STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi, anajiamini kupita kiasi na akawaambia mashabiki wa Yanga, waendelee kumzomea hivyo hivyo, kwani kelele zao zinaingilia kulia na kutokea kushoto na mwisho wa siku watampenda tu.
Okwi raia wa Uganda, ana utata na Yanga ambayo ana mkataba nayo lakini ameukana mkataba huo na kusaini Simba kutokana na sababu mbalimbali ambapo juzi Jumamosi aliichezea kwa mara kwanza klabu hiyo ya Msimbazi kwenye mechi ya kirafiki waliyoifunga Gor Mahia mabao 3-0.
Katika mchezo huo, Okwi alipata tabu kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao kila alipogusa mpira walikuwa wanamzomea jambo ambalo limeelezwa na wadau wengi wa soka kuwa litamfanya ashindwe kucheza mpira.
Lakini alipozungumza na Mwanaspoti, Okwi alisema: “Hiyo zomea zomea yao, watazomea sana lakini kamwe hawataweza kunifanya nishindwe kucheza mpira.
“Mimi ni mchezaji mkubwa, najielewa, hicho wanachikifanya ni kujisumbua tu, nitacheza na kupiga mabao kama kawaida na wakibisha wataona.”
Beki wa Yanga, Mbuyu Twite, ambaye awali alikuwa kwenye rada ya Simba aliwahi kukumbana na zomea zomea ya Simba waliokuwa wakimkejeli kwa kumuita mwizi kwa madai kwamba alichukua fedha zao za usajili akaingia mitini.
Tofauti na Twite ambaye alikuwa akiwajibu kwa ishara mbalimbali akiwa uwanjani, Okwi alifanya jambo dogo sana ambapo kila alipokuwa akiitwa jina hilo alikuwa akiwanyooshea dole mashabiki wa Simba ambao walijibu kwa kumshangilia kwa nguvu jambo lililoleta raha.
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Phiri amefurahishwa na uwezo ulioonyeshwa na Okwi lakini akampa jukumu moja kubwa ambalo anatakiwa kulikamilisha mapema ili aweze kutisha.
“Namjua Emmanuel (Okwi) ni kijana mzuri, lakini amenifurahisha sana na uwezo aliouonyesha amecheza vizuri kwa kiasi chake lakini bado ananafasi ya kufanya vizuri zaidi,” alisema Phiri.
“Bado hayupo sawa sana, lakini hilo lipo mikononi mwake. Kuhakikisha anajituma zaidi mazoezini, anaweza kuwa sawa zaidi endapo atajituma kufanya mazoezi ya nguvu.
“Kama akifanikiwa hilo atarudi katika uwezo na kuweza kuisaidia Simba.”
No comments:
Post a Comment