MBUNGE wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala, amejitosa rasmi katika mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwaka 2015.
Tangazo hilo la Kigwangala, linaongeza idadi ya wanaowania kiti hicho baada ya January Makamba, Bernard Membe, Edward Lowassa,William Ngeleja, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza nia na baadhi yao kutajwa kuwa na nia ya kufanya hivyo mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari, wazazi wake, familia yake na makada wa CCM, akiwemo William Malecela (Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani John Malecela), Dk. Kigwangala alitumia muda mrefu kufafanua hotuba yake iliyokuwa na kurasa sita akielekeza kuwa, watanzania wanapaswa kubadili mipangilio ya kipaumbele na kusimiamia mambo wanayoyasema ili kujikwamua kiuchumi.
Kigwangala aliwaambia waandishi kuwa, anatangaza rasmi sasa, kuwa anatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Alisema amefikia uamuzi huo bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, isipokuwa utashi utayari wake.
Bila kuwataja majina, Kigwangala aliponda njia wanazotumia wengine akisema kuwa yeye hasubiri kuoteshwa, kushauriwa au kuombwa kama wanavyofanya wagombea wengine kupitia CCM. Alisema baadhi ya wanasiasa wa CCM, wamekuwa waoga kujitosa au kutangaza nia zao bali husema kuwa wanasubiri kuoteshwa, au wengine wameombwa na watu wengine.
Alibainisha kuwa, anatangaza nia ya kugombea urais mapema ili kuwapa fursa watanzania wampime na kumtazama mwenendo na uwezo wake, akiamini kuwa ataungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yake, si kwa jinsi yake, si kwa umri wake au kwa daraja lake kijamii, dini, ama kabila lake, bali kwa sifa na uwezo wake kama mtanzania.
Kigwangala alitumia msemo wa kilatini kusema kuwa yeye ni baina ya wengi, mmoja! (E Pluribus unum), hivyo hawezi kuwa salama ikiwa wengine wanateseka.
Bila kutaja wazi kuwa anakosoa utendaji wa serikali ya Kikwete, Kigawangala alitoa mifano mbalimbali ikiwemo kitisho cha njaa, kucheleweshwa hukumu za mahakamani, shida za mzee mmoja wa Pemba aliyefiwa na mtoto wake, au kasoro za operesheni za wamachinga na mamantilie jijini Dar es Salaam.
“Kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu, hata kama siyo familia yangu. Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu,” alisema.
Aliongeza kuwa Mama Ntilie wa Sokoni Kariakoo, akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula chake na mgambo wa Jiji la Dar es Salaam inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye si mama yangu,” alisema.
No comments:
Post a Comment