Monday, September 8, 2014

Di Maria aibua zengwe Madrid

MADRID, HISPANIA
WINGA, Angel Di Maria ameibua jipya kuhusu klabu yake ya zamani ya Real Madrid.
Staa huyo mpya wa Manchester United raia wa Argentina amefichua kwamba Real Madrid ilimtumia barua siku ya fainali ya Kombe la Dunia nchini Brazil ikimtaka asicheze mechi hiyo.
Alibainisha kwamba amekuwa hana uhusiano mzuri na rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, mtu ambaye hasa ndiye anayepaswa kubeba lawama kutokana na kuondoka kwake  katika Uwanja wa Bernabeu katika dirisha la usajili lililomalizika karibuni.
“Nilipata barua kutoka Real Madrid, ilinifikia saa 5 asubuhi ilikuwa ni siku ya fainali ya Kombe la Dunia na ilielezea kuwa nisicheze mechi hiyo,” alisema winga huyo.
“Mechi ilikuwa saa 10 jioni na nilikuwa najiandaa kujiweka vizuri kwa sababu nilikuwa nimeumia. Mawazo yangu yalikuwa ni kucheza mechi ya fainali, ingawa nilifahamu hilo lilikuwa na asilimia 90 tu.
“Mara nikapata barua hiyo na niliichapa.  Sikujali kitu kwa chochote ambacho kingetokea. Nilipata mawazo mengi  asubuhi ile na kusema nini hiki kimetokea kwenye maisha yangu. Sikumwambia yeyote pale klabuni kwa kuwa sikutaka maoni ya mtu mwingine bali nilitaka kutafakati mwenywe.”
Di Maria aliongeza: “Nilikuwa na uhusiano safi tu na wachezaji wenzangu. Sikuwa vizuri na Florentino Perez. Niliposaini mkataba wangu klabuni hakuwapo.”

No comments: