Tuesday, April 30, 2013

Mbunge aishauri Serikali kuivunjavunja Tanesco

Mbunge wa Kilwa Kaskazini kupitia CCM, Murtaza Mangungu ameshauri Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), livunjwe ili kutoa nafasi kwa mashirika mengine yatakayoweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mangungu ameitaka Serikali kutamka kama inaweza kuivunja Tanesco au kuipa mtaji ili ijiendeshe yenyewe.
Katika swali la msingi Mangungu alihoji Serikali kushindwa kutekeleza agizo la Rais katika kupeleka umeme maeneo ya Banduka, Mtandago, Miteja, Sinza, Puyu, Matandu na Njenga ambayo hayapati umeme licha ya umeme huo kupita katika maeneo hayo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene alisema masuala ya kuivunja Tanesco au kuiboresha yanategemea maoni ya wadau ambayo yalikusanywa ndani na nje ya nchi ambayo bado yanachambuliwa.
Alisema ahadi ya Rais imeanza kutekelezwa ambapo baadhi ya maeneo ya Somanga Fungu yana umeme na wateja 200 wameunganishwa.
Simbachawene alieleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi mdogo ambapo inatarajia kuunganisha wateja wengine 50 wakati wowote.
Alisema, katika mradi huo tayari nguzo 60 zimetengwa na tayari nguzo 40 zimeshasimamishwa huku Wizara ikifungua milango kwa wananchi kuanza kutuma maombi ya kuunganishiwa umeme.

No comments: