Tuesday, April 30, 2013

‘Siyo ajabu mtu wa nje kuajiriwa hapa’

Serikali imesema hakuna shida na wala sio ajabu kuajiri watu kutoka nje ya nchi hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo ambaye alisema hakuna shida vijana kutoka Kenya kufanya kazi Tanzania katika sekta mbalimbali.
Mulugo alisema kuwa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unatoa nafasi ya watu kutoka nchi moja na kwenda nchi nyingine na kufanya kazi wakiwamo Watanzania kuwapokea wageni kutoka nje na Vijana wa Tanzania kwenda nchi nyingine.
Alikuwa akijibu swali la Christowaja Mtinda (Viti Maalumu-Chadema), ambaye alitaka kujua Tanzania ina mkakati gani wa makusudi katika kuwaandaa Vijana wake kielimu ili waweze kushindana katika soko la ajira la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mbunge huyo pia alihoji ni kwa nini Serikali inatoa kipaumbele kwa Vijana wanaosoma masomo ya Sayansi pekee na kuyasahau masomo mengine yakiwamo ya masuala ya uhasibu.
Naibu Waziri alisema kuwa Serikali inatekeleza mikakati katika ngazi zote za kielimu ya kuwaandaa vijana wa kitanzania ili waweze kushindana katika soko la ajira la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alitaja baadhi ya mikakati ni kuvijengea uwezo Vyuo vya Ufundi ili viweze kuzalisha wataalamu ambao watakuwa na uwezo wa kitaaluma na kitaalamu wa kuingia kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Mulugo aliwashukuru wabunge wanaofuatilia mambo bungeni.
Aliwasihi wabunge kushirikiana na Serikali katika mipango yake ya kuboresha vyuo vya ufundi na kwamba lengo ni kuhakikisha vijana wengi wanakuwa na elimu hiyo na kuweza kujiajiri.

Chanzo:Mwananchi

No comments: