Monday, September 8, 2014

JUMUIYA YA ZAKA NA SADAKA ZNZ (JUZASA) YAFANYA MKUTANO WA MAENDELEO YA JUMUIYA HIYO

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Zaka na Sadaka Zanzibar (JUZASA) Shekh Said Suleiman Masoud Mwenyekoti Jeusi akitoa nasaha zake kwa Wanachama na Waalikwa katika Mkutano wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ukumbi wa Shamtimba Kiembesamaki Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Zaka na Sadaka Zanzibar (JUZASA) Shekh Said Suleiman Masoud Mwenyekoti Jeusi akitoa nasaha zake kwa Wanachama na Waalikwa katika Mkutano wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ukumbi wa Shamtimba Kiembesamaki Zanzibar.

ZANZIBAR

Kukosekana kwa Utaratibu nzuri wa Utoaji na Usambazaji wa Zaka ni moja ya matatizo yanayopelekea Zanzibar kuendelea kuwa na Watu wanaoishi katika mazingira magumu na Umasikini uliopindukia.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Zaka na Sadaka Zanzibar (JUZASA) Shekh Said Suleiman Masoud ameyasema hayo alipokuwa akitoa nasaha katika Mkutano wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ukumbi wa Shamtimba Kiembesamaki Zanzibar.
Amesema Zanzibar kuna watu Wenye nafasi nzuri kiuchumi lakini  wanashindwa kutoa Zaka katika utaratibu Unaofaa na hivyo kushindwa kuwafikia Walengwa wenye Mahitaji.
Amesema Watu hao wenye uwezo wangekuwa wanatoa Zaka na kusambazwa katika utaratibu unaofaa, Zanzibar ingekuwa haina Watu Masikini kutokana na Zaka hizo kuwakomboa katika kiuchumi.
Shekh Said amesema wameamua kuanzisha Jumuiya ya (JUZASA) ili kurahisisha Upatikanaji na Usambazaji wa Zaka baada ya kukosekana jambo hili kwa miaka mingi.
Ameongeza kuwa kwa muda mrefu Zanzibar kumeundwa Taasisi nyingi za Serikali na za kibinafsi kwa ajili ya kumkomboa Mwananchi na Umasikini lakini malengo yanashindwa kutimia kutokana na kukosekana Elimu ya Utoaji wa Zaka.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya JUZASA Omar Abubakar ameelezea Malengo ya Zaka kuwa ni pamoja na Kuitakasa Mali ya Mtoaji na kumkomboa Muislamu kutokana na Janga la Njaa.
Ametoa wito kwa Waisalmu kujitokeza kuwaunga Mkono sambamba na kupeleka Zaka zao katika Jumuiya yao ili Waziwasilishe kwa walengwa wanaofaa kupewa Zaka katika jamii.
Katika Mkutano huo Jumuiya hiyo imefanya Uchaguzi ambapo Mwenyekiti wake na Katibu wake wamechaguliwa tena kuiongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Jumuiya hiyo iliyopata Usajili mwaka 2011 inapokea na kusambaza Zaka kwa walengwa,ambapo malengo yake makuu ni kutekeleza vyema Suala la Zaka ili kuweza kuwasaidia Wanajimii wanaoishi katika mazingira magumu na umasikini uliokithiri.
 

MBUNGE MGIMWA APANIA KUKAMILISHA UJENZI WA MAABARA YA SAYANSI KIDAMALI SEKONDARI

KATIKA  kile  kinachoonyesha ni  kuunga mkono maagizo ya  Rais Dr Jakaya  Kikwete  katika  uanzishaji  ujenzi  wa  maabara za  sayansi  katika  shule  za sekondari  nchini ,mbunge wa  jimbo la Kalenga  Godfrey Mgimwa ameahidi  kuchangia   kushirikiana na  shule ya sekondari Kidamali na   shule  nyingine  jimboni  humo ambazo  zitaanzisha ujenzi wa maabara.
 
Akizungumza katika harambee ya  kuchangia  ujenzi  wa maabara  katika  shule ya Sekondari Kidamali ,mbunge Mgimwa  alisema  kuwa  mbali ya kuupongeza uongozi wa  shule  hiyo kwa  kuja na  wazo la  kujenga maabara  kwa upande wake kama mbunge atakuwa  bega kwa bega na  wananchi wake  katika  ujenzi wa maabara katika  shule za  sekondari kama  ni  sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dr Kikwete .
 
” Kazi  mnayoifanya ni kubwa na inapaswa  kuungwa mkono na kila mdau  wa maendeleo katika  jimbo la Kalenga  kwani  kati ya  maagizo ya  Rais mheshimiwa Dr  Jakaya mrisho  Kikwete ni Halmashauri za  wilaya na mikoa  kuanzisha  ujenzi wa maabara za  sayansi  katika  shule zake  za  sekondari …..hivyo  mimi kama  mbunge  wenu  nimefurahishwa  sana na jitihada  hizi” alisema mbunge Mgimwa 
 
Kuwa  iwapo  shule  zote za  sekondari katika  jimbo la Kalenga zikaanza  mkakati wa ujenzi  wa  maabara  za  sayansi  ari ya  wanafunzi  kupenda masomo  ya  sayansi  itakuwa  juu zaidi na  kuwa kazi yake kama  mbunge ni  kuona anaendelea   kuunga mkono shule  zote zitakazoanzisha  ujenzi wa maabara  hizo.
 
Alisema  kuwa mbali ya  kuwa  elimu katika  jimbo lake la  Kalenga  inaendelea  vema ila bado  kuna haja ya  shule  zote za  sekondari katika jimbo  hilo  kuwa na maabara ya masomo ya  Sayansi .
 
” Maendeleo  ambayo mmeanzisha  ni makubwa  sana na  mimi kama  mbunge  najivunia  kuona  shule  inaanzisha  mpango  huu na  zaidi nampongeza  sana mkuu wa  shule ambaye amekuja na  wazo   hilo na mdau mkubwa wa maendeleo kata ya   Nzihi mkulima  George  Filiakosi aliyejitolea  kuandaa  chakula  ili  watu  wafike  kuchangia ujenzi  huo …..mimi kama  mbunge nitawachangia milioni  1  pamoja na  kujitolea  bati  zote  za  kuezekea  jengo  hilo  pindi  litakapo malizika “
 
Mbali ya  mbunge  huyo kujitolea  kwa  upande wake  mkuu  wa  shule  hiyo  Sixtus Kanyama  aliwapongeza  wadau  mbali mbali hasa   George Filiakosi kwa  kuendelea  kujitoa  kwa ajili ya  ujenzi wa maabara  hiyo huku akiwaomba  wadau  wengine  waliopo nje ya  jimbo la Kalenga  kuunga mkono  jitihada za mbunge  wao kwa kujitokeza kuchangia ujenzi huo .
 
Mkuu  huyo wa  shule alisema  kuwa  ili kukamilisha  ujenzi wa maabara   hiyo ya kisasa  jumla ya zaidi ya Tsh  milioni 200 zinahitajika na  kuwa  kwa  wale ambao  watakuwa tayari  kuunga mkono  ujenzi huo  wanaweza  kuchangia kwa kupitia  akaundi  ya shule  Kidamali sec School namba 6051100149 benki ya NMB ama kwa jina ya M- Pesa kwa namba  ya  mkuu wa shule  0752 507519
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya  wilaya ya  Iringa na  diwani  wa kata ya Nzihi Stephen Mhapa alisema  kuwa   wapo  baadhi ya  wananchi  wa kata  hiyo ambao  mbali ya  kualikwa  kufika kuchangia ujenzi huo  ila hawakuweza  kufika jambo ambalo alisema halipaswi kuendelea  kwani  kufanya  hizo ni  kurudisha  nyuma maendeleo ya ujenzi huo na maendeleo mengine kwa ujumla  wake.

Kigwangala ajitosa rasmi urais 2015

Awaponda wanaosubiri kuoteshwa .Mtoto wa Malecela amuunga mkono
 MBUNGE wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala, amejitosa rasmi katika mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwaka 2015.
Tangazo hilo la Kigwangala, linaongeza idadi ya wanaowania kiti hicho baada ya January Makamba, Bernard Membe, Edward Lowassa,William Ngeleja, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza nia na baadhi yao kutajwa kuwa na nia ya kufanya hivyo mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari, wazazi wake, familia yake na makada wa CCM, akiwemo William Malecela (Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani John Malecela), Dk. Kigwangala alitumia muda mrefu kufafanua hotuba yake iliyokuwa na kurasa sita akielekeza kuwa, watanzania wanapaswa kubadili mipangilio ya kipaumbele na kusimiamia mambo wanayoyasema ili kujikwamua kiuchumi.
Kigwangala aliwaambia waandishi kuwa, anatangaza rasmi sasa, kuwa anatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Alisema amefikia uamuzi huo bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, isipokuwa utashi utayari wake.
Bila kuwataja majina, Kigwangala aliponda njia wanazotumia wengine akisema kuwa yeye hasubiri kuoteshwa, kushauriwa au kuombwa kama wanavyofanya wagombea wengine kupitia CCM. Alisema baadhi ya wanasiasa wa CCM, wamekuwa waoga kujitosa au kutangaza nia zao bali husema kuwa wanasubiri kuoteshwa, au wengine wameombwa na watu wengine.
Alibainisha kuwa, anatangaza nia ya kugombea urais mapema ili kuwapa fursa watanzania wampime na kumtazama mwenendo na uwezo wake, akiamini kuwa ataungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yake, si kwa jinsi yake, si kwa umri wake au kwa daraja lake kijamii, dini, ama kabila lake, bali kwa sifa na uwezo wake kama mtanzania.
Kigwangala alitumia msemo wa kilatini kusema kuwa yeye ni  baina ya wengi, mmoja! (E Pluribus unum), hivyo hawezi kuwa salama ikiwa wengine wanateseka.
Bila kutaja wazi kuwa anakosoa utendaji wa serikali ya Kikwete, Kigawangala alitoa mifano mbalimbali ikiwemo kitisho cha njaa, kucheleweshwa hukumu za mahakamani, shida za mzee mmoja wa Pemba aliyefiwa na mtoto wake, au kasoro za operesheni za wamachinga na mamantilie jijini Dar es Salaam.
Kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu, hata kama siyo familia yangu. Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu,” alisema.
Aliongeza kuwa Mama Ntilie wa Sokoni Kariakoo, akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyanganywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula chake na mgambo wa Jiji la Dar es Salaam inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye si mama yangu,” alisema.

Waislamu watibuka kuzikwa Mahakama ya Kadhi

WAKATI Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, akitarajia kutoa msimamo wake leo kuhusu hatua ya Bunge Maalumu la Katiba kuzika suala la Mahakama ya Kadhi, Waislamu kupitia Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu (Hayat), wameapa kuipigia kura ya hapana Rasimu ya Katiba pindi itakapofika kwa wananchi.
Akizungumza siku ya Jumapili, Naibu Katibu Mkuu wa Hayat na Mwenyekiti wa Jukwaa la Waislamu la Kuratibu maoni ya Katiba, Sheikh Mohamed Issa, alisema kama Bunge hilo litarudisha Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba kupigiwa kura na wananchi ikiwa haina kipengele cha Mahakama ya Kadhi, wataipigia rasimu hiyo kura ya hapana.
Alisema kitendo cha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walio wengi kutogusia suala la Mahakama ya Kadhi ni mwendelezo wa kuwanyima Waislamu haki yao ya muda mrefu.
Lakini hili tumeliona toka katika Tume ya Jaji Warioba walipotuambia kwamba suala hili lisiingizwe katika maoni ya Rasimu ya Katiba hadi nchi mbili washirika kwa maana ya Zanzibar na Tanganyika zitakapokuwa na Katiba zao na waliingize suala hili katika katiba hizo,” alisema Sheikh Issa.
Alisema walihoji jambo hilo, lakini majibu yaliyotoka waliona hayakuwa na nia njema katika kuleta Kadhi katika nchi hii.
Tulipata majibu ambayo yalionyesha kabisa mwelekeo mzima juu ya Kadhi ni negative, kwahiyo toka ilipoanzia na hapa ilipofikia hatushangai,” alisema Sheikh Issa
Sheikh Issa alisema kwa sasa wataendelea kuhamasishana kwa nia ya kupiga kura ya hapana katika rasimu itakayorudishwa kwa wananchi
Mimi sielewi kwanini katika nchi hii tunaogopa Kadhi, majirani zetu wa Kenya wameingiza Kadhi kwenye Katiba yao, jambo hili tumeliomba siku nyingi na tuliambiwa tusubiri mchakato wa Katiba, lakini mchakato ndiyo huu na mambo ndiyo hayo yanayotokea,” alisema Sheikh Issa.
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Simba, alipotafutwa kuzungumzia kuhusu suala zima la Mahakama ya Kadhi, alisema angetoa tamko lake jana baada ya kukutana na viongozi wa Baraza la Maimamu (Ulamaa).
Nimekutana na Ulamaa, katika makubaliano yetu tunasubiri kukutana na wawakilishi wetu wa bungeni watupe taarifa rasmi ili tunapotoa tamko tusije tukapishana wakatulaumu kwamba hatujawashirikisha,” alisema Mufti Simba jana wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu kikao chake na Ulamaa kilichofanyika juzi.
Wakati Mufti akisema hayo, Msemaji wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Forum), Sheikh Rajab Katimba, alisema Waislamu kudai Mahakama ya Kadhi si jambo la huruma bali ni haki yao.
Mimi nashangaa kwanini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanakataa Kadhi wakati ilikuwa moja ya jambo waliloweka katika Ilani ya chama chao, najiuliza kwanini watu hawa hawa wakati ule waone linafaa na sasa hivi waone halifai, wanataka kutuaminisha kwamba wao ni vinyonga wanabadilika badilika au vipi, lakini wafahamu kabisa kwamba jambo hili ni haki ya Waislamu na wanachofanya ni kuukataa ukweli kwa muda tu,” alisema Sheikh Katimba.
Suala la Mahakama ya Kadhi liliibua mjadala mkali katika vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hadi kuundiwa kamati ndogo iliyokuwa inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu.
Hata hivyo, juzi wakati kamati hiyo ikiwasilisha maoni yake, suala hilo lilionekana kuzimwa kwa sababu ambazo hazikuelezwa bayana.
Ilidaiwa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo waliweka misimamo ya kutozungumzia suala hilo ingawa baadhi ya wajumbe wachache wa kamati namba nne na tisa waliibua licha ya kutopata mwitikio kama ilivyokuwa katika vikao vya awali.

Di Maria aibua zengwe Madrid

MADRID, HISPANIA
WINGA, Angel Di Maria ameibua jipya kuhusu klabu yake ya zamani ya Real Madrid.
Staa huyo mpya wa Manchester United raia wa Argentina amefichua kwamba Real Madrid ilimtumia barua siku ya fainali ya Kombe la Dunia nchini Brazil ikimtaka asicheze mechi hiyo.
Alibainisha kwamba amekuwa hana uhusiano mzuri na rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, mtu ambaye hasa ndiye anayepaswa kubeba lawama kutokana na kuondoka kwake  katika Uwanja wa Bernabeu katika dirisha la usajili lililomalizika karibuni.
“Nilipata barua kutoka Real Madrid, ilinifikia saa 5 asubuhi ilikuwa ni siku ya fainali ya Kombe la Dunia na ilielezea kuwa nisicheze mechi hiyo,” alisema winga huyo.
“Mechi ilikuwa saa 10 jioni na nilikuwa najiandaa kujiweka vizuri kwa sababu nilikuwa nimeumia. Mawazo yangu yalikuwa ni kucheza mechi ya fainali, ingawa nilifahamu hilo lilikuwa na asilimia 90 tu.
“Mara nikapata barua hiyo na niliichapa.  Sikujali kitu kwa chochote ambacho kingetokea. Nilipata mawazo mengi  asubuhi ile na kusema nini hiki kimetokea kwenye maisha yangu. Sikumwambia yeyote pale klabuni kwa kuwa sikutaka maoni ya mtu mwingine bali nilitaka kutafakati mwenywe.”
Di Maria aliongeza: “Nilikuwa na uhusiano safi tu na wachezaji wenzangu. Sikuwa vizuri na Florentino Perez. Niliposaini mkataba wangu klabuni hakuwapo.”

Okwi ajibu makelele ya Yanga

STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi,  anajiamini kupita kiasi na akawaambia mashabiki wa Yanga, waendelee kumzomea hivyo hivyo, kwani kelele zao zinaingilia kulia na kutokea kushoto na mwisho wa siku watampenda tu.

Okwi raia wa Uganda, ana utata na Yanga ambayo ana mkataba nayo lakini ameukana mkataba huo na kusaini Simba kutokana na sababu mbalimbali ambapo juzi Jumamosi aliichezea kwa mara kwanza klabu hiyo ya Msimbazi kwenye mechi ya kirafiki waliyoifunga Gor Mahia mabao 3-0.
Katika mchezo huo, Okwi alipata tabu kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao kila alipogusa mpira walikuwa wanamzomea jambo ambalo limeelezwa na wadau wengi wa soka kuwa litamfanya ashindwe kucheza mpira.
Lakini alipozungumza na Mwanaspoti, Okwi alisema: Hiyo zomea zomea yao, watazomea sana lakini kamwe hawataweza kunifanya nishindwe kucheza mpira.
Mimi ni mchezaji mkubwa, najielewa, hicho wanachikifanya ni kujisumbua tu, nitacheza na kupiga mabao kama kawaida na wakibisha wataona.
 Beki wa Yanga, Mbuyu Twite, ambaye awali alikuwa kwenye rada ya Simba aliwahi kukumbana na zomea zomea ya Simba waliokuwa wakimkejeli kwa kumuita mwizi kwa madai kwamba alichukua fedha zao za usajili akaingia mitini.
Tofauti na Twite ambaye alikuwa akiwajibu kwa ishara mbalimbali akiwa uwanjani, Okwi alifanya jambo dogo sana ambapo kila alipokuwa akiitwa jina hilo alikuwa akiwanyooshea dole mashabiki wa Simba ambao walijibu kwa kumshangilia kwa nguvu jambo lililoleta raha.
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Phiri amefurahishwa na uwezo ulioonyeshwa na Okwi lakini akampa jukumu moja kubwa ambalo anatakiwa kulikamilisha mapema ili aweze kutisha.
Namjua Emmanuel (Okwi) ni kijana mzuri, lakini amenifurahisha sana na uwezo aliouonyesha amecheza vizuri kwa kiasi chake lakini bado ananafasi ya kufanya vizuri zaidi,” alisema Phiri.
Bado hayupo sawa sana, lakini hilo lipo mikononi mwake. Kuhakikisha anajituma zaidi mazoezini, anaweza kuwa sawa zaidi endapo atajituma kufanya mazoezi ya nguvu.
Kama akifanikiwa hilo atarudi katika uwezo na kuweza kuisaidia Simba.

DALADALA ZAGOMA KUTOA HUDUMA MANISPAA YA IRINGA

KITUO CHA MABASI MIYOMBONI KUKIWA HAKUNA DALADALA HATA MOJA BAADA YA KUGOMA

STENDI YA MASHINE TATU ABIRIA WAKISUBIRI DALADALA BAADA YA KUGOMA KUTOA HUDUMA
BAADHI YA ABIRIA WAKILAZIMIKA KUTUMIA USAFIRI WA TOYO BAADA YA DALADALA KUGOMA



MADEREVA wa daladala manispaa ya Iringa leo wameanza mgomo usio na kikomo” wakizishinikiza mamlaka zinazohusika kuwazuia madereva wa pikipiki za miguu mitatu Bajaj” kufanya biashara ya daladala. 
Hatua hiyo imeleta adha kubwa kwa watumiaji wa usafiri wa daladala japokuwa imekuwa neema kubwa kwa waendesha bodaboda, Bajaj na malori madogo aina ya Suzuki Carry. 
Wakizungumzia mgomo huo, baadhi ya wakazi wa mjini hapa wamesema kwamba umewaathiri kwa kiasi kikubwa huku wakiutupia lawama uongozi wa mamlaka ya usafiri wan chi kavu na majini (SUMATRA) mkoa wa Iringa.
Aidha mmoja wa madereva wa daladala hao ambaye hakutaja jina lake amesema kuwa tatizo hilo la mgomo ni kutokana na utaratibu mbovu wa waendesha bajaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wasafirishaji kwa kutumia pikipiki mkoa wa Iringa Bw. Joseph Mwambabe, amewatupia lawama viongozi wa Sumatra kwa kuuchochea mgomo huo
Hata hivyo Mwambabe  amesema tatizo hilo wamelifikisha katika ofisi za mkuu wa mkoa na mpaka sasa wanasubiri unatatibu utakao waongoza katika kazi zao.
 Mgomo huo umechukua zaidi ya masaa 10 kuanzia saa kumi na mbili hadi habari hii inatumwa ulikuwa bado ukiendelea Mjengwablog lilimtafuta Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Leopord Fungu ofisini kwake alikuwa katika kikao pamoja viongozi wa kamati ya usalama barabarani kwa kushirikiana na uongozi wa Sumatra mkoa wa Iringa.

`Kujiuzulu mwanasheria wa Zanzibar hakutaathiri Bunge`

Bunge Maalum la Katiba limesema kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar katika Kamati ya Uandishi wa Katiba mpya hakutaathiri upatikanaji wa katiba mpya.

Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamadi, alisema kitendo cha kujiuzulu kwa mwanasheria mkuu, Othman Masoud Othman, ni jambo la kawaida na kwamba uwakilishi wa Zanzibar ndani ya chombo hicho utakuwepo.

Alisema hajapata taarifa rasmi ya kujiuzulu kwa Othman katika kamati hiyo ambayo ipo chini ya Uenyekiti wa Mbunge wa Bariadi Mashariki, Adrew Chenge, lakini kama amefanya hivyo atakuwa ametimiza wajibu wake kisheria.

Hamad, alisema kwamba mwanasheria huyo hakuingia katika Kamati ya uandishi wa Katiba mpya kutokana na wadhifa wake, bali ni uteuzi wake ulifanywa na uongozi wa Bunge hilo kama wajumbe wengine.

Katibu huyo aliongeza kuwa uwakilishi wa Zanzibar katika kamati hiyo utakuwepo kwa sababu kuna wajumbe wengine kutoka upande huo wa Muungano wanaendelea na kazi hiyo kikamilifu.
 

BENKI KUU YATOA SARAFU YA SH.500

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kutoa toleo jipya la sarafu ya Sh. 500, inayotarajiwa kuingizwa kwenye mzunguko na kutumika rasmi kama fedha halali nchini, kuanzia mwezi ujao.

Hatua hiyo imechukuliwa na BoT kwa kuzingatia sababu mbalimbali, ikiwamo noti ya Sh. 500 iliyopo sasa kwenye mzunguko kupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi na hivyo, kuchakaa haraka.

Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BoT, Emmanuel Boaz, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana kuwa sarafu hiyo itakuwa ikitumika sambamba na noti zilizopo za Sh. 500 mpaka hapo noti hizo zitakapokwisha katika mzunguko.

“Hatua hii imezingatia kwamba, noti ya Sh. 500 ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida ya kila siku ya wananchi wengi kuliko noti nyingine yoyote. Hivyo, noti hiyo hupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi sana na kuchakaa haraka,” alisema Boaz.

Alitaja sababu nyingine iliyozingatiwa katika kutoa sarafu hiyo kuwa ni noti hizo (za Sh. 500) kukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe zinapokuwa zimefikia ukomo wake.

Sababu nyingine ni sarafu kuwa na uwezo wa kukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi (zaidi ya miaka 20) zaidi kuliko noti.

Alisema sarafu hiyo ina umbo la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5, ina rangi ya fedha na imetengezwa kwa madini aina ya chuma na “Nickel”.

Pia upande wake wa mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sheikh Abeid Aman Karume, na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani.

Vilevile, ina alama maalumu ya usalama iitwayo “latent image”, iliyopo upande wa nyuma, ambayo ni kivuli kilichojificha, ambacho huonesha thamani ya sarafu “500” au neno BoT inapogeuzwageuzwa.