Monday, September 8, 2014

MBUNGE MGIMWA APANIA KUKAMILISHA UJENZI WA MAABARA YA SAYANSI KIDAMALI SEKONDARI

KATIKA  kile  kinachoonyesha ni  kuunga mkono maagizo ya  Rais Dr Jakaya  Kikwete  katika  uanzishaji  ujenzi  wa  maabara za  sayansi  katika  shule  za sekondari  nchini ,mbunge wa  jimbo la Kalenga  Godfrey Mgimwa ameahidi  kuchangia   kushirikiana na  shule ya sekondari Kidamali na   shule  nyingine  jimboni  humo ambazo  zitaanzisha ujenzi wa maabara.
 
Akizungumza katika harambee ya  kuchangia  ujenzi  wa maabara  katika  shule ya Sekondari Kidamali ,mbunge Mgimwa  alisema  kuwa  mbali ya kuupongeza uongozi wa  shule  hiyo kwa  kuja na  wazo la  kujenga maabara  kwa upande wake kama mbunge atakuwa  bega kwa bega na  wananchi wake  katika  ujenzi wa maabara katika  shule za  sekondari kama  ni  sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dr Kikwete .
 
” Kazi  mnayoifanya ni kubwa na inapaswa  kuungwa mkono na kila mdau  wa maendeleo katika  jimbo la Kalenga  kwani  kati ya  maagizo ya  Rais mheshimiwa Dr  Jakaya mrisho  Kikwete ni Halmashauri za  wilaya na mikoa  kuanzisha  ujenzi wa maabara za  sayansi  katika  shule zake  za  sekondari …..hivyo  mimi kama  mbunge  wenu  nimefurahishwa  sana na jitihada  hizi” alisema mbunge Mgimwa 
 
Kuwa  iwapo  shule  zote za  sekondari katika  jimbo la Kalenga zikaanza  mkakati wa ujenzi  wa  maabara  za  sayansi  ari ya  wanafunzi  kupenda masomo  ya  sayansi  itakuwa  juu zaidi na  kuwa kazi yake kama  mbunge ni  kuona anaendelea   kuunga mkono shule  zote zitakazoanzisha  ujenzi wa maabara  hizo.
 
Alisema  kuwa mbali ya  kuwa  elimu katika  jimbo lake la  Kalenga  inaendelea  vema ila bado  kuna haja ya  shule  zote za  sekondari katika jimbo  hilo  kuwa na maabara ya masomo ya  Sayansi .
 
” Maendeleo  ambayo mmeanzisha  ni makubwa  sana na  mimi kama  mbunge  najivunia  kuona  shule  inaanzisha  mpango  huu na  zaidi nampongeza  sana mkuu wa  shule ambaye amekuja na  wazo   hilo na mdau mkubwa wa maendeleo kata ya   Nzihi mkulima  George  Filiakosi aliyejitolea  kuandaa  chakula  ili  watu  wafike  kuchangia ujenzi  huo …..mimi kama  mbunge nitawachangia milioni  1  pamoja na  kujitolea  bati  zote  za  kuezekea  jengo  hilo  pindi  litakapo malizika “
 
Mbali ya  mbunge  huyo kujitolea  kwa  upande wake  mkuu  wa  shule  hiyo  Sixtus Kanyama  aliwapongeza  wadau  mbali mbali hasa   George Filiakosi kwa  kuendelea  kujitoa  kwa ajili ya  ujenzi wa maabara  hiyo huku akiwaomba  wadau  wengine  waliopo nje ya  jimbo la Kalenga  kuunga mkono  jitihada za mbunge  wao kwa kujitokeza kuchangia ujenzi huo .
 
Mkuu  huyo wa  shule alisema  kuwa  ili kukamilisha  ujenzi wa maabara   hiyo ya kisasa  jumla ya zaidi ya Tsh  milioni 200 zinahitajika na  kuwa  kwa  wale ambao  watakuwa tayari  kuunga mkono  ujenzi huo  wanaweza  kuchangia kwa kupitia  akaundi  ya shule  Kidamali sec School namba 6051100149 benki ya NMB ama kwa jina ya M- Pesa kwa namba  ya  mkuu wa shule  0752 507519
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya  wilaya ya  Iringa na  diwani  wa kata ya Nzihi Stephen Mhapa alisema  kuwa   wapo  baadhi ya  wananchi  wa kata  hiyo ambao  mbali ya  kualikwa  kufika kuchangia ujenzi huo  ila hawakuweza  kufika jambo ambalo alisema halipaswi kuendelea  kwani  kufanya  hizo ni  kurudisha  nyuma maendeleo ya ujenzi huo na maendeleo mengine kwa ujumla  wake.

No comments: