote asiyetahiriwa asimle. 49 Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini. 50 Ndivyo walivyofanya wana wa Israel wote kama Bwana alivyowaagiza Mussa na haruni ndivyo walivyofanya. 51 Ilikuwa siku ile ile moja,Bwana akawatoa wana wa Israel katika nchi ya Misri kwa majeshi yao”(KUTOKA 12:42-51)

    Kwa maelekezo hayo hapo juu kutoka katika kitabu cha tano cha Mussa kiitwacho “KUMBUKUMBU LA TORATI” na kitabu cha pili cha Mussa kiitwacho “KUTOKA” moja kwa moja tunaona kuwa pasaka ni sikukuu iliyoanza wakati wa Nabii Mussa baada ya kuamriwa na Mungu wake kusheherekea pasaka pamoja na wana wa Israel kwa kuchinja Kondoo na Ng’ombe baada ya Mussa kufanikiwa kuwatoa wana wa Israel kutoka katika mikono ya mateso ya mfalme Firauni(Farao),Hivyo kwa maneno hayo moja kwa moja tunaona kuwa sikukuu ya pasaka si  kufufuka bwana Yesu kama baadhi ya wakristo wanavyodai

    Jambo la kushangaza na kustaajabisha ni kuona baadhi ya watu hususani jamii ya Wakristo wakidai kuwa pasaka ni sikukuu ya kufufuka kwa Yesu wakati kwa mujibu wa vitabu vyao wanavyoviamini na kuvitumia kila siku vinakanusha suala la pasaka kuwa ni sikukuu ya kufufuka Bwana yesu.

     Baada ya kuona maandiko hayo hebu tuangalie je kweli bwana yesu alikufa na kufufua na je wanaosheherekea pasaka kuwa ni sikukuu ya kufufuka yesu wako sahihi?

LUKA 2:41-45  “Basi wazee wake huenda yerusalemu kila mwaka wakati wa sikuku ya pasaka.Na alipopata umri wa miaka kumi na miwili walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuuu.Na walipokwisha kutimiza siku wakati wa kurudi kwao,Yule mtoto yesu alibaki nyuma huko yerusalemu na wazee wake walikuwa hawana habari.Na wakadhani ya kuwa yumo katika msafara wakaenenda mwendo wa kutwa wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao.Na walipomkosa wakarejea Yerusalemu huku wakimtafuta”

     Kwa maelezo hayo hapo juu tunaona kuwa hata yeye mwenyewe yesu alikula sikukuu ya pasaka wakati akiwa mdogo na umri wake ulikuwa ni miaka kumi na miwili akiwa na wazee wake ambao walikuwa wakienda Yerusalemu kama ilivyokuwa desturi yao.

     Swali la kujiuliza hapo je ni nani alikufa na kufufuka ikiwa Yesu mwenyewe alikula pasaka akiwa na umri wa miaka kumi na miwili je kusema kuwa sikukuu ya pasaka ni kufufuka kwa Yesu je huyo ni yesu gani?
    Ukweli ni kwamba kusheherekea sikukuu ya pasaka ni kupoteza mwelekeo kwani sikukuu hiyo ya pasaka ni sikukuu ya wayahudi.

    Ushahidi unaothibitisha kuwa pasaka ni sikukuu ya wayahudi ni YOHANA 6:4 “Na pasaka sikuku ya wayahudi ilikuwa karibu”

     Nihitimishe makala hii fupi ya UKWELI KUHUSU PASAKA kwa maneno ya kitabu kitukifi cha QUR’AN pale ambapo ALLAH S W aliposema katika sura ya 4:157-158

    “Na kwaajili ya kusema kwao sisi tumemuua Masihi Isa mwana wa Mariamu mtume wa mungu hali hawakumuua wala hawakumsulubu bali walibabaishiwa (mtu mwingine wakamdhani Nabii Isa) Na kwa hakika wale waliokhitalifiana katika hiyo(ya kumuua Isa)wako katika shaka nalo (jambo hilo la kusema kauawa)wao hawana yakini juu ya jambo hili isipokuwa wanafuata dhana tu.Na kwa yakini hawakumwua. Bali Mwenyezimungu alimnyanyua kwake na Mwenyezimungu ni mwenye nguvu na mwenye hikima.

      Kwa aya hiyo ndipo ambapo tunaona kuwa Nabii ISSA(a.s) au YESU hakufa wala hakusulubiwa ila walifananishiwa tu hao mayahudi waliotaka kumsulubu na kumuua bwana Yesu.

    Hivyo kusheherekea sikukuu ya pasaka ni kufuata mila za wayahudi na watu wasio na dini.

Kwa kifupi huo ndio ukweli kuhusu pasaka na historia yake ambapo tumeona kuwa pasaka ilianza kwa Nabii Mussa pale alipoambia na Mungu wake aende kwa Firauni(Farao) akawaokoe wana wa Israel kutokana na mateso waliyokuwa wanayapata kutoka kwa mfalme Firauni(Farao) lakini pia tumeona kuwa pasaka ni sikukuu ya iliyokuwa inasheherekewa na mayahudi wa kipindi hicho.

     Nakuacha na swali hili; Kusema kuwa pasaka ni siku ya kufufuka kwa Yesu je ni Yesu gani huyo aliyekufa na kufufuka wakati yeye mwenyewe amekula pasaka?

Makala hii imeandaliwa na
Adinani  H chorobi 0753-733217